Maalim Seif Awasha moto.
Katibu  Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amewasha moto upya visiwani Zanzibar kwa kuwahimiza wananchi kufanya vitendo vinavyoonyesha kuikataa serikali inyoongozwa na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein

Maalim aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na watendaji na viongozi wa CUF kutoka Wilaya ya Micheweni katika Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tano hapa.
 
‘Tukikazana, serikali hii itaondoka, ikiwa mnangoja Maalim Seif au Marekani kuiondoa, kwa sheria ya kimataifa haitawezekana kwani Marekani haiwezi kuingilia mambo ya ndani ya Zanzibar,” aliongeza Maalim Seif, ambaye alijitoa kwenye uchaguzi wa marudio wa Zanzibar uliofanyika Machi 20, mwaka huu na Dk Ali Mohamed Shein kuibuka mshindi.
 
Uchaguzi wa marudio wa Zanzibar ulifanyika baada ya Tume ya Uchaguzi ya huko kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
 
Hata hivyo, Maalim Seif alisema Serikali ya CCM imeanza kutikisika kutokana na vikwazo vinavyoendelea kuwekwa na wahisani pamoja na hatua ya chama chake CUF kutowatambua viongozi wake pamoja na serikali.
 
“CCM wajue wamekalia kuti kavu, siku yoyote wataanguka...tufanye kazi mpaka haki yetu tuhakikishe imerudi na wenzetu hawana safari ya kudumu,” alisema Maalim Seif.
 
Aidha, aliwataka wanachama wa CUF kutumia mshikamano wao wa kuhakikisha wanafanikisha mpango wa kutoitambua Serikali ya CCM badala ya kuendelea kumsubiri yeye (Maalim Seif) au Marekani kuleta mabadiliko ya kiutawala visiwani humu.
 
Hata hivyo, Maalim Seif ameendelea kumshtumu Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kwamba ndiye chimbuko la kufutwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar.
 
"Baada ya Kikwete kupokea taarifa za CCM kushindwa Zanzibar, ndipo mipango ya kuvuruga matokeo ilipoanza kutekelezwa kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama," alidai.
 
Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu wa Zanzibar, alisema Kikwete alichukua hatua za kumtaka Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kusitisha mara moja kazi ya kutangaza matokeo ya uchaguzi huo.
 
Alisema wakati wajumbe wa ZEC wanaendelea kumsubiri ukumbini Mwenyekiti Jecha Salim Jecha, kuendelea kutangaza, alitoweka na baadaye kuibuka kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa Oktoba, mwaka jana bila kuwashirikisha viongozi wenzake wa Zec kinyume cha Katiba na sheria.
 
Maalim Seif alisema katika mkasa huo, Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Abdulhakim Ameir Issa, alikamatwa na kushindwa kuendelea kutangaza matokeo ya wagombea urais katika uchaguzi huo.
 
Alisema kitendo alichofanya Kikwete hakikubaliki katika misingi ya demokrasia na utawala bora ni sawa na kufanya mapinduzi ya utawala.
 
Maalim Seif alisema kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, hakuna kifungu kinachompa uwezo Mwenyekiti wa ZEC kufuta matokeo ya uchaguzi ambao tayari umeaisha kamilika.
 
Alisema Sheria ya Uchaguzi na Katiba ya Zanzibar imewapa haki wabunge, wawakilishi pamoja na madiwani kwenda mahakamani kama hawakuridhika na mchakato wa uchaguzi.

“Zanzibar hakuna kifungu cha Katiba au sheria kinachoruhusu kurudiwa uchaguzi na uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana ulikuwa huru na wa haki kwa mujibu wa ripoti za waangalizi wa uchaguzi wakiwamo Umoja wa Ulaya Marekani na Uingereza,” alisema Maalim Seif.
 
Aidha, alisema Mataifa ya Ulaya zikiwamo Marekani, Uingereza, Norway pamoja na Umoja wa Ulaya, yameanza kuchukua hatua za kuinyima misaada ya maendeleo Tanzania ikiwamo Zanzibar kutokana na mgogoro wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
 
Alisema wahisani hao pamoja na Shirika la Changamoto la Milenia (MCC) wamesema hawatotoa msaada mpaka suala la uchaguzi la Zanzibar likae sawa na kupatiwa muafaka wake.
 
Maalim Seif aliwataka wanachama wake kuonyesha kwa vitendo vya kweli vya kutoitambua serikali ikiwamo kukataa kulipishwa kodi za ovyo vyo pamoja na kujitenga na viongozi wa serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Mfano tunaweza kuamua siku flani kuanzia saa sita, tunasimamisha vyombo vyote vya usafiri na siku nyingine tunaamua kupiga honi Zanzibar nzima kuonyesha hatuitaki serikali ya CCM" Alisema Maalim Seif huku akishangiliwa na umati uliofurika katika ofisi za chama hicho.

"Wanasema ukitaka kumshinda adui unampiga akiwa dhaifu na udhaifu wao hawana fedha, na ili kuwadhibiti ni kuwanyima fedha na kuwachokoza kwa kuwaita majina mabaya kama dikteta, Nduli," alisema. 
 
Kuhusu suala la wakulima kuuzia serikali karafuu au kutoiuzia, alisema wananchi wenyewe ndiyo watakaoamua, lakini lengo la CUF ni kuona Serikali ya CCM inashindwa kuongoza Zanzibar kabla ya kumalizika miaka mitano.
 
Kwa mujibu wa Maalim Seif, tayari hali mbaya ya kiuchumi imeanza kujitokeza Zanzibar kutokana na bajeti ya mwaka huu kupoteza miradi mingi ya maendeleo kwa ufinyu wa fedha.
 
Kuhusu vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu, Maalim Seif alisema tayari yupo mwanasheria mzalendo ambaye ameanza kukusanya vielelezo mbalimbali kabla ya kufungua kesi katika Mahakama ya Kimataifa dhidi ya viongozi wenye dhamana ya kusimamia vyombo vya ulinzi na usalama wa raia.
 
Alisema tayari Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Muungano, wamepewa notisi ya kuarifiwa kufunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa kutokana na vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu uliofanyika Zanzibar.
 
Alisema kwa sasa wanasheria wanapitia sheria kwa umakini za kuanzishwa kwa mahakama hiyo ya kimataifa ili kuangalia uwezekano wa serikali ya Zanzibar kufunguliwa mashtaka katika mahakama hiyo.

Wakati wa ziara hiyo, Maalim Seif alipata wakati mgumu kutokana na barabara kufungwa na wafuasi wake wakimtaka atoe kauli juu ya hali ya kisiasa ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment