JUSSA: awanasihi vijana kujifunza kutoka kwa wazee

Ismail Jussa na Maalim Seif Sharif Hamad (pichani mwaka 1993) nyumbani kwa Maalim Seif, Mtoni Unguja.

NASAHA NJEMA KWA VIJANA WETU
Ismail Jussa

Nimeraghibika kuitumia picha hii leo kuwapa nasaha vijana wanaochipukia kupenda siasa na ambao wanadhihirisha uzalendo mkubwa kwa nchi yetu Zanzibar kwamba wasome na kukaa na wazee wenye hazina ya maarifa na historia ili waweze kuijua zaidi Zanzibar na pia kuongeza maarifa yao katika siasa na historia.


Picha hii ilikuwa ni katika mwaka 1993 nikiwa na Maalim Seif Sharif Hamad nyumbani kwake Mtoni, Zanzibar. Wakati huo Maalim Seif alikuwa ni Makamu Mwenyekiti wa CUF na mimi nilikuwa Katibu (Private Secretary) wa Katibu Mkuu wa CUF Marehemu Shaaban Khamis Mloo.

Tokea nikiwa mwanafunzi nilikuwa napenda kujifunza sana mambo yanayohusu siasa na historia. Kutokana na kupenda huko kujifunza nilikuwa na kawaida ya kukaa sana na watu walioshiriki harakati za siasa Zanzibar na pia kusoma vitabu na maandishi mbali mbali yanayohusu siasa na historia. Nashukuru nimechota mengi kwao.

Ni kwa sababu hiyo niliitumia kikamilifu miaka ya mwanzo mwanzo wakati CUF inaundwa kukaa na kuzungumza na kumuuliza maswali mbali mbali Maalim Seif na kupitia mazungumzo kama hayo nilijifunza mengi sana.

Nilikuwa na kawaida ya kumtembelea Maalim nyumbani kwake Mtoni jioni baada ya saa za kazi na huko kulikuwa na barza ya mazungumzo ya siasa ambapo kwa aliyetaka kujifunza aliyapata mengi.

Watu wengine ambao nilipata bahati ya kukaa nao, kuzungumza nao na kuchota mengi kwao ni pamoja na Mzee Ali Haji Pandu, Mzee Shaaban Khamis Mloo (Marehemu), Mzee Mkubwa Makame (Marehemu), Mzee Said Salim Baes (Marehemu), Maalim Juma Ngwali (Marehemu), Maalim Masoud Omar Said (Marehemu), Mzee Machano Khamis Ali, Juma Othman Juma, Hamad Rashid Mohamed, Khatib Hassan Khatib, Maalim Soud Yussuf Mgeni (Marehemu), Dk. Maulidi Makame Abdallah (Marehemu), na Bwana Juma Haji wa Mchangani (Marehemu).

Katika vipindi tofauti nimepata pia fursa za pekee na bahati kubwa kukaa na kujifunza kutoka kwa watu kama Sheikh Ali Muhsin Barwani (Marehemu), Maalim Salim Kombo Saleh (Marehemu), Sheikh Suleiman Sultan Malik (Marehemu), Sheikh Salim Masoud Riyami (Marehemu), Sheikh Issa Nasser Issa Al-Ismaily, Mzee Mohamedali Karim Jinnah wa Masomo Bookshop (Marehemu), Bwana Ali Nabwa (Marehemu), Bi Inaya Himid Yahya (Marehemu), Maalim Mohamed Idris (Marehemu), Prof. Ibrahim Lipumba, Prof. Haroub Othman (Marehemu), Sheikh Ahmed Badawi Qullatein (Marehemu), Prof. Abdul Sheriff, Maalim Salim Mzee, Ali Ameir Mohamed, Mzee Hassan Nassor Moyo, Sheikh Salim Said Rashid, Dk. Salim Ahmed Salim, na sasa Dr. Amani Karume.

Bila shaka wapo na wengi wengine ambao nimejichanganya na kujumuika nao kwa muda mfupi mfupi na kufaidika na hazina na maarifa yao lakini hao niliowataja hapo juu ni katika waliosarif mawazo yangu na mitazamo yangu kuhusiana na mengi yanayohusu siasa na historia ya Zanzibar.

Moja ambalo litabainika ni kwamba nimekaa na kujumuika na kuzungumza na watu wa mirengo tofauti ya siasa za Zanzibar (ASP, ZNP, ZPPP, Umma Party na ambao hawakujitambulisha na vyama vya siasa) na hilo limenifundisha kusikiliza mitazamo inayokinzana na kisha kuchambua na kupima mwenyewe yale niliyoyasikia huku nikifanya rejea kwenye vyanzo vyengine vya khabari kama vitabu na maandiko mengine mbali mbali.

Nawaombea kheri wote walionipa na wanaoendelea kunipa fursa kama hizi na wale waliokwisha tangulia mbele ya haki Mwenyezi Mungu Awalaze mahala pema Peponi. Amin.

Nawahimiza vijana wa kizazi cha leo watumie fursa zilizopo kukaa na wazee na watapata mengi kutoka kwao yatakayowasaidia kupanua ufahamu wao wa mambo.
Ukiona vyaelea, vimeundwa

By: Ismail Jussa
Picha imenikumbusha mbali, nakumbuka wakati huo, pamoja na Jussa na ‘Cameraman’ wetu Hamiyar, tulikuwa tunakwenda Mtoni, kumfanyia ‘Interview’ Maalim Seif, kama njia moja ya kujenga chama..

No comments:

Post a Comment