Maruhani hawakupindua Zanzibar

Ahmed Rajab
Toleo la 233
4 Apr 2012
SINA tabia ya kusutana, kubishana au hata kujibizana na wasomaji wa makala zangu wenye kutoa maoni tofauti na yangu. Ninaamini kwamba kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yoyote ayatakayo hasa pale maoni hayo yanapokuwa ni ya ufafanuzi au uchanganuzi wa matukio ya kihistoria.
Kufanya ufafanuzi lakini ni tofauti na kuuelezea ukweli hasa ule ukweli wenye kuhusika na tendo ama vitendo fulani.
Nimekuwa nikisubiri kwa shauku kubwa hitimisho la makala za mwandishi mwenzangu wa Raia MwemaJoseph Mihangwa kumhusu John Okello.  Mfululizo huo wake wa makala zake kuhusu Okello na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ulikuwa ni majibu ya maandiko yangu juu ya mada ya Okello. Kwenye sahafu (safu) ya leo nataka kuyajibu baadhi ya yaliyomo kwenye majibu yake.
Kuna baadhi ya Wazanzibari wanaoona kwamba hakuna faida yoyote kujadili yaliyopita hasa sasa wakati wa mchakato wa Katiba mpya. Lakini wanakosea kwani tunaposonga mbele ni lazima tujue si tu hapa tulipo lakini pia tulikotoka. La sivyo tutajikuta tunajikwaa kila tunapopiga hatua.
Kuna tatizo kubwa kumtathmini Okello na dhima yake katika Mapinduzi ya Zanzibar. Sababu yake ni kuwako kwa simulizi zenye kukinzana kuyahusu Mapinduzi hayo na walioshiriki kwenye matukio yaliyoanzia Januari 12, mwaka 1964.
Migongano ya simulizi hizo yanamfanya mtu afikirie kwamba labda mapinduzi hayo yalifanywa na maruhani na kisha ndipo wanaadamu nao wakaingia. Ndio maana wengine chambilecho Sheikh Thabit Kombo, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Afro-Shirazi Party (ASP), wanaifikiria historia ya Zanzibar yote kuwa ni uongo mtupu. 
Lazima niseme hapa kwamba baadhi ya wanaotoa simulizi mbadala huwa hawana nia njema na Zanzibar. Simulizi zao huupotosha ukweli ili ziweze kuwa na mishiko. Mihangwa si miongoni mwao.  Yeye ni mwandishi mahiri mwenye kuandika baada ya kuridhika kuwa amefanya uchunguzi wa kina kuhusu mada inayohusika.
Nimekuwa nikiyafuatilia maandishi yake kuhusu Zanzibar kwa muda mrefu na kwa maoni yangu huyu ni mwandishi mwenye kutupenda laisa kiasi sisi wazawa wa Zanzibar. 
Lakini kwa vile yeye si mzaliwa wa Zanzibar na wala hajakuwako Visiwani (hasa Unguja) wakati wa Mapinduzi kwa kiwango kikubwa amekuwa akiwategemea wengine kwa masimulizi yake.  Pingine hao ndio waliompotosha.
Sitothubutu kusema kwamba ubara wake umeugubika utaalamu wake kwa sababu hakuteleza kuyaeleza ya Zanzibar tu kama alivyomuelezea Othman Sharif kuwa alikuwa Mkomunisti wakati bwana huyo akijulikana kwa chuki zake dhidi ya wenye siasa za mrengo wa kushoto.
Mihangwa ameteleza kwa mengine pia.  Kwa mfano, amemuelezea Idi Amin kuwa ni Mlangi, mtu wa kabila la Lango, ilhali tunajua kwamba alikuwa Mnubi wa kabila la Kakwa.
Tukiliacha hili la Okello, ambalo hakika Mihangwa halielewi, maandishi yake mengine kuhusu Zanzibar hayakirihishi kama ya wenzake wengi wa Bara. Mara kadha wa kadha kabla ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa huko Zanzibar alikuwa akiwavua nguo watawala wa Visiwani kwa kufuata kisiri siri sera za kibaguzi zilizopitishwa na Mkutano Mkuu wa ASP mwaka 1973 kule Pemba.
Kwa kiwango Fulani Mihangwa amesaidia kuwaelimisha Wabara wenzake kuhusu mgongano wa maneno na vitendo vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Juu ya hayo lazima tumkumbushe Mihangwa kwamba Che Guevara, mzawa wa Argentina, hakwenda Cuba kama mfanyakazi mhamiaji kama alivyokuwa Okello.   Che alikuwa msomi aliyeshirikiana na akina Fidel Castro, Raul Castro, Camilo Cianfuegos na Wacuba wengine waliokuwa uhamishoni kwenda Cuba kwa dhamira thabiti ya kufanya Mapinduzi ya kuikomboa nchi hiyo kutokana na udikteta wa Batista.
Wala Che hakuwahi kujaribu kudai na kupora haki ya kutawala na uongozi kama alivyofanya Okello  Zanzibar. Wacuba walimtunuku Che nyadhifa za uongozi  kwenye serikali yao mpya kwa ridhaa yao na kwa heshima kubwa. Walimfanyia hayo kwa vile walitambua mchango wake adhimu kwenye Mapinduzi yao.
Kiashiria kingine cha mapenzi ya Wacuba kwa Che ni pale Wacuba walipokwenda Bolivia alikouawa Che na kulisaka kaburi lake na kisha kuirejesha Cuba maiti yake kwa mazishi ya kitaifa.  Kumfananisha Che na Okello ni kumtukana Che bila ya kiasi.
Okello alionyesha chuki kubwa kwa Wazanzibari na kujisifu kwa kuwaua wengi mbali na kujaribu kupora hatamu za utawala kutoka viongozi wa ASP. Ukweli ni kwamba Okello anafaa kulinganishwa na jamaa yake Joseph Kony wa Lords Resistance Army ya kule Uganda na sio kumweka pamoja na Major Ernesto ‘Che’ Guevara.
Laiti Okello angalikuwa hai basi yakini angelijiunga na LRA kwani ni muumini wa dini ya Ukristo uchwara wa kuendesha mauaji ya kikatili sawa na mhalifu Kony.
Okello mwenyewe alizidi kuipotosha historia pale alipolalama kuwa Waafrika wa Zanzibar wamemfukuza baada ya yeye kwenda Visiwani kuwasaidia kuwashinda Waarabu waliokuwa wakiwachinja. Hapo ndipo tatizo linapoanza na hicho ndicho kielelezo au kiashirio cha uzushi unaobatizwa kuwa ‘historia ya nyumbani’.
Kwenye makala yake ya mwisho juu ya kadhia ya Okello, Mihangwa amemalizia kwa kuibua maswali muhimu kuhusu uhasama mkubwa uliojitokeza upande wa baadhi ya wakuu wa ASP dhidi ya Makomredi, yaani wafuasi wa Abdulrahman Babu na chama cha Umma Party.
Hii ni mada nzito lakini lazima tuigusie. Hali ya kutoaminiana kati ya Makomredi na wakereketwa wa ASP imekuwepo wakati wote chini kwa chini tangu kilipoundwa chama cha Umma Party mwaka 1963.
Juu ya kuwepo hali hiyo ilibidi pia wakati ule pawepo na aina ya ushirikiano kati yao katika kukabiliana na wapinzani wao yaani vyama vya Zanzibar Nationalist Party na Zanzibar and Pemba Peoples’ Party.
Haja hiyo ndiyo iliyopelekea pawepo umoja uliovishirikisha vyama vya ASP na Umma, vyama vya wafanyakazi pamoja na Jumuiya ya Wanafunzi.
Kiini cha kuwepo hali hiyo ya kutoaminiana ni ule msimamo wa itikadi ya kikabila wa takriban viongozi wote wa ASP wa kuwaepuka kisiasa Wazanzibari wenye asili ya kiarabu sembuse waliotokana na damu ya Hizbu. Mtazamo huu wa aina ya ‘kikaburu’ ndio uliokuwa msimamo na unaendelea hivyo hadi leo kwa upande wa wahafidhina wa iliyokuwa ASP.
Wabara wasioitakia kheri Zanzibar wamekuwa wakiipalilia moto hali hii iliwaweze kuidhibiti Zanzibar kwa maslahi yao. Kwa hiyo dhana ya Umma Party ya kuyasuka Mapinduzi ili yawe na mtazamo wa kitabaka pekee badala ya ‘ugozi’ (ubaguzi wa kikabila na wa rangi) ilisambaratishwa muda wote tangu kuanzia miaka ya mwanzo ya mwongo wa 1960 na akina Othman Sharif, Jamal Ramadhan Nasib na Mdungi Usi.
Baadaye usambaratishaji huo uliendelezwa na wanapinduzi kina Seif Bakari, Abdalla Said Natepe na kaumu yote ya ile ijulikanayo kama ‘Kamati ya Watu 14.’ Hao ndio waliomshinikiza Sheikh Karume kutowashirikisha Makomredi kwenye uongozi wa nchi.
Siku zote walikuwa wakimtisha Mzee Karume kuwa Makomredi walikuwa na njama na jamaa zao Wakiarabu za kuutokomeza utawala wa Waafrika. Hatimaye walifaulu pale Karume alipowatimua kutoka kwenye serikali kina Badawi Qullateinna Ali Sultan na kubwa lao Babu kudondoshwa na Julius Nyerere.
Kuna siku ambapo Brigadia Yusuf Himidi aliwasikitia baadhi ya wafuasi wa Umma Party waliokuwa naye kwa kuwaambia: “Eh jamaa fitna nyingi zimepita kutugombanisha.” Hakumtaja mtu lakini ilikuwa wazi kwamba mafatani walikuwa baadhi ya wahafidhina wa ASP.
Tatizo kubwa la Zanzibar ni kwa Wazanzibari kukubali kuhadaiwa na wanasiasa uchwara kuendelea kuwa wafungwa wa historia ya kisiasa iliyoigawa jamii katika makundi ya kikabila na kinasaba.
Jukumu linalotukabili sasa ni namna ya kutafuta njia za kuuyayusha urathi huu muovu unaoigawa jamii ya Wazanzibari na unaoutia sumu ufahamu au utambuzi wa pamoja wa Wazanzibari.
Okello alifurushwa Zanzibar kwa sababu alikuwa akileta matatizo. Alikuwa ni adha lakini hakuwa kitisho cha kisiasa. Angelikuwa ni  kitisho cha kisiasa basi isingekuwa rahisi kumng’oa nchini kama alivyotolewa.
Wala si peke yake kati ya wageni waliokuwa wakifanya fujo aliyefukuzwa Zanzibar. Mwengine alikuwa Engine kutoka Kenya.  Naye pia alitimuliwa baada ya kukamatwa huko Maruhubi, kwa amri ya Sheikh Karume, na kikundi cha Makomredi wakiongozwa na Ali Mshangama.
Mwengine aliyekuwa akiitwa Mfarinyaki alikamatwa Chwaka na Komredi Hamed Hilal aliyempeleka gerezani Kiinua Miguu.  Amri za kukamatwa Mfarinyaki aliitoa Yusuf Himidi akiwa mkuu wa jeshi.  Kwa nini hajawahusisha wanajeshi wengine na wapinduzi wa ASP, haijulikani.  Labda Yusuf Himidi alikwishang’amua kwamba wenzake walikosa nidhamu, wakijihusisha zaidi na wizi wa ngawira, wakati Makomredi walikuwa na nidhamu ya hali ya juu.
Hatujui pia kwa nini Karume alihiyari kuwatumia Makomredi kuwatimua akina Okello, Engine na wapinduzi wengine waliokuwa si wenyeji wa Zanzibar.
Yumkini Karume aliamua kuwatumia Makomredi kumfukuza Okello badala ya kuwahusisha akina Said Washoto, Mohamed Abdalla Kaujore, Seif Bakari, Khamis Darwesh na wengine wa Kamati ya Watu 14 kwa sababu alihisi wangelisitasita na pengine kuibua mgogoro. Said Abdallah Natepe aliwahi kuhadithia kwamba waliwahi kumjadili Okello miongoni mwao na hata pakatolewa wazo la kumuua. 
Sheikh Aboud Jumbe amekiri kwenye kitabu chake ‘The Part-nership’ kuwa alikuwa hawajui na hakupata kuwaona baadhi ya waliokuwemo kwenye  Kamati ya Watu 14, wakiwa pamoja na Okello.
Nakiri kwamba ni taabu kuamini ya kuwa Okello aliibuka ghafla Raha Leo kutoka halaiki ya watu waliokuwa wamekusanyika hapo.  Lakini pia tuna uhakika kwamba  Okello hakuwa na uwezo wala heshima anayobandikwa nayo na Mihangwa. 
Hatusemi hivi kwa sababu Okello hakuwa Mzanzibari.  Tunasema hivi kwa sababu huo ni ukweli huku tukikubali kwamba kuna haja ya kuiangalia upya nafasi yake Okello katika mchakato mzima wa maandalizi ya Mapinduzi.
Nimalizie kwa kukumbusha jingine.  Nalo ni kwamba kadhia niliyoieleza ya kutimuliwa Okello kutoka Zanzibar haikuwa ya mwanzo ya kufukuzwa Okello.  Mara ya kwanza alifukuziwa kutoka uwanja wa ndege wa Dar es Salaam na kusindikizwa hadi Nairobi na Oscar Kambona, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanganyika.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/maruhani-hawakupindua-zanzibar#sthash.0FaflFge.dpuf
Ahmed Rajab
Toleo la 233
4 Apr 201
Ahmed Rajab
Toleo la 233
4 Apr 201
Ahmed Rajab
Toleo la 233
4 Apr 201
Ahmed Rajab
Toleo la 233
4 Apr 201

No comments:

Post a Comment