UONGOZI WA CHAMA CHA CUF

The Civic United Front (CUF- Chama cha Wananchi). CUF ni chama cha uliberali wa kidemokrasia ambacho kauli mbiu yake ni Haki Sawa kwa Wote. CUF inasimamia elimu bora, afya madhubuti, mfumo adilifu wa kodi, Muungano wa haki, siasa kuwa utumishi ulioutukuka kwa umma na fursa sawa katika kujiendeleza kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba
Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba
HAKI SAWA KWA WOTE
Kaulimbiu ya Haki Sawa kwa Wote inalenga visheni ya CUF ya jamii tuitakayo. Hiyo ni jamii yenye wananchi wanaopendana, kuheshimiana, kuhurumiana, na wanaochukia uonevu, ukandamizaji na ubaguzi. Msingi Mkuu wa CUF ni haki za binaadamu na demokrasia na hivyo suala la usawa lina nafasi ya pekee katika kuijenga jamii inayokusudiwa na Chama chetu.
Azma ni kujenga jamii ambayo itahakikisha inapiga vita ubaguzi wa kila aina na ambayo itahakikisha kila mwananchi anathaminiwa utu wake, na ana haki na fursa sawa katika nyanja zote za maisha yake.
Lengo ni kujenga jamii ya demokrasia ya kweli na yenye kuongozwa na utawala wa sheria na Serikali nzuri (good governance), ambayo msingi wake ni kuwekwa madarakani na wananchi wenyewe.
Shabaha, Malengo na Madhumuni makuu ya CUF yameelezwa kwa urefu katika Katiba yake. Lakini kwa ufupi Shabaha kuu ya CUF ni kuona kwamba nchi yetu na wananchi wake wote wamepata uhuru wa kweli na kujigomboa na mapepe yaliyobaki baada ya ukoloni mkongwe kuondoka na, pia, kujikinga na athari za ukoloni mamboleo. CUF inakusudia kuhakikisha kwamba uwezo wa kuiongoza nchi na wa kutoa maamuzi mazito ya mambo makubwa ya Taifa uko mikononi mwa Watanzania wenyewe.
CUF siku zote itaongoza juhudi za wananchi zenye kuelekezwa katika kuiletea nchi yetu ukombozi wa kiuchumi. CUF itatilia maanani umuhimu wa rasilmali za nchi yetu kuwanufaisha wananchi wenyewe. Katika kufikia lengo hilo CUF itakuwa na uangalifu mkubwa katika kuwashirikisha wageni wenye uwezo wa fedha na teknolojia. Wimbo wa Taifa wa CUF unasema hivi:
Ni haki sawa kwa watu wote, kuendeleza taifa letuUtajirisho itikadi yetu, tukatae kuonewa.Siasa itumikie, uchumi wa Nchi yetuNi mwiko huo uchumi, kutumikia siasa
Wimbo huu unabeba mantiki nzima ya itikadi, falsafa na sera za CUF.
ITIKADI YA ULIBERALI
Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji
Makamu Mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji
Itikadi kuu ya Chama cha Wananchi (CUF) ni Uliberali ambayo inalenga kuwazindua wananchi waweze kuitumia neema waliyopewa na Mwenyezi Mungu kwa manufaa yao binafsi na Taifa kwa ujumla. CUF inaamini kuwa Tanzania ni nchi tajiri kwa rasilimali na watu, lakini imefanywa kuwa masikini kwa kukoseshwa uongozi wenye sera na mtazamo (dira) wa kimaendeleo.
Inaposema Tanzania ina neema, CUF inakusudia uwezo wa akili na nguvu pamoja na utajiri wa asili tulinao. Nchi hii inao utajiri mkubwa wa ardhi ifaayo kwa kuzalisha mazao ya aina mbalimbali na inao utajiri mkubwa wa maji ya mito maziwa na bahari.
Itikadi ya Utajirisho inamhamasisha mwananchi ili aweze kuutumia ipasavyo utajiri wetu wa ardhi, bahari na madini ya thamani kama dhahabu, almasi, gesi, na tanzanite.
Kuhusu siasa, CUF kinasimama kama chama halisi na makini cha kisiasa kinachotumia siasa kwa maana yake halisi kufanya siasa kufikia malengo na dhamira yake kwa njia za kisiasa. CUF inasisitiza kuwa siasa si mchezo mchafu, ingawa inafahamu kwamba CCM imezifanya siasa zionekane hivyo kutokana na viongozi wake kuiharibu siasa kutokana na ulaghai wao kwa Watanzania. Kwa hivyo, mwelekeo wa siasa ya Chama Cha Wananchi ni kuwaelimisha na kuwaandaa wana-CUF na Watanzania wote katika kutoa utumishi wa kuridhisha kwa wananchi ili kurudisha hadhi na heshima ya siasa kama utumishi uliotukuka kwa umma.
Kuhusu mamlaka ya dola, CUF inaamini kwamba Serikali ndiyo dola na kwamba mamlaka yake yanapatikana kutokana na ridhaa ya wananchi kwa kufanyika uchaguzi ulio halali na huru na Serikali hiyo lazima iweajibike huko huko kwa wananchi. Kwa mujibu wa Itikadi hii, Serikali itakayoundwa na CUF lazima iwajibike kwa wananchi. Ndani ya Serikali ya CUF, kwa hivyo, hakutokuwa na nafasi ya walaghai wachache kuendesha mambo kwa ujanja, ufisadi na utapeli kama ambao umekuwa ukitekelezwa na viongozi wa serikali za CCM.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kwenye uchumi na maendeleo, CUF inakusudia kujenga uchumi ulio imara kwa kuanzisha taratibu za kiuchumi zainazowashawishi kwa kadiri ya uwezo wao na kuchangia Taifa kwa ziada wapatayo. Mtazamo wa CUF kijumla ni wa kiliberali, kwa hivyo uhuru wa mtu binafsi kujiendeleza na kutumia fursa zilizopo kujinufaisha na kulinufaisha Taifa.
Kuhusu ardhi, CUF inachukulia kuwa ni mali ya watu wote, hivyo Serikali ya CUF itasimamia matumizi yake kwa uangalifu mkubwa. Ardhi itamilikiwa na wananchi wenyewe au Serikali yao. Kwa hivyo, ingawa CUF inakaribisha uwekezaji rasilimali kutoka nje, lakini Serikali yake haitomilikisha ardhi kwa wageni. Iwapo mwekezaji anahitaji ardhi kwa ujenzi wa kiwanda, kuendesha shughuli za kilimo au kuendeshea shughuli nyinginezo, mwekezaji huyo atawajibika kuingia ubia na mwananchi ambaye ndie atakayemilikishwa ardhi inayohitajika.
Kuhusu elimu, CUF imekusudia kutoa elimu ya darasa la kwanza hadi la kumi na mbili bure katika mashule yenye vifaa na walimu wenye sifa ya kufanya kazi hiyo wala sio katika hali ya sasa ambapo shule zilizopo hazina vifaa vya kutosha wala walimu wenye sifa hasa za kuwa walimu. CUF inaamini kwa elimu ndio msingi wa ujenzi wa taifa na kwamba taifa lisilo na watu walioelimika haliwezi kwenda mbele. Kusoma na kuelimika ni haki ya kila mwananchi na CUF inakusudia kuilinda na kuigawa haki hiyo kwa wenyewe, wananchi.
Kama ilivyo elimu, CUF inaamini kuwa afya nayo ni haki ya msingi ya kibinaadamu. Kwa hivyo, inakusudia kuboresha huduma za kinga pamoja na zile za tiba. Katika kulifanikisha hili, CUF itahakikisha kuwa mahospitali yaliyopo yanapatiwa vifaa bora pamoja na kuzingatia mafunzo kwa wafanyakazi.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), Magdalena Sakaya.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), Magdalena Sakaya.
Kwenye nyanja ya wafanyakazi, Serikali ya CUF inakusudia kupanga pato la mfanyakazi kwa saa wala sio kwa mwezi. Utaratibu huu ni wenye manufaa kwa pande zote mbili, wakati mfanyakazi anajitahidi kufanyakazi kwa masaa mengi ili ajipatie donge nono, mwajiri ananufaika kwa kulipa kulingana na kazi iliyofanywa.
Kuhusu umeme na maji, CUF inasisitiza kuwa kulingana na umuhimu wa huduma hizi kwa uhai na uchumi, Serikali yake itahakikisha kuwa wananchi wanapatiwa maji pale walipo na kunakuwepo umeme wa uhakika katika sehemu zote zilizokubalika kupata huduma hiyo.
Kwenye ushuru, Serikali ya CUF itahakikisha kwamba baadhi ya ushuru unaokusanywa na Serikali Kuu unahamishiwa Serikali za Mitaa na Serikali hizi zinakuwa bunifu.
Juu ya mabenki na huduma za fedha, Serikali ya CUF inakusudia kurekebisha mfumo wa uendeshaji wa Mabenki hapa nchini. Katika mabadiliko hayo, mabenki na taasisi nyingine za kifedha zitajiendesha kibiashara huku zikizingatia kutoa fursa ya kuwahudumia wananchi wote kwa kuondoa masharti yanayokwamisha wananchi wa kawaida kunufaika na huduma hiyo.
Kilimo kitapewa umuhimu mkubwa na wakulima wananchi watasaidiwa kuboresha njia zao za ukulima. Kwa sababu ardhi ndio rasilmali kuu ya nchi yetu basi ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba ardhi yetu inatumika vyema.
Hivyo watumiaji wote wa ardhi watashawishiwa na kuelimishwa juu ya matumizi bora ya ardhi ili ardhi itoe mazao bora na mengi na wakati huo huo kuwahakikishia wakulima bei nzuri za mazao yao ili zilingane na juhudi zao na ubora wa mazao yao. Nia ni kuwafanya wananchi wawe na maisha mazuri kutokama na rasilmali ya nchi na juhudi zao.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Mhe. Nassor Mazrui.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Mhe. Nassor Mazrui.
Sekta za viwanda na madini zitapewa mwelekeo mpya ambao utakidhi hali halisi na ambao utatawaliwa na matumizi sahihi ya sayansi na teknolojia na sekta hizi zitaongozwa na wataalamu waliofunzwa na kufunzika, zitapata usimamizi wa makini na zitafanywa ziweze kuzalisha bidhaa zinazokidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa ili bidhaa hizo ziweze kuuzika kwa urahisi.
Na kwenye suala la muhimu kwa uhai wa Taifa hili kama taifa, yaani Muungano, CUF inatambua umuhimu wa Muungano uliopo baina ya Tanganyika na Zanzibar bali inataka pawepo na Muungano wa ukweli unaozingatia maslahi ya wananchi wote.
Kwa mfano, kwa mujibu wa Makubaliano ya Muungano (Articles of Union), Rais wa Zanzibar anakuwa mmoja wa Makamo wawili wa Rais, na hivyo CUF inayachukulia Mabadiliko ya 11 ya Katiba ya Muungano kama ukiukwaji mkubwa wa Mkataba wa Muungano, na ambao unavunja misingi ya Muungano wenyewe. Sera ya CUF kuelekea Muundo wa Muungano ni Serikali Tatu, yaani ile ya Zanzibar, ya Tanganyika na nyengine ndogo ya Muungano.

Dira hii ya CUF inaweza kufanywa kuwa hai ikiwa kila Mtanzania ataungana na CUF kuihuisha. Jiunge sasa na ukombozi, saa ndiyo hii.

No comments:

Post a Comment