Mjue Maalim Seif Shariff Hamad

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF , Maalim Seif Sharif Hamad
Kwa Ufupi:

Maalim alihudhuria masomo ya shule ya msingi katika Shule ya Msingi Uondwe iliyoko Pemba na kisha akasoma shule ya wavulana ya Wete (Shule zote hizi za msingi amesoma katikati ya mwaka 1950 – 1957) kabla ya kujiunga na elimu ya Sekondari (Kidato cha kwanza hadi cha nne) kati ya mwaka 1958 – 1961 katika Shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Mfalme George, iliyoko katika Kisiwa cha Unguja, na pia akaendelea na kidato cha tano na sita katika sekondari hii kati ya mwaka 1962 -1963.



Historia yake
Maalim Seif Sharif Hamad ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar na pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF. Maalim Seif alizaliwa Oktoba 22, 1943 huko Nyali, Mtambwe katika Wilaya ya Wete iliyoko kisiwani Pemba.

Maalim alihudhuria masomo ya shule ya msingi katika Shule ya Msingi Uondwe iliyoko Pemba na kisha akasoma shule ya wavulana ya Wete (Shule zote hizi za msingi amesoma katikati ya mwaka 1950 – 1957) kabla ya kujiunga na elimu ya Sekondari (Kidato cha kwanza hadi cha nne) kati ya mwaka 1958 – 1961 katika Shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Mfalme George, iliyoko katika Kisiwa cha Unguja, na pia akaendelea na kidato cha tano na sita katika sekondari hii kati ya mwaka 1962 -1963.
Pamoja na kufaulu vizuri sana masomo ya kidato cha sita, Maalim Seif hakwenda chuo kikuu kwa sababu serikali ilimtaka afanye kazi serikalini ili kuziba nafasi za kazi zilizokuwa wazi kutokana na kuondoka kwa wingi kwa Waingereza kurudi nchini kwao. Maalim aliajiriwa kama mwalimu kwa miaka tisa, yaani 1964 – 1972 na alifundisha Sekondari Fidel Castro iliyoko Pemba na Chuo cha Ualimu cha Lumumba kilichoko Unguja.
Mwaka 1972 aliruhusiwa kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kusomea shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa, Usimamizi wa Umma na Uhusiano wa Kimataifa, alihitimu shahada hii mwaka 1975 akiwa mmoja wa wanafunzi waliofaulu vizuri sana kiasi kwamba chuo kilipenda abakie kufundisha, jambo ambalo hakukubaliana nalo.
Maalim Seif alianza kujifunza na hata kuingia katika masuala ya uongozi mkubwa wa serikali mwaka 1975, alipoteuliwa kuwa Msaidizi Binafsi wa Rais wa Zanzibar wakati huo (Aboud Jumbe) ambapo aliifanya kazi hiyo hadi mwaka 1977. Mwaka 1977 akateuliwa kuwa Waziri wa Elimu wa Zanzibar na akatumika katika nafasi hiyo hadi mwaka 1980.
Mwezi Februari 1984 akateuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Zanzibar (Cheo sawa na cha Waziri Mkuu wa Tanzania, kimajukumu). Maalim Seif amekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar katika kipindi chote cha uongozi wa Rais Mwinyi kama Rais wa Zanzibar, na mwaka 1985 alipochaguliwa Rais Idris Abdul Wakil kuongoza Zanzibar, bado Maalim Seif aliteuliwa kuwa Waziri Kiongozi na alishikilia wadhifa huo hadi Januari 1988 alipoondolewa katika baraza la mawaziri na baadaye kufukuzwa ndani ya CCM. Kwa hivyo, Maalim Seif amekuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar kuanzia mwaka 1977-1988.
Tokea Maalim Seif aondolewe katika utumishi wa uongozi wa juu wa Zanzibar (akiwa mwanachama wa CCM), imemchukua miaka zaidi ya 22 ndipo tena amerejea kileleni, sasa akiwa ni Makamu wa Kwanza Rais wa Zainzibar, lakini akitokea Chama Cha Wananchi CUF.
Kisiasa, Maalim Seif amepitia katika nafasi nyingi sana. Mwaka 1977 – 1988 alikuwa Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM lakini pia mwaka 1977 – 1987 alikuwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM huku mwaka 1982 – 1987 akiteuliwa kuongoza Idara ya Uchumi na Mipango ya Chama cha Mapinduzi (kitaifa).
Maalim Seif na wenzake kadhaa walifukuzwa kutoka Chama Cha Mapinduzi mwaka 1988 baada ya kushindana kimsimamo na CCM na alikuwa mmoja wa waanzilishi wa vuguvugu la “Kamahuru” la Zanzibar lililoungana na CCW (Chama Cha Wananchi) ya Tanzania Bara na kuunda Chama Cha Wananchi CUF ambapo yeye (Maalim Seif) alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kwanza wa CUF akihudumu katika wadhifa huo hadi mwaka 1999 alipochaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa CUF hadi hivi sasa.
Kimataifa, Maalim amewahi kushikilia wadhifa mkubwa sana kimataifa kati ya mwaka 1997 - 2001, alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu wa “The Unrepresented Nations and Peoples Organization (UNPO)” (Nchi zisizowakilishwa na Mashirika ya Watu) - Tafsiri yangu. Hii ni taasisi ambayo makao makuu yake yapo jijini The Hague nchini Uholanzi na inahusisha mataifa zaidi ya 50 duniani na watu ambao siyo wajumbe wa Umoja wa Mataifa, yaani ambao wakienda Umoja wa Mataifa wanakuwa na hadhi ya waangalizi tu (au wageni).

Baadhi ya nchi mwanachama wa umoja huu ni pamoja na Taiwan, Tibet na Zanzibar. Lakini pia amewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Vyama vya Kiliberali Duniani kati ya mwaka 2002 – 2003.
Maalim Seif amemuoa Aweina Sinani Masoud tangu mwaka 1977 na wana watoto watatu.
Mbio za ubunge
Maalim Seif si mgeni katika masuala ya uwakilishi na Ubunge. Yeye ni mmoja kati ya Watanzania wachache waliobahatika kupitia nafasi zote za kuwawakilisha wananchi kwa pande zote mbili za muungano.
Mwaka 1977 – 1982 amekuwa Mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia kati ya mwaka 1977- 1980 na 1984 – 1988 amekuwa ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Kwa muktadha huu anafahamu vizuri shughuli za kibunge na kiuwakilishi na amepata kuzishiriki vilivyo.
Mbio za urais
Maalim Seif, “Rais wa Mioyo ya Wazanzibari” ameshiriki katika mbio za urais za Zanzibar mara nne bila mafanikio, lakini zikiwa chaguzi ambazo hata waangalizi wa kimataifa wamekuwa bila kupepesa macho wakisisitiza kuwa zina walakini mkubwa.
Uchaguzi Mkuu wa Kwanza alioshiriki ni ule wa mwaka 1995 akigombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF. Maalim Seif alikosa kuingia ikulu kwa sababu “ilitangazwa” kuwa amepata asilimia 49.76 ya kura zote dhidi ya Rais Salmin Amour “Komandoo” aliyekuwa na asilimia 50.24. Pamoja na CUF kupinga matokeo hayo, pia Waangalizi wa kimataifa walisisitiza kuwa uchaguzi ule ulikuwa “uchafu”.
Mwaka 2000 tena Maalim Seif alitaka kuingia Ikulu lakini haikutokea. Ilitangazwa kuwa amepata asilimia 32.96 ya kura zote dhidi ya asilimia 67.04 za Amani Karume wa CCM. Huu ni uchaguzi ambao pia hata waangalizi wa kimataifa waliutaja kama moja ya chaguzi zisizofuata kabisa misingi ya kidemokrasia huku ukandamizaji wa vyama vya upinzani hususani CUF ukiwa wazi. Kwa mfano, waangalizi wa Jumuiya ya Madola waliutaja uchaguzi huu kama “Shambels” (Msambaratiko) – Tafsiri yangu.
Kwenye uchaguzi wa mwaka 2005, Maalim Seif aliangushwa kwa mara nyingine na Rais Amani Karume wa CCM, Safari hii Maalim akitangaziwa kupata asilimia 46.07 dhidi ya 53.18 za Karume. CUF ilikataa matokeo haya na ikatangaza kutomtambua Karume kama Rais wa Zanzibar. Waangalizi wa kimataifa kama Jumuiya ya Madola na Taasisi ya Demokrasia ya Marekani ziliweka wazi kuwa uchaguzi ule haukuwa huru na wa haki, baadhi ya maandiko yanasisitiza kuwa huwenda hii ndiyo sababu iliyofanya Marekani (kama nchi) isitume hata balozi wake au mwakilishi kushuhudia sherehe za kumwapisha Karume (mara ya pili).
Maalim Seif alitupa karata ya nne ya kusaka urais wa Zanzibar mwaka 2010 mara hii akipambana na Dk Ali Mohamed Shein ambapo pia Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilitangaza kuwa Dk Shein amemzidi Maalim Seif kwa kura 4471. Ndiyo kusema kuwa Maalim Seif alipata asilimia 49.1 dhidi ya asilimia 50.1 za Shein. Uchaguzi wa mwaka huo pia ulionekana kuwa na kasoro nyingi sana.
Kwa mwaka huu 2015 tayari Maalim Seif Sharif Hamad amekishachukua fomu na kupitishwa na CUF kuwa mgombea urais wa Zanzibar kwenye uchaguzi wa mwaka huu n CUF upande wa Zanzibar inaonekana imejipanga sana kushiriki kwenye uchaguzi mwaka huu, huwenda kuliko wakati wowote ule kama alivyowahi kuandika Ismail Jussa, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa chama hicho, kwenye ukurasa wake wa “Facebook”.
Nguvu yake
Kwanza, Maalim Seif ndiye kiongozi mwenye uzoefu mkubwa sana wa kisiasa kati ya viongozi wa upinzani, akianza utumishi wa juu kabisa serikalini alipokuwa kijana mdogo tu na ameendelea hadi kufikia nyadhifa za juu kabisa. Uzoefu wake ni silaha tosha kuwa ukimpa uongozi wa nchi wala hawezi kwenda kuanza kujifunza, tayari anajua wapi aanzie na kwa nini.
Lakini nguvu kubwa na sifa maalum ya Maalim Seif ni kuwa Msimamo thabiti na usioyumba. Kiongozi huyu ana misimamo yake juu ya baadhi ya masuala na ikifika hapo hawezi kuyumba. Mathalani, hivi karibuni amekuwa na msimamo wa dhati wa kudai mamlaka kamili ya Zanzibar, msimamo huu umekuwa ajenda kubwa sana katika siasa za Zanzibar na ni moja ya masuala ambayo. Lakini pia watu waliowahi kufanya naye kazi.
Katika siasa ukiwahi kupitia kifungo cha kisiasa, kunyanyaswa moja kwa moja na kuteswa kwa sababu ya msimamo wako kidemokrasia, jambo hili hugeuka na kuwa ushujaa. Maalim Seif alipofukuzwa CCM mwaka 1988 alikaa muda mfupi tu kabla ya kuanza kuwa mfungwa.

Alikamatwa mwezi Mei 1989 na kufikishwa mahakamani akishitakiwa kwa kukutwa na nyaraka za siri za serikali (mashtaka ya kupikwa). Alikaa gerezani kwa miaka mitatu (hadi mwaka 1991). Wananchi na marafiki wan chi yetu kimataifa walipoomba sana Maalim Seif na wenzake watolewe gerezani, Rais wa Zanzibar wakati huo, Salmin Amour “Komando”, aliwakebehi hadharani kuwa “wanapaswa kukaa huko huko, hawataoza kwa sababu wao siyo mapapai!”
Lakini pia mwaka 2000 alikamatwa tea na kupewa mashtaka ya kumshambulia askari polisi na kumyang’anya bunduki (kosa la kubambikizia pia). Shitaka hili lilitupwa na mahakama mwaka 2003. Maalim Seif ni mmoja wa viongozi wakubwa sana wa kisiasa hapa Tanzania ambaye amewahi kukaa gerezani muda mrefu sana. Jambo hili ni umadhubutu muhimu kwa mtu anayetaka kuongoza nchi. Kama ameweza kukaa gerezani kwa ajili ya demokrasia na akatoka akaendelea kuipigania, inamjenga katika sifa ya uvumilivu na kutokata tamaa.
Udhaifu wake
Kwanza, Maalim Seif amekuwa na uungwana uliopita kiasi katika mazingira ambayo Zanzibar inahitaji kufanya maamuzi magumu. Uungwana huu kisiasa unaweza kuwa na shida siku za mbele. Hivi karibuni, Mzee anayeheshimika sana Zanzibar na mtu wa karibu na Maalim Seif alitangaza hadharani kuwa mwaka 2010 “yeye Mzee Moyo ndiye alitumwa kwenda kumuomba Maalim Seif ayakubali matokeo ya uchaguzi”. Ndiyo kusema kuwa matokeo yale yalikuwa yamechakachuliwa na ilimpasa Maalim Seif ayakubali ili kuiepusha Zanzibar kuingia kwenye shari. Pamoja na mzee Moyo kurudia kauli hii mara kadhaa, Si Maalim Seif au CUF vimewahi kukanusha.
Kama hiyo hali ni ya kweli basi, tutegemee tena mwaka huu CCM itakuja na mpango huo huo wa kupora ushindi Zanzibar na kutegemea uungwana na huruma ya Maalim Seif. Hakika ifikie wakati Maalim Seif awaachie Wazanzibari wenyewe waamue hatma yao ikiwa wataendelea kufanyiwa ujanja kwenye masanduku ya kura. Uungwana wa namna hii unazika haki za kidemokrasia za wapiga kura na si jambo linalopaswa kujirudia tena na tena kwa kiongozi mkubwa.
Tulipokuwa katika Bunge Maalum la Katiba na nadhani waliokuwa wakifuatilia matangazo ya bunge hilo kupitia kwenye luninga walikuwa wakisikia kwa uwazi kabisa wajumbe wa BMK ambao ni viongozi wakubwa wa CCM kutoka Zanzibar wakitamka waziwazi kuwa hawawezi kuuachia Urais wa Zanzibar kwenye masanduku ya kura. Hii ina maana kuwa CCM itaendelea kupora ushindi wa kidemokrasia wa Wazanzibari kwa kutumia uungwana na busara za Maalim Seif. Jambo hili likiendelea litahesabiwa tena kama udhaifu mkubwa sana.
Nini kimefanya apitishwe
Jambo la kwanza lililofanya CUF impitishe kugombea urais ni kwa sababu yeye ni Mhimili wa siasa za Zanzibar kitaifa na kimataifa. Huwezi kutaja mustakabali wa Zanzibar na Wazanzibari bila kumtaja kiongozi huyu, amehusika katika sehemu kubwa za mabadiliko kadhaa tangu alipokuwa ndani ya CCM na hata alipohamia upinzani. Hali hii nadhani imeivutia CUF na kuona kuna haja ya kuendelea kumpa nafasi.
Lakini sababu ya pili nadhani ni kwa sababu amegombea Urais mara nne zilizopita huku ndiye pekee akionekana bado ana mvuto na ukubalikaji mkubwa zaidi kuliko mwanachama mwingine wa CUF. Hadi sasa CUF haina mgombea mwenye sifa, uwezo, uzoefu na umaarufu au umashuhuri kama wa Maalim Seif. Nadhani chama hicho kimempitisha kikitegemea kwamba yeye peke yake kwa sasa ndiye anaweza kuaminiwa sana na wananchi kiasi cha kuweza kupigiwa kura na kupata ushindi.
Nini kingeweza kumwangusha
Jambo moja ambalo lingemkwamisha Maalim Seif kuwa mgombea urais wa CUF upande wa Zanzibar ni ikiwa yeye mwenyewe angeamua kupumzika au kutogombea. Kwa hali ya kisiasa ya Zanzibar ilivyo “chanya” kwake, sikutegemea kuwa angeliweza kutopitishwa, na labda sana angetokea mwanachama mwingine wa CUF mwenye sifa, uwezo na vigezo kwa upande wa Zanzibar, ambaye hadi sasa sijamuona.
Mpango B kama asingepita
Mipango kama mitatu hivi inaweza kufuatwa na Maalim Seif ikiwa asingepitishwa kugombea urais;
Mpango wa kwanza ni Kuendelea na wadhifa wake wa kiserikali aliona sasa hivi pamoja na kuendelea na uongozi wa CUF ambao unapaswa kukamilika mwaka 2019. CUF bado inamhitaji kiongozi huyu na nadhani bado serikali ya Zanzibar inamhitaji zaidi kiutumishi.
Lakini jambo la pili ni uimarishaji wa maridhiano na utangamano wa Wazanzibari. 

Ikumbukwe kuwa Maalim Seif ni mmoja wa waasisi wawili wa Maridhiano ya sasa yanayoifanya Zanzibar iwe kwenye utulivu na amani ya sasa. Naamini kuwa angekuwa na jukumu la kujipanga kuanza kusimamia masuala ya utangamano wa Wazanzibari kwa vitendo, ikiwemo kuanzisha taasisi maalumu ambazo zingeendelea kufanya naye kazi kwa lengo la kuimarisha mustakabali wa Zanzibar.
Lakini lingine ambalo nadhani ni ajenda yake ya kudumu ni kupigania Zanzibar yenye mamlaka kamili. Ajenda hii naamini ingeendelea kuwa mikononi mwa Maalim Seif na wanachama wake kwa sababu imekuwa na “mashiko makubwa” na kwa wazanzibari wanaweza kuona kuwa inahitaji kuendelezwa na walioianzisha akiwemo yeye mwenyewe. Namuona akiipigania ajenda hii hata ikiwa atachaguliwa kuingia Ikulu.
Hitimisho
Vijana ambao hawakuwahi kufanya kazi na Maalim Seif wamekosa kujifunza uongozi thabiti kutoka kwa mtu ambaye anajua uongozi unafanywaje. Maalim Seif ni Mwalimu wa Siasa na Uongozi na anajua muda gani afanye nini ili kuendelea kuweka utulivu mahali anapoongoza.
Nakumbuka wakati anatangaza kumtambua tena Rais Karume, vikao vya chama vilitoa baraka za jambo hilo lakini vikiwa na hofu kubwa ya nini kitakachotokea. Maalim Seif aliihimili hali ile, akamtambua Karume, akatengeneza maridhiano na Wazanzibari wakamuelewa. Ni nadra sana kwa dunia ya sasa kupata viongozi wanaokubalika, kuheshimika na kuaminiwa na wafuasi wao, kama ilivyo kwa Maalim Seif.
Maalim Seif si mtu wa mambo makuu sana, mara nyingi utamkuta yumo mitaani kabisa akiwatembelea wagonjwa huku na kule, wazee na watu wasiojiweza. Staili yake ya uongozi ni ya kuamini kuwa watu wa chini wanahitaji msaada na faraja kubwa ya uongozi. Namna anavyosimamia ajenda muhimu ndani ya Zanzibar huku misimamo yake ikiwa wazi ni karata muhimu kwake kuzidi kuaminiwa na huwenda kukabidhiwa dola.
Mimi namtakia kila le heri kiongozi huyu, katika safari yake ya kurejesha hadhi ya Zanzibar na Wazanzibari wote kwa ujumla.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment