Makala ya Ally Saleh “CCM Zanzibar imeshindwa tena si kidogo”


Hii ni makala yangu iliyotoka gazeti la MTANZANIA

 Hapana chembe ya shaka kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 CCM ilishindwa. Tena si kushindwa kidogo imeshindwa kiasi ambacho hakuna wasiwasi wowote kwamba Chama cha Upinzani CUF ndio washindi wa dhahir.

Kwa kulinganisha takwimu zilotolewa katika vituo ambazo CUF ilifanya bidii ya ajabu kuzikusanya ambapo taarifa hizo zina matokeo ya vyama vyote, na CUF kuchukua bidii ya kukotoa, basi ni wazi kuwa CCM imeshindwa kwa karibu kura 25,000 na ushindi wa CUF ni lazima utambuliwe.

Lakini kwa bahati mbaya kwa kuendelea kuishi katika ndoto, kuishi katika sayari nyengine CCM iliona kuwa mara hii pia baada ya 1995,2000,2005 na 2010 kuwa pia mara hii itaweza kuiibia CUF, lakini CUF zamu hii waliweka mbele ule msemo kuwa kwenda ndio kupotea njia lakini kurudi ni kujua.

Mimi naamini ndani ya dhati ya moyo wangu kuwa CCM tayari wamekiri kushindwa.
Ambacho kimewaumiza bila shaka ni ile hatua ya CUF kuwahi kuweka matokeo yote hadharani na kwa hivyo kuondosha uwezekano wa kuchezea matokeo kama ambavyo CUF imetendwa chaguzi zote na kubaki
kulia kilio cha mbwa.

Tatizo jengine linaloikuta CCM ni vipi watatoka. Kwa hakika kama
tulivyosema wameshindwa, lakini vipi watawaambia wanachama wao ambao wamezoea kuwaambia kuwa kwanza wao hawawezi kushindwa, kuwa ushindi ni wa lazima, na kuwa hata wakishindwa hawatoi kwa kuwa nchi haiwezi kutolewa kwa vikaratasi yaani kura.

Na wanachama wa CCM wakaamini kabisa kauli hizo pamoja na kila mara kuingizwa katika chaguzi ambazo kwa akili ya kawaida tu ni kujua kuwa kwenye uchaguzi siku zote kuna mshindi na mshindwa na kwa hivyo , CCM pia ingeweza kushinda kama ilivyotokea kwa vyama vikongwe vya Malawi, Zambia, Kenya na kwengineko.

Na hata hivi karibuni kabisa kuna mfano mzuri sana kwa CCM huko Myanmar au zamani ikiitwa Burma ambako utawala wa kijeshi umedumu kwa miaka kupitia chama tawala kikongwe na kuthubutu hata kumuweka kiongozi wa magezui Aan Su kyi kizuizini kwa miaka kadhaa, na juzi hapa kimeshindwa uchaguzi, na kimekiri kuwa kimeshindwa.

Jengine ambalo linaisumbua CCM kuachia madaraka ni suala la kuzoea madaraka kwa miaka 50. Kimejenga mtandao mkubwa wa watendaji na magolikipa wa siasa ambao kuondoka madarakani ni kun’goa mizizi yao iliyokita kiuchumi, kisiasa na jamii na wengine wanafikiri watakwenda wapi, mtandao wao ukiondolewa.

Pia kuna suala la woga wa matendo yao waliyoyafanya kwa miaka, na kuyaendeleza hadi hivi sasa ya kudhulumu, kutesa na kuonea raia na ambayo wameyafanya kwa nguvu zao za kisiasa na kwa kuwa walikuwa wakijua kuwa sheria wao kamwe haitawagusa.

Lakini kwa jawabu zote mbili Maalim Seif amewahakikishia CCM kuwa hatakiuka taratibu yoyote ile ambayo ipo hivi sasa ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kwa vile matokeo ya Uwakilishi ni 27-27 basi tabaan ataunda Serikali ya usawa.

Na kabla hapo CUF ilishasema wazi wanataka kuwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo itashuka chini na sio kama ilivyo sasa ambapo Dk. Ali Muhammed Shein hakuwa na nia na wala hakupenda kutimiza ndoto ya kupanua dhana ya kuundwa kwa serikali ya pamoja. Na hata pia hakutimiza masharti ya kuwatoa wakuu wa mikoa na wilaya katika mstari wa kutumikia serikali na chama cha siasa.

Vilevile Maalim Seif ametoa uhakikisho kuwa hana nafasi ya kufufua makaburi. Atapiga mstari matendo yote yaliofanywa nyuma ili nchi isonge mbele kwa sababu kufanya visasi na kufufua maovu ni kuendeleza vidonda na Zanzibar tayari ina vidonda kadhaa ambavyo havijapona.

Huu sasa ni wakati mzuri na muwafaka kabisa kwa Rais Mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Pombe Magufuli kulikabili na kulimaliza suala la uchaguzi wa Zanzibar kwa njia ya suluhu na suluhu yenye uhalali ni moja tu nayo ni ya kuendela kutangazwa matokeo na aliyeshinda apewe ushindi.

Dk. Magufuli tunaamini tayari vyombo vyake vimeshampa taarifa za kutosha kuweza kujua kila kilichotokea kuanzia utandu mpaka ukoko yaani pia atapata taarifa za ziada kwa kuwaita au kukutana na wadau wakuu wa kadhia hii.

Tunajua kuwa matokeo yaliokusanywa na CUF yatakuwa sawa na yaliokusanywa na CCM na kwa hivyo yakilinganishwa na fomu ziliopo Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC, hayawezi kusema uongo. Huko nyuma matokeo yalikuwa yanatekwa nyara njiani, na kwa hivyo kuchezewa na kutangazwa nje ya ukweli.

Tume ilishatangaza matokeo ya majimbo yote kwa upande wa Uwakilishi yalikuwa yameshantangazwa na hakuna sababu yoyote ya kisheria kufutwa na hivyo ZEC itengue amri yake ya kufuta matokeo kama vile ya kufuta madiwani.

Hatua ya pili iwe kwa ZEC kuendelea kutangaza matokeo ya Urais ambapo hadi sasa ilishatangaza majimbo 31 ambayo uhalali wake haufutiki. Na kuna taarifa zisizo na utata kuwa ZEC ilikwisha thibitisha matokeo ya majimbo 9. Kwa hivyo ZEC ithibitishe majimbo 14 na kuyatangaza pamoja na hayo 9.

Tunamuomba Dk. Magufuli afanye uungwana na wajibu wake wa kwanza kwa Zanzibar kuimaliza kadhia hii. Anajua kuwa kwa kutaarifiwa kuwa ushindi wa CUF hauwezi kukatalika maana hauna shaka kwa kuwa imepata kura 25,000 zaidi ya CCM.

Dk. Magufuli aiambie CCM kuwa kushindwa ni sehemu ya ushindani na kuwa maisha yapo baada ya uchaguzi na kuwa aliyeshindwa leo ana nafasi zaidi ya kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa kesho na kubwa zaidi Zanzibar ni kubwa zaidi kuliko vyama vyetu.

Nakusihi Dk. Magufuli kuwa suluhu nyengine yoyote haitaiokoa Zanzibar. Wala suala la kurejewa uchaguzi halipaswi wala haliwezi kuwa ni mbadala. Hakuna mbadala ila kumpa mwenye haki yake ushindi wake. Na mwenye haki ni CUF na Maalim.

Kupitia kwa Dk. Magufuli CCM inapaswa iwaambie wanachama wa CCM kuwanchi inahitaji kusonga mbele na itasonga kwa kulimaliza tatizo hili. Mheshimiwa Rais chukua uongozi na ujipambanue na waliofanywa wenzako katika hali kama hii katika chaguzi zote zilozopita.
Kumbuka tatizo hili lisipotatuka kwa uhalali itakuwa kama ule mkasa wa tembo aliyemeza chura.
 Kwa miaka mitano na kwa historia nzima chura atakusumbua ndani ya tumbo lako.

No comments:

Post a Comment