Jiji la Dar kuwa chini ya Ukawa

By Raymond Kaminyoge, Mwananchi
Monday, November 30, 2015

Kama wingi wa madiwani katika halmashauri ndicho kigezo cha chama kumpata meya, basi safari hii jiji la Dar es Salaam litakuwa chini ya mameya kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Manispaa ya Ilala ambayo kuna karibu ofisi zote za Serikali zikiwamo wizara na Ikulu itakuwa chini ya meya wa Ukawa kwa mara ya kwanza kama ilivyo Kinondoni ambako karibu vigogo wengi wa serikali wanaishi.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa madiwani katika jiji hilo, Manispaa ya Ilala ina jumla ya madiwani 52 wakiwamo wabunge watatu wa Ukonga, Segerea na Ilala. Kati ya madiwani hao CCM ina madiwani 22, Chadema 23 na CUF saba.

Ukawa inaundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD ambavyo vimeshatoa msimamo wa kusimamisha mgombea mmoja kwenye manispaa hiyo kuwania umeya.

Hii ina maana kwamba Chadema na CUF wakiungana, watakuwa na jumla ya madiwani 30 huku CCM ikiwa na 22.

Katika Manispaa ya Kinondoni, matokeo yanaonyesha kuwa kuna jumla ya madiwani 47 ambao wakichanganywa na wabunge wa majimbo ya Kawe, Kinondoni, Ubungo na Kibamba wanafika 51.

Mchanganuo wa vyama na idadi ya madiwani kwenye mabano ni CCM (15), Chadema (28) na CUF (8).

Katika mchanganuo huo, vyama vya CUF na Chadema vikiungana katika umoja wao vitakuwa na madiwani 36 ambao watapambana na wenzao 15 wa CCM, hivyo kuweka manispaa hiyo yenye idadi kubwa ya vigogo wa Serikali mikononi mwa Ukawa.

Kwa upande wa Manispaa ya Temeke ambayo ndiyo pekee CCM ina madiwani wengi Dar es Salaam, wapo 46 wakiwamo wabunge watatu wa Temeke, Mbagala na Kigamboni.

Kati ya madiwani hao, CCM ina 29 wakati Ukawa ikiwa na jumla ya madiwani 17, Chadema (9) na CUF (8).

Maandalizi ya uchaguzi

Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema Ukawa itasimamisha madiwani kwa ajili ya kuwania nafasi zote za umeya na unaibu meya.

“Kwa idadi ya madiwani wa Ukawa waliopo ambao ni wengi kuliko wa CCM, tuna uhakika kwamba tutashinda nafasi za umeya na unaibu katika manispaa za Ilala na Kinondoni,” alisema.

Alisema Ukawa itahakikisha inaweka utaratibu wa kuwabaini madiwani watakaouhujumu umoja huo kwa kuwapigia kura wagombea wa CCM endapo itatokea: “Kwa hili hatuna mchezo tumeshawaeleza madiwani kwamba ni lazima tupate mameya wa Ukawa.”

Alisema hata Manispaa ya Temeke ambako kuna madiwani wengi wa CCM, baadhi yao wamewahakikishia kwamba watachagua meya wa Ukawa.

Alipoulizwa kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba alisema yanaendelea.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty alisema maandalizi ya ufunguzi wa kikao cha madiwani yanaendelea na kitafanyika mwezi ujao.

“Alhamisi iliyopita ndiyo tumepata madiwani wa viti maalumu, sheria inatutaka tuitishe vikao ndani ya siku 30 tangu siku tuliyopata madiwani wa viti maalumu, hivyo kikao kitakuwa siku yoyote ndani ya mwezi ujao,” alisema.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Protidas Kagimbo aliungana na mwenzake wa Kinondoni akisema vikao hivyo vitakavyochagua meya na naibu meya vitafanyika Desemba.

Madiwani waanza kampeni

Diwani wa Kata ya Vingunguti, Omar Moto alisema madiwani wanaowania nafasi za umeya wameshaanza kupitapita kuomba kura.

“Kuna madiwani wenzangu wamekuja nyumbani kuniomba kura ya umeya lakini nikawaambia hata mimi ninautaka, nasubiri Ukawa waweke msimamo,” alisema.

Katika uchaguzi wa meya wa jiji atakayemrithi Dk Didas Masaburi, upepo pia unavuma kuelekea Ukawa yenye madiwani 83 dhidi ya CCM madiwani 66.

No comments:

Post a Comment