Dr. Salim ashangaa Tangazo la kurudiwa Uchaguzi Zanzibar, ataka haki itendeke

NA ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, ameshangazwa na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta uchaguzi visiwani humo.

Amesema jumuiya za kimatifa zilishtushwa na uamuzi huo.

Salim amesema kutokana na hali hiyo, kinachotakiwa hivi sasa ni haki itendeke kwa kila kila upande kukaa na kutafuta suluhisho la kudumu.

“Tanzania haijazoea migogoro ya siasa jambo ambalo si jema katika sura ya kimataifa,” alisema.

Mwanadiplomasia huyo wa kimataifa ametoa kauli hiyo,baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, mwaka jana.

Siku chache zilizopita, Jecha alitangaza kuwa uchaguzi huo unatarajiwa kurudiwa Machi 20 mwaka huu.

Salim aliyasema hayo alipozungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu nyumbani kwake, Msasani, Dar es Salaam jana.

Mwanadiplomasia huyo wa kimataifa aliwahi kushika nafasi mbalimbali ikiwamo ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) ambayo kwa sasa inatambulika kama Umoja wa Afrika (AU).

Alisema hatua ya kufutwa uchaguzi wa Zanzibar ni jambo lililowashangaza wengi kwa kuwa uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu, huku waangalizi wa ndani na nje wakiusifia katika ripoti zao.

“Ni hatua ambayo imewashangaza wengi…imeibua sintofahamu kubwa katika nchi yetu kwa sababu uchaguzi uliopita Tanzania ilipata sifa,baada ya uchaguzi kufanyika kwa amani na utulivu. Lakini kitendo cha kufutwa kumewashangaza wengi na bado suala hili halieleweki.

“Pia hili jambo sidhani kama ni la mtu mmoja…sidhani kama ni la Jecha peke yake. Huu si mustakabali mzuri kabisa, Zanzibar ni nchi ndogo, lakini ina historia kubwa kisiasa hivyo juhudi za pamoja zifanyike kutatua mgogoro huu kwa matakwa ya Watanzania kwa ujumla.

“Viongozi wasisitize amani na utulivu na katika hili la Zanzibar kwa kweli haki itendeke na waache ushabiki wa vyama iwe CCM au Upinzani, wote waweke ushabiki pembeni na watatue mgogoro huu kwa mustakabali wa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla,” alisema Dk. Salim.

Alisema ingawa viongozi mbalimbali wamekutana na kufanya mazungumzo bila kupata suluhu,pande zote ziendelee kukutana hadi suluhu ya pamoja ipatikane.

Salim, alisema kuendelea kuachia hali hiyo iendelee kuna hatari ya kujenga uhasama zaidi hivyo ni vema viongozi wafikirie zaidi masilahi ya Zanzibar.

“Nchi ipo katika hali mbaya, migogoro iko kila pahala,Watanzania hatujazoea. Jambo hili la Zanzibar likiendelea litazaa matatizo makubwa katika Taifa letu.

“Waliangalie kwa uzito hata kama tarehe ya uchaguzi imetangazwa waendelee na mazungumzo,” alisema mwadiplomasia huyo wa kimataifa.

Dk. Salim ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alipoulizwa kama Kamati Kuu ya chama tawala katika vikao vyake ilijadili suala la Zanzibar, alisema limegusiwa ingawa haikuzungumzwa na ni nini kifanyike.

“…japo sikushiriki vikao vyote hivi karibuni kwa sababu nilikuwa katika majukumu mengine, jambo hili limezungumzwa japo halikugusiwa nini kifanyike.

“Jambo hili, linastahili kupewa kipaumbele hata katika vikao vya Kamati ya Kuu ya CUF (Chama cha Wananchi) na vyama vingine kwa sababu madhara yakitokea yataathiri kila upande,” alisema.

MABANGO

Akizungumzia kuibuka vitendo vya ubaguzi yakiwamo mabango katika sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar,Dk. Salim alishangazwa na hali hiyo.

Alisema kitendo cha baadhi ya wanachama wa CCM kubeba bango lililokuwa linaonyesha ubaguzi wa rangi wakati wa sherehe hizo, wakati suala la ubaguzi lilimalizika tangu mwaka 1964.

Alisema hatua hiyo, imeitia doa na ni aibu kwa Zanzibar na Tanzania.

“Nchi imekuwa mstari wa mbele kupinga ubaguzi,nimeshangazwa sana kwa kitendo kile. Ni jambo la kufedhehesha na lisipewe nafasi hata kidogo, ukianza kubagua watakaoathirika wengi ni watoto wa viongozi, huu ni ujinga na inaudhi,” alisema Dk. Salim.

Alisema kitendo cha wanachama hao kubeba bango hilo,kinadhihirisha wazi kuwa wameishiwa hoja kwa sababu suala la Hizbu ililikufa tangu mwaka 1964.

“Maswali ya kujiuliza ni kwamba siku wale wanachama walipobeba yale mabango katika sherehe za Mapinduzi kwa nini waliachiwa kufanya hivyo, viongozi waliokuwapo hawakuona?

“…kwa sababu nchi imedumisha utu, undugu na kupambana na ubaguzi wa kila aina hili, kitendo hiki kinasikitisha. Hata kama kuna mtu yeyote anayesema hili ni sawa huko ndiyo kufilisika kabisa,” alisema.

AKUMBUKA YA MWAKA 2005

Akizungumzia jinsi alivyotuhumiwa kwa kuitwa Hizbu wakati wa mchakato wa urais mwaka 2005, Dk. Salim alisema yalikuwa ni mambo ya kufadhaisha na yaliyojaa uongo.

“Nilizushiwa uongo sana na hata magazeti yakawa ‘part of the process’ (sehemu ya mchakato). Ilikuwa ni uongo wa kupindukia…watu wanapoona unakubalika na hauna sifa yoyote mbaya wanatafuta mambo ya uongo ili tu ‘wakudestroy’ (kukuharibu),” alisema.

MSAMAHA KWA WANAMTANDAO

Alipoulizwa endapo ikitokea wanamtandao ambao waliomuumiza katika siasa, ikiwamo hata kumsingizia kwa hoja za kumpaka matope, kama atawasamehe endapo watakwenda kumwomba msamaha, alisema wapo baadhi yao wamejitokeza na kwenda kwake.

“Wapo waliojitokeza wakiniomba msamaha, nimewasamehe kabisa… lakini sipo tayari kuwataja majina,” alisema.

KASI YA RAIS MAGUFULI

Akizungumzia utendaji kazi wa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, Dk. Salim alisema kuna wakati Serikali ilionekana kama imelala hivyo nchi ilihitaji kiongozi ambaye angeleta mabadiliko ya kweli.

“Magufuli ameanza vizuri ni muhimu aendelee hivyo, azingatie anahakikisha anapata ‘support’ (anaungwa mkono) kutoka kwa Watanzania, ahakikishe wanafanya wajibu wao bila vitisho. “Kuna wakati Serikali ilionekana kama imelala, amshaamsha hii ndivyo Serikali inavyotakiwa,” alisema.

SAFARI ZA NJE

Akizungumzia uamuzi wa Serikali kuzuia safari za nje zisizo za lazima kwa watumishi wa Serikali, Dk. Salim, alisema zipo safari za lazima zisizozuilika kwa sababu hata uamuzi wa Rais Magufuli si wa kudumu.

“Kuna safari za lazima, sidhani kama Rais amezuia, kuna zile za fujofujo ambazo hazina manufaa kwa Taifa hazina umuhimu.

“Safari lazima ipimwe kwanza, je kuna haja ya kwenda nje au ni kwenda kutumia fedha za umma tu. Naamini uamuzi huu si ‘permanent’ (wa kudumu),” alisema.

BOMOABOMOA

Akizungumzia bomoabomoa inayoendelea baadhi ya maeneo nchini, Dk. Salim alisema suala hilo linahitaji kutazamwa kwa pande zote mbili hasa kwa viongozi na wananchi.

“Watu wanapojenga katika hali ya hatari, lazima wahamishwe kwa sababu mvua ikinyesha wanakufa,wanapobomolewa Serikali ihakikishe watu hawapati usumbufu ni kitu cha balance (kulinganisha),” alisema.

KATIBA MPYA

Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Dk. Salim alisema hatua iliyofikia ni vema ziwepo jitihada za pamoja za kuondoa tofauti zilizopo.

“Katiba ni sheria mama ya nchi. Ni maelewano na maafikiano na wadau wa Katiba ambao ni wananchi. Nadhani unakumbuka mchakato ulivyoendeshwa na hata huu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umetokana na ile katiba baada ya kususia.

“Sasa ni muhimu kuleta kila jitihada za maelewano…ni muhimu sana juhudi zifanyike kuondoa tofuati zilizopo,” alisema.

CHANZO: MTANZANIA.

No comments:

Post a Comment