Hatutageuza tena shavu la kushoto, tukipigwa la kulia – Maalim Seif



Na Mwandishi wetu.

Sasa ni wazi kuwa vitendo vya kihalifu vinavyoaminika kufanywa na makundi ya vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) visiwani Zanzibar maarufu kwa jina la “Mazombi” na ambao wanaonekana kupewa ulinzi na ridhaa ya serikali na vyombo vya dola dhidi ya wafuasi na mali za wanachama cha Chama cha Wananchi (CUF), vimewafikia viongozi wakuu wa chama hicho kooni, baada ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kuthibitisha kauli ya hivi majuzi ya naibu wake, Nassor Mazrui, kuwa sasa “watajilinda.”

Akizungumza na wafuasi wake waliomtembelea nyumbani kwake Mbweni akiwa ametokea ziara ya matibabu India na Oman mchana wa leo (Machi 4), Maalim Seif alisema kuwa jeshi la polisi lilimkamata na kumuhoji Mazrui hapo jana kwa madai ya kutoa kauli ya uchochezi, lakini naye yuko tayari kukamatwa kwa kuwa msimamo wake ni huo huo.

“Musidhani kuwa mutatupiga shavu la kulia tukawageuzia la kushoto. Kila mara tunaibiwa, tunapigwa, tunafanywa kila kitu. Tukisema kuwa watu wajilinde, inakuwa nongwa. Basi tunawaambia kuwa kuitwa polisi, kuwekwa ndani, kufunguliwa mashitaka ya bandia, hata kuteswa, hayo ni mambo yamekuwa yakitutokea tangu 1992. Tumeshayazowea.”

Akishangiriwa na hadhira yake, Maalim Seif alisema udhalilishwaji kama huo haujawahi kukirudisha nyuma chake, zaidi ya kukiongezea umashuhuri na ufuasi mkubwa visiwani Zanzibar, huku akilituhumu jeshi la polisi kwa kuwa “tawi la CCM” ambalo litakuwa dhamana wa machafuko yoyote yatakayotokezea.

Katika hatua nyengine, Katibu Mkuu huyo wa CUF ambaye alikuwa mgombea urais kwenye uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015, amerejelea msimamo wa chama chake wa kutoshiriki kile kinachoitwa uchaguzi wa marudio ulioitishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha Salim Jecha, hapo Machi 20, akisema kuwa yeye alishahiriki uchaguzi na kushinda na hahusiki kabisa na uchaguzi mwengine.

“Ninamuambia Jecha kuwa uchaguzi huo ni wenu peke yenu,” alisema Maalim Seif, huku akimshangaa Dk. Ali Mohamed Shein kwa kutangaza sasa kuwa yuko tayari kukubali kushindwa kwenye uchaguzi wa tarehe 20 Machi endapo atashindwa, kauli ambayo hakuwahi kuitoa hata mara moja kuelekea uchaguzi halali wa Oktoba 25.

Maalim Seif amewasili nyumbani zikiwa zimesalia takribani wiki mbili tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi uliotangazwa na Jecha baada ya kuufuta ule wa Oktoba 25, ambao CUF inaamini kuwa ilishinda.

Chanzo: Zanzibar Daima

No comments:

Post a Comment