TAMKO LA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA JUU YA KUTEKWA KWA MWANDISHI WA HABARI WA SAUTI YA UJERUMANI ( DW ) SALMA SAID.



TAMKO LA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA JUU YA KUTEKWA KWA MWANDISHI WA HABARI WA SAUTI YA UJERUMANI ( DW ) SALMA SAID.
Salma Said mwandishi wa DW Zanzibar ametoweka baada ya kutekwa na watu ambao hawajafahamika jijini Dar es salaam, hali ambayo imeleta fadhaa na mshtuko kwa waandishi, jamii na familia yake  hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa marejeo Zanzibar.

Ifahamike kuwa Kazi  ya mwandishi wa habari ni kutoa habari juu ya kila kinachoendelea katika jamii , hivyo kama kuna dosari , dosari hiyo ni ya jamii na sio ya anayeieleza dosari .

UTPC inalaani na kupinga utekaji uliofanywa ambao sababu zake bado hazijulikani, hivyo tunaitaka serikali kuhakikisha Salma Said anatafutwa, kupatikana  na anaachiwa huru mara moja kwa kuwa Serikali ndio yenye jukumu la kulinda raia wake.

Kama utekwaji wa Salma umefanywa kutokana na kazi yake ya uandishi habari tunalaani vikali hatua hiyo, vitendo hivi havipaswi kuendelea katika  nchi inayoheshimu misingi haki na Demokrasia, Vitendo vya namna hii vinadumaza na kufifisha  uhuru wa habari .

Tunapinga kwa nguvu zetu zote  waandishi wa habari kukamatwa na vyombo vya dola au makundi ya kihalifu kwa visingizio ama vya uchochezi au maslahi ya taifa.

Waandishi tutaendelea kufanya kazi zetu bila kujali vitisho vya aina yoyote ile kutoka kwa mtu yoyote au Serikali.

Imetolewa na
DEOGRATIUS NSOKOLO
RAIS WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA -UTPC.
March 19, 2016.

No comments:

Post a Comment