Maalim Seif awasili Washington DC

Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad amewasili Washington DC amefuatana na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa CUF, Ismail Jussa, na Katibu wake ambaye pia ni Mkuu wa Watumishi katika Ofisi ya Katibu Mkuu, Issa Kheir Hussein.


Katibu Mkuu wa chama cha wananchi CUF Maalim Seif Sharif Hamad, pamoja na Mhe Jussa waliopowasili, kwenye uwanja wa kimataifa  Dulles  Airport, Jijini Washington DC,  siku ya Jumamosi June 11, kwaajili ya  ziara ya kikazi itakayochukua siku 14 nchini Marekani pamoja na Canada. 

Katika ziara hiyo, Maalim Seif na ujumbe wake watashiriki katika vikao na mikutano maalum na pia kufanya mazungumzo na viongozi na maofisa wa Serikali za Marekani na Canada, Wabunge wa nchi hizo, taasisi (think tanks) zinazoshauri sera za mambo ya nje za nchi hizo, taasisi za fedha, taasisi na jumuiya zinazohusika na masuala ya demokrasia na haki za binadamu pamoja na vyombo vya habari.
Mbali na mikutano hiyo ya kikazi, Maalim Seif na ujumbe wake pia watakutana na kuzungumza na Watanzania wanaoishi nchi jijini Washington DC na vitongoji vyake.

Akizungumzia ziara hiyo wakati anaondoka akiwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, mjini Dar es Salaam, Maalim Seif alisema: "Tumewaambia Wazanzibari kuwa ni lazima tuidai haki yao ya maamuzi ya kidemokrasia waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 kupitia kura zao. Tumewaambia tutaidai haki hiyo ndani ya Zanzibar, ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika jumuiya ya kimataifa. Ziara hii ni sehemu muhimu ya kufanikisha malengo yetu katika uwanja wa kimataifa na matunda yake yataonekana Inshallah".

 Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika mapokezi

No comments:

Post a Comment