MIAKA 16 YA KUMBUKUMBU YA MAUAJI NA UKIUKWAJI MKUBWA WA HAKI ZA BINAADAMU ULIOFANYIKA TAREHE 26-27, JANUARY, 2001
THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF- Chama Cha Wananchi)
Office of the Secretary General
P.O. BOX 3637, Zanzibar, Tanzania
TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI
Imetolewa Leo tarehe 26/1/2017
Na kurugenzi ya Haki za binaadamu na Sheria
KUHUSU MIAKA 16 YA KUMBUKUMBU YA MAUAJI NA UKIUKWAJI MKUBWA WA HAKI ZA BINAADAMU ULIOFANYIKA TAREHE 26-27, JANUARY, 2001
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF-Chama Cha Wananchi) kinawatangazia wanaCUF, wapenzi na watanzania kwa ujumla kuwa kesho tarehe 27 January, 2017 ni siku ya kuadhimisha miaka 16 ya kumbukumbu ya mauaji na ukiukwaji wa haki za binaadamu uliofanya na vyombo vya dola dhidi ya wanachama na wafuasi CUF waliojitokeza katika maandamano ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, pamoja na kudai kupatikana kwa katiba mpya, na Tume Huru za Uchaguzi –NEC na ZEC. Maandamano hayo yalipingwa na jeshi la polisi na kwa kutumia nguvu kubwa kuyazuia yalisababisha mauaji ya wafuasi wa CUF takribani 45 waliotambuliwa na tume ya Hashimu Mbita huku CUF tukikusanya takwimu za mauaji ya wanachama 73 ambao walipigwa risasi za moto na jeshi la polisi ambalo kwa wakati huo lilikuwa likiongozwa na IGP Omari Mahita na waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mohamed Seif Khatibu, chini ya serikali ya awamu ya tatu iliyokuwa inaoongozwa na Rais Benjamini Mkapa na Makamu wake Marehemu Dokta Omar Ali Juma. Ghasia hizo zilisababisha Uharibifu mkubwa wa mali za wananchi kwa uporaji wa makusudi uliofanywa na vyombo vya dola na vikosi vya SMZ maarufu kwa wakati ule Janjawid, zaidi ya watu 1800 walijeruhiwa vibaya na wengine kupata ulemavu wa kudumu. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, Tanzania ilizalisha wakimbizi wa kisiasa zaidi ya 4000 ambao walikimbilia katika kambi za ukimbizi Mombasa nchini Kenya, na wengine kukimbilia Somalia katika kambi ya Daadab.
MARIDHIANO NA MUAFAKA WA KISIASA ZANZIBAR;
JUHUDI ZA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD NA RAIS MSTAAFU Dk. AMANI ABEID KARUME KUWALETA WAZANZIBAR KUWA KITU KIMOJA:
Ni kutokana na Juhudi za Maalim Seif Sharif Hamad na Dk Amani Abeid Karume ambao walipata ridhaa na ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wazanzibari waliweza kuirejesha Zanzibar katika hali ya amani na utulivu baada ya uhasama uliodumu kwa kipindi kirefu miongoni mwa wananchi. Mwafaka wa kwanza na baadae uratibu wa kufanyika kwa kura ya maoni (referendum) na kutengenezwa muundo wa serikali ya umoja wa kitaifa (Government of National Unite-GNU) yaliyorasimishwa kikatiba ni mafanikio na hatua kubwa ya kisiasa, kiutawala, kijamii, kiuchumi, na kiusalama iliyofanikiwa kupatikana kutokana na hekima na busara za viongozi wetu hao. Viongozi hao walitanguliza maslahi ya wazanzibari na watanzania kwa ujumla mbele na kuweka kando ubinafsi, chuki, ubaguzi, na tamaa ya madaraka. Viongozi hawa wanapaswa kuheshimiwa na kuenziwa kutokana na juhudi hii kubwa waliyoifanya kuitoa Zanzibar katika dimbwi la uhasama na mtafaruku mkubwa wa kisiasa na kijamii miongoni mwa wananchi. Ama kwa hakika Mashujaa hawa wanapaswa kuheshimiwa na kila Mtanzania mpenda maendeleo, kwani hali ya kisiasa Zanzibar ilikuwa imechafuka na ilikuwa haitoi fursa ya kutosha kwa ustawi mzuri na maendeleo endelevu.
WAHAFIDHINA WA SERIKALI YA CCM WAMESHINDWA KUJIFUNZA NA KUTAKA KUTUREJESHA TULIKOTOKA:
Wakati kesho tukiadhimisha kumbukumbu hii kwa huzuni na majonzi makubwa ya kupotelewa kwa ndugu zetu na madhila waliyoyapata wazanzibari kutokana na kadhia hiyo, Kwa maksudi Wazanzibari wamerejeshwa tena katika mgogoro wa kisiasa na kusababisha uhasama, chuki na mkwamo wa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na wananchi wanaishi kwa hofu kubwa kuchelea usalama wao kutokana na vitendo vinavyofanywa na vyombo vya dola na vikosi vya SMZ (Mazombi). Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi-ZEC, Jecha Salum Jecha ameirejesha nchi yetu katika zahama kubwa baada ya kushinikizwa na wahafidhina wa CCM kinyume cha matakwa ya kikatiba na sheria za uchaguzi kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, 2015 siku tatu baada ya uchaguzi kufanyika na baadae kutangaza kurejewa kwa uchaguzi mwingine mpya tarehe 20 Machi, 2016. Huku Waangalizi wa ndani na wa wakimataifa walishuhudia mchakato mzima wa uchaguzi huo na kuridhishwa kuwa ulikuwa huru na haki. Matokeo hayo yalikipa ushindi mkubwa chama cha CUF na wazanzibari walimchagua kipenzi chao Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Rais wao.
Wazanzibari wameendelea kupata madhila makubwa ikiwemo kupigwa, kubambikiziwa kesi, kuharibiwa mali zao, kuchomewa nyumba zao na mazao yao mashambani, sera za ubaguzi zimerejeshwa upya na vijana wa CCM (UVCCM) vitendo hivyo vinafanywa mbele ya viongozi wa chama chao na serikali bila kukemea; tumeshuhudia watu wakiitwa machotara na mahizbu, nakadhalika; ni kutokana na juhudi, hekima na busara za viongozi wa CUF, na Maalim Seif Sharif Hamad Wananchi wa Zanzibar wameendelea kuwa watulivu, na wenye subira. Hata hivyo, Subira na uvumilivu una kikomo chake. Viashiria vya vitendo vya kuturejesha katika matukio ya January 27 mwaka 2001 yanapaswa kupingwa na kila Mzanzibari na Mtanzania mpenda amani, na maendeleo ya nchi yetu. Bado tuna deni kubwa la kuwahudumia mayatima na wajane waliotokana na mauaji hayo.
MATUMIZI MAKUBWA YA NGUVU ZA DOLA KATIKA UCHAGUZI WA MAREJEO KATIKA JIMBO LA DIMANI;
Kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi –NEC kushindwa kuusimamia uchaguzi huu kwa misingi ya haki, huru na kuzingatia sheria na taratibu za uendeshaji wa uchaguzi ni kiashiria tosha cha kusudio la kusababisha maafa makubwa katika nchi yetu kwa wakati ujao kama hali hiyo haitarekebishwa. Uchaguzi unaendeshwa kwa njia ya vitisho na wananchi kujengewa hofu na vyombo vya dola. Hii ni baada ya miaka 50 ya kujitawala bado serikali ya CCM inatumia dola kulazimisha kushinda uchaguzi. Wananchi wa jimbo la Dimani wamenyimwa haki yao ya kikatiba ya kumchagua mbunge wao. Uchaguzi umevamiwa na vyombo vya ulinzi, na vikosi vya SMZ. Tunafahamu kuwa uchafuzi wa demokrasia ndio sababu ya ghasia nyingi zinazotokea duniani. Tumeshuhudia katika uchaguzi wa Jimbo la Dimani masanduku ya kura yakipelekwa vituoni yakiwa yamejazwa kura, madaftari ya kupiga kura yalibadilishwa na wapiga kura halali wameondolewa, mawakala wengi walitolewa kwenye vyumba vya kupiga kura, wapiga kura na vitambulisho visivyo vyao, mapandikizi waliletwa kwa magari kwenye vituo kupiga kura wakisindikizwa na kulindwa na askari polisi, marehemu wapiga kura, wapiga kura kuingia kwenye chumba cha kupiga kura wakiwa na zaidi ya karatasi moja ya kupigia kura, fomu za majumuisho ya kura zaletwa vituoni na gari za polisi haya na mengine mengi ni miongoni mwa masuala ambayo kama si busara na hekima ya viongozi wetu isingezingatiwa nchi inaingizwa katika machafuko na ghasia kubwa. Matukio ya uharifu wa kupangwa kwa makusudi ni mengi, na yamekuwa yakifanyika kwa kuratibiwa na viongozi wa CCM kupitia askali wa vikosi vya SMZ maarufu Mazombi. Visiwa vyote viwili vya Zanzibar (Unguja na Pemba) vimekuwa ni waathirika wakubwa wa vitendo hivi vya kihalifu.
MUENDELEZO WA MATUKIO YA UKIUKWAJI WA HAKI ZA KIDEMOKRASIA TANZANIA BARA:
Hivi sasa kwa kasi kubwa vitendo vilivyozoeleka kufanywa visiwani Zanzibar, hivi vimehamia Tanzania bara, hii ni dalili tosha kuwa uelewa wa wananchi na nguvu ya umma imekuwa kubwa dhidi ya utawala wa mabavu wa serikali ya CCM. Shughuli za kisiasa za vyama vya siasa zinazuiliwa kinyume na katiba na sheria za nchi, viongozi wa vyama vya siasa wanakamatwa hovyo, kufunguliwa mashataka ya kubambikizwa na wengine kufungwa magerezani na au kunyimwa dhamana kwa makusudi, wakati haya yanaendelea kwa upinzani pekee haijawahi kuonekana hili likitokea kwa viongozi wa CCM wanaojulikana kwa uhalifu wanaofanya. Hivi karibuni kumekuwa na matukio mpaka ya utekaji wa viongozi wa CUF, wanachama kupigwa visu ndani ya mahakama lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kwa wahalifu hao mbali na jeshi la polisi kufungua jalada la mashauri hayo na au wakati mwingine kushuhudia uhalifu huo unapotokea. Hivi ni viashiria vya hatari kwa ustawi wa demokrasia nchini na inatishia usalama na amani ya wananchi.
Mwisho:
1. CUF-Chama cha Wananchi kinalaani mauaji ya raia wasio na hatia na vitendo vyote vya ukiukwaji wa haki za binaadamu vilivyofanywa na serikali ya CCM. Wananchi ambao walikuwa wanatekeleza haki yao ya kikatiba na kidemokrasia. Tunatoa wito na kuitanabaisha serikali ya CCM na Amiri jeshi Mkuu Rais Magufuli kutofanyia mzaha suala hili la matumizi makubwa ya nguvu za dola katika kuendesha shughuli za kidemokrasia na uchaguzi katika nchi yetu. Jeshi la Polisi limeshindwa kutekeleza wajibu wake kwa misingi ya haki, sheria na uadilifu; na badala yake limekuwa likitumika kama mkono wa kulazimisha ushindi wa CCM katika uchaguzi na kufanya kazi zake kisiasa zaidi badala ya kutanguliza uzalendo na weledi.
2. Tunatoa tahadhari kwa serikali ya CCM kuwa wananchi wamechoka uonevu na ukiukwaji wa haki za binaadamu. Wamechoka kunyanyaswa na kushindwa kuheshimiwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi nchini, misingi ya demokrasia na chaguzi zilizo huru na haki. Serikali ya CCM na vyombo vya dola visiirejeshe nchi katika matukio yaliyotokea January 26-27, 2001 na kusababisha umwagaji wa damu na mauaji ya raia wasio na hatia. Nchi hii wataitumbukiza katika maafa makubwa.
3. Chama cha CUF kitaendelea na juhudi zake za kuhakikisha kuwa migogoro ya kisiasa ya inapatiwa ufumbuzi kwa kutumia njia ya kidemkrasia na amani, na kuwaunganisha wazanzibari na watanzania wote kwa ujumla kuwa kitu kimoja kutanguliza maslahi mapana ya nchi yetu na Taifa kwa ujumla, kwa kuhamasisha na kusimamia kujengwa umoja na mshikamano wa dhati kwa mustakbali mwema wa kizazi cha sasa na kijacho.
4. Tunatoa wito na shukrani za pekee kwa viongozi wetu wote, wanachama, wapenzi na wananchi kwa ujumla, makhsusi kwa wakaazi wa Visiwa vya Unguja na Pemba kwa uungwana, ustahamilivu wao ambao unadhihirisha ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa, licha ya hujuma, mauaji, uchokozi na usumbufu wa makusudi uliofanywa na Jeshi la Polisi na vyombo vya dola pamoja na vikosi vya ulinzi tarehe 26-27 January, 2001 na vinavyoendelea kufanywa dhidi yao hivi sasa.
5. THE CIVIC UNITED FRONT (Chama Cha wananchi) kitaendelea kushirikiana na vyama vingine vya siasa, wadau mbalimbali ambao wanaunga mkono kuheshimiwa kwa demokrasia na misingi ya utawala bora kuhakikisha kuwa serikali ya CCM inaheshimu misingi ya demokrasia na watanzania tunapata tume huru za uchaguzi na katiba inayotokana na ridhaa ya watanzania wenyewe. Madai haya yanaungwa mkono na Jumuiya za kimataifa ambazo zilishiriki katika uangalizi wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na katika ripoti ya waangalizi wa Jumuiya ya Ulaya (EU EOM ELECTION OBSERVATIONS REPORT) walipendekeza utekelezwaji wa masuaa kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ikiwa ni pamoja na;
• kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi Zanzibar na Tanzania Bara (NEC na ZEC).
• Kupatikana haki ya wagombea binafsi katika uchaguzi wowote wa Muungano au Zanzibar.
• Kuruhusu haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais kisheria.
• Haki ya vyama vya siasa kuunda umoja wa kiuchaguzi.
• Kuangalia upya sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015.
• Kuendelezwa kwa muundo wa kudumu wa NEC katika ngazi za mikoa na marekebisho ya mchakato wa uteuzi wa makamishna wa uchaguzi wa NEC na ZEC.
• Kuangalia upya mchakato wa uandikishwaji wa wapiga kura Zanzibar ili kuhakikisha ushirikishi zaidi na imani ya wapiga kura.
• Kuhakikisha vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi zake kwa weledi, na kutotumika kisiasa na kuharibu michakato ya uchaguzi.
HAKI SAWA KWA WOTE
___________________________
PAVU ABDALLAH JUMA
NAIBU MKURUGENZI WA HAKI ZA BINAADAMU NA SHERIA
MAWASILIANO: 0773 110534/ 0777 414112
No comments:
Post a Comment