Malumbano haya ya Maalim Seif na ZEC yanaitia doa Z’bar

Juzi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad aliitisha mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam na kutoa tuhuma nzito dhidi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) akidai kuwa iliandikisha na kuruhusu watu wasiostahili zaidi ya 10,000 kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2010, kati ya hao, 8,507 wakiwa ni marehemu.
Maalim Seif, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF alidai kuwa wapigakura hao wasiostahili bado wapo kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura la Zanzibar.
Alitoa tuhuma hizo nzito alipokuwa akizungumzia utafiti wa Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa Zanzibar uliofanywa na chama chake kati ya Agosti 2014 hadi Machi 2015.


Alidai kwamba kwa mujibu utafiti huo, ZEC iliandikisha katika daftari hilo wapigakura wenye umri chini ya miaka 18, ambao si wakazi katika maeneo waliojiandikisha na waliotumia majina na picha ambazo siyo zao na kwamba Katika kutia uzito madai yake Maalim Seif aliwataja watu hao walioandikishwa na kuonyesha picha zao na maeneo wanayotoka akidai kuwa hiyo ni sehemu ya rafu zilizofanywa na ZEC ambazo chama chake kimezibaini kwenye utafiti na kwamba ina ushahidi wa kila aina ukiwamo wa majina yao, wanapoishi, vitambulisho vyao na picha zao.
Lakini siku moja tu baada ya madai hayo ZEC ilijitokeza na kukanusha vikali madai hayo huku Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi ambayo nayo ilishutumiwa na Maalim Seif kwa kuwanyima vitambulisho hivyo Wazanzibari wenye sifa nayo ikikana lawama hizo.
Katika majibu yake, ZEC imesema kwa mujibu wa sheria na taratibu za uchaguzi, kabla ya wananchi kupiga kura, daftari huhakikiwa na kubandikwa majina hadharani katika vituo vya kupigia kura na kama kulikuwa na dosari kwa watu wasiokuwa na sifa majina yao kujitokeza, ilipaswa kuwekewa pingamizi.
Tume hiyo ilisema kwamba sekretarieti yake inafanya kazi zake kwa kupokea maelekezo kutoka kwa makamishna wake wakiwamo wawili kutoka CUF ambao wanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na katika uchaguzi huo hapakuwahi kujitokeza malalamiko ya aina hiyo.
ZEC ilisema endapo kungekuwapo na kasoro ndani ya Tume za kiutendaji, makamishna hao wa CUF ndiyo wangekuwa wa mwanzo kulalamika kwa vile wapo jikoni na si viongozi wa chama chao kulalamikia kwenye vyombo vya habari.
Hakuna shaka kwamba kutokana na siasa za Zanzibar zilivyo ni dhahiri kwamba tuhuma na majibu haya yamewagawa wananchi. Wapo ambao wanaamini moja kwa madai ya Maalim Seif na ushahidi alioutoa lakini kwa upande wa pili, wapo ambao wameridhishwa kabisa na majibu dhidi ya madai hayo.
Lakini sisi tuna mtazamo tofauti kidogo na pande zote mbili. Kwa vyovyote vile, mambo haya yanatia doa misingi ya kidemokrasia ya visiwa hivyo na Tanzania kwa ujumla.
Kwa sababu hiyo, tunaziomba pande zote zinazohusika kukaa meza moja na kuchambua kwa pamoja na kwa nia njema madai yote hayo na kuyapatia ufumbuzi wa pamoja ili kila mmoja aridhishwe na ustawi wa demokrasia katika visiwa hivyo.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment