Msichana aliyevunja ungo kisiasa


Ahmed Rajab Toleo la 405 13 May 2015
 
ZILZALA au Mapinduzi? Nini hasa kilichotokea Uskochi alhamisi iliyopita, Mei 8, wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Uingereza?

Pengine utauliza: yanatuhusu nini yanayojiri Uskochi iliyo masafa ya kilomita zaidi ya 7,000 na Tanzania? Ni swali halali. Jawabu la mkato ni kwamba jinsi ulimwengu ulivyokunjana siku hizi na kuwa mithili ya kijiji, hatuwezi kuyakwepa yanayotokea upande wa pili wa dunia. Hata kama tunataka kufanya hivyo, enzi hii ya digitali haitupi nafasi.

Tukitaka tusitake, tukipenda tusipende, tunajikuta tunayaangalia ya wengine.Tunayapima, tunayatathmini na tunayalinganisha na ya kwetu.


Hivyo ndivyo tufanyavyo sasa, ikiwa imesalia miezi mitano kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania.Si ajabu tukishughulishwa na uchaguzi mkuu wa Mei 8 uliofanywa Uingereza, taifa lenye kujigamba kwamba ndio “mama wa demokrasia.”

Nakubali kuwa mfumo wa demokrasia uliozaliwa na Uingereza, unaojulikana kwa jina la “demokrasia ya Westminster,” ni mfumo wenye walakini nyingi na madosari yasiyosemeka. Si mfumo uliokamilika hata kidogo.Wala hawajakosea wanaohoji kwamba mfumo huo haufai.

Kusema kweli “demokrasia ya Westminister”ni mfumo ambao si lazima Tanzania au nchi yoyote nyingine ya Kiafrika iwe inaufuata. Juu ya hayo, sisemi kwamba mfumo huo hauna maana kabisa, tuutupe jaani au tuutose baharini.Bila ya shaka, una mazuri yake.

Ikiwa sisi tunajidai kwamba tunauiga basi hatuna budi kuuangalia namna ulivyo na unavyosarifiwa huko ulikozaliwa.Kadhalika, na muhimu zaidi, tuyaangalie na kuyaiga mema yake.

“Muungano” ni sababu nyingine inayotufanya tupaswe kuyaangalia kwa makini yaliyojiri Mei 8 Uskochi, moja ya nchi nne zilizo katika muungano wa United Kingdom (Utawala wa Kifalme ulioungana ambao sisi tumezoea kuuita Uingereza). Nyingine ni Wales, Ireland ya Kaskazini, na England (ambayo pia sisi huiita Uingereza).

Uskochi ni nchi yenye serikali yake na waziri kiongozi wake. Pia inachagua wabunge kuwapeleka kwenye Bunge la Westminster la Uingereza, jijini London.

Wales nayo ina waziri kiongozi wake, serikali yake na bunge lake liitwalo Baraza la Kitaifa la Wales lenye uwezo wa kutunga sheria kuhusu “Mambo 20 ya Wales” bila ya kulishauri Bunge la Uingereza au kumshauri Waziri wa Wales aliyeko London.

Ireland ya Kaskazini vile vile ina waziri kiongozi wake, serikali yake na bunge lake linalotunga sheria kuhusu mambo ya Ireland ya Kaskazini. Kwa sababu ya matatizo ya Ireland ya Kaskazini, bunge hilo mara kwa mara limewahi kusimamishwa na madaraka yake yakahaulishwa London kwenye wizara inayohusika na mambo ya Ireland.

England (Uingereza), kwa upande wake, haina serikali yake peke yake, wala bunge lake. Inaendeshwa na serikali inayoundwa na chama chenye wingi mkuu wa wabunge katika bunge la Westminster.

Kati ya nchi hizo nne ni Uskochi yenye watu wenye hamasa kubwa za kizalendo kuhusu nchi yao. Wamefika hadi ya kutaka Uskochi ijitenge na iwe dola huru yenye mamlaka yake kamili.

Tunaweza kuulinganisha wito wao na ule wa Wazanzibari wanaodai nchi yao irejeshewe mamlaka kamili.

Septemba 18, mwaka jana Waskochi waliulizwa kwenye kura ya maoni waamue iwapo wanataka wabakie ndani ya Muungano wa Uingereza ama watoke wawe na uhuru wao kamili.

Waliamua kuendelea kuwa sehemu ya Muungano. Asilimia 55.3 walikataa kuwa huru na asilimia 44.7 walisema wanataka Uskochi iwe huru.

Vyama vikuu vya Conservative na Labour viliwaunga mkono wanaopinga uhuru.
Aliyewaongoza wenye kudai uhuru alikuwa Alex Salmond, aliyekuwa waziri kiongozi wa Uskochi na kiongozi wa Chama cha Wananchi wa Kiskochi, Scottish Nationalist Party (SNP). Baada ya upande wake kushindwa alijiuzulu na mahala pake pakashikwa na Nicola Sturgeon, mwanamke wa mwanzo kuzishika nyadhifa zote hizo mbili.

Ijapokuwa wenye kutaka uhuru kamili wa Uskochi walishindwa mwaka jana kwenye kura ya maoni hata hivyo, hisia za kizalendo za kuipigania Uskochi na kuiweka mbele bado ziko hai.

Hisia hizo zilijitokeza kwa nguvu wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Alhamisi iliyopita.

Kura za majimbo ya uchaguzi ya Uskochi zilipohesabiwa ilibainika kwamba SNP kilinyakua viti 56 kati ya viti 59 vya bunge la Uingereza.Kabla ya uchaguzi huu, chama hicho kilikuwa na viti sita tu katika bunge hilo.

Cha Labour kilichoshinda viti 41 katika uchaguzi wa 2010, safari hii kilibakishwa na kimoja tu cha kufutia machozi. Wazalendo wa Kiskochi waliamua kukitia adabu kwa msimamo wake wa kupinga uhuru wa Uskochi.

Hapajawahi kupatikana ushindi wa kishindo kama hicho Uskochi. Vyama vikuu vya Uingereza viligharikishwa.

“Simba wa Kiskochi amenguruma,” alisema Salmond. Alisahau kuongeza kwamba simba huyo alivimeza vizimavizima vyama vyote vingine.

Ndipo tunapouliza iwapo yaliyotokea huko Alhamisi iliyopita yalikuwa ni matokeo ya zilzala ya kisiasa au kimbunga cha kisiasa? Au ni “tsunami” ya kisiasa iliyovizamisha vyama vote vingine na zaidi cha Labour? Au ni mapinduzi tu yasiyomwaga damu lakini yaliyowatoa wengi machozi?

Uchaguzi huo ulikuwa tukio kubwa la kihistoria si kwa Uskochi tu bali kwa Uingereza nzima. Ni uchaguzi ambao matokeo yake yataitikisa misingi ya Muungano wa Uingereza. Ni uchaguzi uliokuwa na mengi ya kusisimua na mengi ya kujifunza hususani kutokana na michuano ya kuwania majimbo ya Uskochi.

Jambo moja la kupigiwa mfano ni jinsi kampeni za uchaguzi na uchaguzi wenyewe, katika Uingereza nzima, kwa jumla, ulivyoendeshwa kwa usalama bila ya fujo au ghasia za aina yoyote ile.

Waliogombea uchaguzi, walioshinda na walioshindwa, walionyesha uungwana kwa kumwagiana sifa bila ya kinyongo cha dhahiri wakati wa kutangazwa matokeo ya kura.

Jingine ni kujiuzulu siku ya Ijumaa kwa viongozi wa vyama vikuu vilivyoshindwa vibaya katika uchaguzi huo, yaani Ed Milliband (Labour) na Nick Clegg (Liberal Democrats). Nigel Farage, kiongozi wa chama kidogo cha UK Independence Party (UKIP) naye pia alijiuzulu kwa sababu alisema kabla ya uchaguzi kwamba akishindwa kuchaguliwa akaingia bungeni atajiuzulu. Alishindwa na akajiuzulu.

Lakini kilichonisisimua mimi zaidi ya yote hayo, kuliko hata ushindi wa kishindo au zilzala au mapinduzi ya SNP ni namna alivyoshindwa Douglas Alexander, kigogo wa chama cha Labour aliyekuwa waziri kivuli wa mambo ya nje. Huyu ni mwanasiasa aliyebobea katika siasa kiasi cha kufanywa awe mratibu wa kampeni ya kitaifa ya chama chake.

Alikuwa mmoja kati ya walioupanga na kuongoza mkakati wa kukipatia ushindi chama hicho. Ajabu ya mambo ni kwamba hakuweza hata yeye mwenyewe kujipatia ushindi. Aliangushwa vibaya katika jimbo lake la huko Uskochi na kisichana kidogo, Mhairi Black (jina lake la mwanzo linatamkwa “Mary”) wa SNP.

Ushindi wa msichana huyo ni wa kusisimua kwa sababu ni msichana mwenye umri wa miaka 20 tu ambaye hata hakuhitimu bado masomo ya shahada ya mwanzo ya siasa na sera za serikali katika chuo kikuu cha Glasgow. Anatarajiwa kukamilisha masomo yake mwishoni mwa mwezi huu atapomaliza kuandika tasnifu yake.

Mhairi, ambaye ni mshabiki wa timu ya soka ya Patrick Thistle ya Glasgow (“Jags”), anakuwa mbunge wa Uingereza aliye mdogo kabisa kwa umri tangu mwaka 1667. Mwenyewe anasema kwamba jambo lililomtia hamasa zaidi aamue kupiga mbizi katika bahari ya siasa ni kura ya maoni ya mwaka jana kuhusu uhuru wa Uskochi.

Kabla ya uchaguzi, Mhairi aliwahi kusikika akisema kwamba watu wamechoka na chama cha Labour kwa sababu hakina lake jambo ila “kutaka kuwa na madaraka ili kiwe na madaraka.”
Kwa hayo, alikuwa anakusudia kusema kwamba chama hicho, ambacho awali akikiunga mkono, hakiyasikilizi tena matakwa ya wananchi, hasa wananchi wenzake wa Kiskochi. Sauti yake imekuwa sauti mpya ya SNP, sauti ya kuutetea mustakbali wa Uskochi.

Wenye kumjuwa wanasema kwamba pamoja na uzalendo wake wa Kiskochi, Mhairi anaaminika ana msimamo na ni msichana mwenye huruma.

Yaliyotokea Uskochi Alhamisi iliyopita ni ushahidi wa wazi kwamba muundo uliopo sasa wa muungano wa Uingereza karibu utaanza kumomonyoka na kufa. Hamna hili wala lile, mambo lazima yatabadilika.

Mapinduzi ya kikatiba yatakayoipa Uskochi mamlaka zaidi yapo njiani. Hayawezi kuzuilika kwa sababu wabunge wa SNP katika bunge la Uingereza wataingia katika bunge hilo wakiwa na msimamo mmoja wa kupigania maslahi ya nchi yao.

Wabunge hao, ambao wataongozwa na Salmond, wamekwishajipangia kazi yao: kudai Bunge la Uingereza lilipe mamlaka zaidi Bunge la Uskochi. Kwa ufupi, kudai Uskochi iwe na mamlaka yake kamili ya kujitawala.

Waskochi wamekuwa wakisema wamechoka kutawaliwa na serikali iliyo London.

Yalinganishe maneno hayo na malalamiko ya Wazanzibari wanaosema kuwa wamechoka kuwaona viongozi wao wa CCM/Zanzibar wakicheza ngoma inayopigwa Dodoma.

Kadhalika Waskochi wamekuwa wakisema wamechoka kutungiwa sheria zenye kuyaathiri maisha yao na Bunge lililo London. Kwa mfano, wanazipinga sera za serikali ya sasa ya Uingereza za kubana matumizi ya serikali.

Watu wenye kuaminika, kama Mhairi Black, ndio wenye kuthaminiwa katika siasa. Sababu iliyowafanya wapiga kura wa Uskochi wakipigie kura kwa wingi chama cha SNP ni kwamba hawakuwa na imani na wanasiasa wa vyama vingine kuwa watayatetea maslahi ya nchi yao.

Nathubutu kusema, kama wasemavyo wengi, kwamba hali itakuwa kama hivyo Oktoba Zanzibar ambako, kwa mambo yalivyo, haielekei kama wapiga kura wa huko watawatilia kura wagombea kura wa CCM.

Hawaamini kwamba watakuwa na ubavu wa kuyapigania maslahi ya nchi yao kwa vile bado wanautetea muundo wa Muungano wa serikali mbili.

Hata wenyewe wakereketwa wa CCM unapowavuta pembeni hukwambia kuwa wanakabiliwa na “hali ngumu.”

Kufyekwa kwa chama cha Labour Uskochi, na kufyekwa kilifyekwa, ni jambo la huzuni kubwa kwa chama hicho.

Ni msiba ambao, katika mfumo wa kidemokrasia, aghalabu huvifika vyama vya siasa vinapokuwa haviyajali matakwa ya wananchi.

Chama cha Labour kina historia ndefu Uskochi. Huko ndiko kilipozaliwa mwaka 1888 na kuitwa chama cha Labour cha Uskochi ingawa mkutano wa mwanzo wa kukiasisi chama hicho kitaifa ulifanywa London Februari 26-27, 1900.Kaulimbiu iliyokuwa ikipigiwa baragumu na waasisi wake ilikuwa “chama kipya kwa karne mpya”.

Waziri mkuu wa mwanzo wa serikali ya chama cha Labour, Ramsey MacDonald, alikuwa Mskochi. Yeye ni babake Malcolm MacDonald, Gavana Mkuu wa mwisho nchini Kenya (1963-1964). Hata waziri mkuu wa mwisho wa serikali ya Labour, Gordon Brown, ni Mskochi.

Kwa muda wa zaidi ya karne moja chama cha Labour kilikuwa kama mwewe juu ya siasa za Uskochi; ilizidhibiti vilivyo. Si leo. Wanaosikilizwa leo ni wanasiasa kama Mhairi Black, msichana mdogo lakini aliyekwishavunja ungo wa kisiasa.
Chanzo:Raia Mwema

No comments:

Post a Comment