Wamasai wapewa Vitambulisho Zanzibar

 Na Jabir Idrissa

NINAONESHWA kwenye simu ya kisasa, nakala ya kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi chenye jina la kijana wa Kimasai, mkaazi wa mtaa wa Darajani, mjini Unguja. Anamiliki kitambulisho kilichotolewa Aprili 2015.

Hakuna mkweli anayeamini Darajani kuna Mmasai amezaliwa na leo afikie kuandikishwa kwenye orodha ya Wazanzibari wanaostahili kupewa kitambulisho hichi.


Saa chache baadaye, mchana huo nilipoingia tu mjini, ninaambiwa lori la Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), sikupata namba zake za usajili, limepinduka likiwa na walioitwa wanachama wa CCM waliotoka majimbo ya mjini wakitoka Nungwi, kuhudhuria “mafunzo ya itikadi.”
Mafunzo ya itikadi kwa walio mjini yanapatikana Nungwi, kijiji cha kwenye rasi kaskazini mwa kisiwa cha Unguja ambako sasa ni ngome ya Chama cha Wananchi (CUF).

Siri ambayo kwa kweli si siri, inafichuka. Ni ushahidi tu mwingine kuwa JKU, pamoja na vikosi vingine vya SMZ, vinatumika kusaidia mikakati ya kisiasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Si hao tu. Rafiki yangu ambaye pia nyumba zetu hazipishani masafa marefu hivyo, ananionesha picha ya harakati za vijana wadogo wakiwasili na kuingia kwenye basi la Millitary Police ili kupelekwa wasikokujua.

Hili ni basi la makao makuu ya Jeshi la Wananchi hapa Zanzibar. Linatumiwa kutekeleza mikakati ya kisiasa ya CCM. Picha imepigwa Jumatatu wiki hii Kijangwani, eneo palipokuwa kituo kikuu cha mabasi ya umma.

Eneo hili siku hizi, ni maskani kuu ya wanajeshi wastaafu waliounda jumuiya na kuiita UMAWA – Umoja wa Majeshi Wastaafu. Wastaafu kweli, bali hapa wanafanya kazi kwa niaba ya CCM.

Kumekuwa na nyendo hizi za kukusanya vijana hata wasiotimia umri wa kupiga kura, kuwaahidi kazi kama si leo basi baada ya uchaguzi ujao, na kwa hivyo basi, lazima kwanza wasajiliwe na kupatiwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Kitambulisho hichi ni sharti muhimu la Mzanzibari kusajiliwa na kupatiwa shahada ya kupigia kura. Usajili wa kitambulisho hufanywa na Idara ya Usajili na Kitambulisho cha Mzanzibari, wakati upigaji kura ili kuchagua Rais wa Zanzibar, Mwakilishi na Diwani, ni haki ya kila mwananchi inayosimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Unaweza kuona hizi ni asasi mbili tofauti za serikali. Ni kweli kabisa. Bali zinafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa. Sheria ya kitambulisho ilipotungwa 2005, haikufungamanishwa na shughuli ya uchaguzi, ilikuja kuingizwa baadaye kwa matakwa ya CCM.

Yalikuwa matakwa ya CCM yaliyofuatwa kwa sababu wajumbe wa CUF katika Baraza la Wawakilishi waliikataa sheria ya kitambulisho, na sababu hasa wakasema kitaleta balaa kwa kuwa kimelenga kuzuia haki ya wananchi kupiga kura. Ilikuwa sheria iliyolenga maslahi ya kisiasa ya kuinufaisha CCM.

Wawakilishi wa CCM kwa wingi wao barazani, walipitisha kwa kauli moja. Serikali ikaitaka Tume ikitumie haraka kushurutisha wapigakura, lakini haikuwa. Tume ilisimama imara kwa kutambua ingekuwa shida.

Lakini Tume ilikubali uchaguzi wa 2010. Tangu baada ya uchaguzi wa 2005, kukipata kitambulisho kumekuwa afadhali ya kupanda mlima Kilimanjaro. Ni hapa viongozi wa CUF na wananchi wenyewe wamekuwa wakilalamika kunyimwa haki ya kuandikishwa ili kuingia kwenye daftari la kudumu la wapigakura la Zanzibar.

Haukupita muda ilithibitika pasina shaka yoyote kuwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi ni silaha ya kisiasa ya kuwakomoa wanaohisiwa kuwa watapigia kura wagombea wa CUF.

Hamkosi kusikia, na nimekuwa nikilieleza suala hili mara nyingi hapa, malalamiko ya wananchi kunyimwa kitambulisho, ambacho sasa ni kila kitu.

Bila ya kitambulisho hichi, Mzanzibari hapati kwa serikali ya mtaa idhini ya kupata cheti cha kuzaliwa, hapati barua ya dhamana kumtoa ndugu yake mahkamani, hapati pasipoti, hapati tiketi ya kusafiria, kuungiwa umeme au kupata leseni ya biashara, udereva.

Fikiria unataka kupeleka mgonjwa Dar es Salaam, huna kitambulisho. Unafanyaje? Unabaki kuhangaika na hatimaye itabidi ughushi.

Na vinawekwa vikwazo kupata kitambulisho hichi wakati sheria inasema wazi ofisa anayemzuilia mtu kukipata ni mkosa, kama alivyo mwananchi anayekutwa hana na akathibitika hanacho. Adhabu ni kifungo au faini, au zote pamoja.

Hapa Zanzibar maandalizi ya uchaguzi yalianza zamani. Ulipokwisha tu wa 2010, watu waliingia kazini. Mpaka sasa inasemekana watu wapatao 140,000 wanaostahili kitambulisho hawajapewa, huku serikali ikijitetea inavyo vitambulisho vingi wenyewe hawajavichukua.

Hakuna aliye tayari kuvitangaza majina ili baadhi yetu tusaidie kuwatafuta wenyewe. Huwezi kuamini, Mzanzibari aache yake na shida zote, afike kituoni kujisajili, apuuze kukichukua kitambulisho chake. Uongo usioaminika daima dawamu.

Wasiri wanasema wakubwa wamo kwenye mipango ya kuziba pengo la kura. Kila wakihesabu wanaona kama wamezidiwa na upinzani. Wao bado wanaamini mbinu chafu zinalipa, unapata ushindi wa kimbunga.

Wamesahau kwamba katika uchaguzi wa 2005, Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa CUF, alipigiwa kura nyingi ndani ya kambi ya Chuo cha Mafunzo Kilimani. Baadhi ya wapiga kura ni askari lakini hawakujali nini, walimchagua.

Ndivyo kunavyofanyika mbinu kuhusu ugawaji mpya wa majimbo. Tayari Waziri wa Tawala za Mikoa, Haji Omar Kheri ametangaza utaratibu wa kuongeza wilaya kisiwani Unguja.

Hatua yake imeweka wazi sasa ni wapi Tume ya Uchaguzi inayoongozwa na Jecha Salim anayejulikana kada wa CCM, itapita katika kuyagawa upya majimbo. Taarifa zinasema wakati wowote mgawanyo utatangazwa.

Zipo taarifa kuwa Pemba itapunguzwa majimbo mawili hivi. Unguja itapata majimbo angalau manne mapya.

Lakini msiri ameniambia amesikia ndani ya Tume wilaya ya Magharibi, ambayo imeongezewa wilaya ndani yake, ndio inatumika kutengeneza majimbo mapya angalau matatu.

Kwa taarifa hizi, ina maana majimbo ya Dimani, Kiembesamaki, Fuoni, Mwanakwerekwe, Koani, Mtoni na Dole, yanakabiliwa na mguso ili kupata majimbo hayo mapya.

Likishatoka tangazo la ZEC itajulikana kama vigezo vyote vya kisheria vya kuyagawa majimbo vimefuatwa. Isije ikawa kumefanywa kazi kubwa ya utafiti ikaishia kuweka mazingira ya kubeba CCM, kama ilivyozoeleka siku zote.

Yote hii inathibitisha ushindani katika uchaguzi safari hii umeongezeka nguvu. CCM inashuhudia ngome zake zikimegwa na CUF, inadai imezidi kupendwa na umma kutokana na sera zake nzuri. Inajivunia mafanikio ya serikali ya umoja wa kitaifa, ingawa wenyewe wanaichimba.

Katika kuthibitisha nguvu zake, CUF imechota waliokuwa makada wa CCM wakirudisha fomu za kugombea kupitia CUF, kama alivyofanya Mohamed Hashim Ismail aliyekuwa Waziri SMZ na Juma Hamad Omar aliyekuwa waziri katika Serikali ya Muungano wakati wa Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
Chanzo: HAPA

No comments:

Post a Comment