Mkutano wa Kumpokea Mgombea Urais wa CUF kisiwani Pemba


Maalim Seif: CCM ijiandae kisaikolojia kukabidhi Z’bar
 Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ameitaka CCM kujiandaa kisaikolojia kukabidhi madaraka kwa chama chake baada ya Oktoba, akisema katika chama chake hakutakuwa na neno “kushindwa”.


Wafuasi wa CUF wakinadi picha za mgombea Urais wa Chama hicho Visiwani, Seif Shariff Hamad katika mkutano wa hadhara wa kumtambulisha mgombea huyo uliofanyika kwenye Viwanja vya Tibilinzi- Chake chake Pemba jana. Picha na Said Khamis

Wafuasi wa CUF wakinadi picha za mgombea Urais wa Chama hicho Visiwani, Seif Shariff Hamad katika mkutano wa hadhara wa kumtambulisha mgombea huyo uliofanyika kwenye Viwanja vya Tibilinzi- Chake chake Pemba jana. Picha na Said Khamis Maalim Seif, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, aliwataka vijana popote walipo kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi ili kujitayarisha na ushindi aliouita mkubwa.Alitoa kauli hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Tibirinzi, Chake Chake Pemba na kuhudhuriwa na maelfu ya wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar.


“Hakuna kushindwa CUF, kwa hivyo mawazo yenu yawe na kushinda tu. Vijana, hakuna kukaa ukasema ushamaliza kupiga kura, unakwenda kwako unasubiri ushindi. Hakuna hilo mwaka huu, lazima mjitahidi kulinda ushindi wenu,” alisema Maalim Seif.Katibu huyo wa CUF alisema wananchi wa Pemba walioko Arusha, Mwanza na sehemu nyingine warudi kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura na kuwataka kutoacha fursa hiyo ambayo ni haki yao ya kidemokrasia.

Akitilia mkazo suala hilo, aliyekuwa waziri wa SMZ, Mansoor Yussuf Himid alimtaka Maalim Seif baada ya kupiga kura yake kurudi nyumbani na kuwaachia vijana kumkabidhi ushindi wa chama hicho.Mansoor ambaye ni mshauri wa Maalim Seif, alisema vijana wasitarajie kuletewa ushindi katika kisahani cha chai, washiriki kikamilifu katika kupatikana ushindi wa chama hicho.

Mansoor alisema hatima ya ushindi wa Zanzibar ipo mikononi mwa vijana, hivyo wanapaswa kuhakikisha ushindi wa Zanzibar unapatikana katika ya mikono yao.Akihutubia mkutano huo, Mwanasiasa Hassan Nassor Moyo alisema kazi ya Maalim Seif na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume kuleta umoja wa kitaifa si jambo jipya kwa kuwa lilianzia kwa Mzee Karume ambaye alitunga sheria kuondosha ubaguzi na kuwaweka wananchi wote wa Zanzibar kuwa kitu kimoja.

Uchumi
Katika hotuba yake ya takriban saa moja iliyorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Star TV, Maalim Seif alisema Maalim Seif alisisitiza nia yake ya kuifanya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ili iondokane na adhabu ambazo siyo stahiki kwake.Seif alisema Wazanzibari wamekuwa wakiadhibiwa kutokana na ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Bara.“…Leo watu wanafanya ufisadi huko, tunanyimwa fedha na wahisani halafu sisi ndiyo tunaadhibiwa kwa makosa ambayo siyo ya kwetu. Hatuwezi kukubali,” alisema Seif na kusisitiza kuwa hali hiyo imesababisha bidhaa kupanda bei na kuwaumiza zaidi Wazanzibari. “Zanzibar haina mamlaka kwenye nchi nyingine, hatuwezi kufungua ubalozi kwenye nchi nyingine. Hatuwezi kusaini mkataba na nchi yoyote, hatuna maamuzi juu ya sera, hatuna sera za kiuchumi. Sera zote zinatungwa Dar es Salaam… hii siyo sawa,” alisema Seif.

“Leo tukizungumzia suala la gawio tunapata asilimia 4.5 badala ya asilimia 11.5…ndiyo maana nasema Muungano uliopo hautusaidii. Tutapata kufaidika pale tutakapotapa mamlaka kamili. Zanzibar iwe na mamlaka yake na Tanganyika iwe na mamlaka yake. Halafu tukae pamoja tuangalie pale tunapoweza kushirikiana tushirikiane. “Kwani Tanganyika haiwezi kwenda bila Zanzibar… kwani kuna nini hapa,” alihoji Seif huku akishangiliwa na umati wa watu waliohudhuria mkutano huo.“Eti wanaokuja Zanzibar kutafuta wadhamini wanasema watawadhibiti wanaovuruga Muungano. Watawadhibiti hao CCM wenzao siyo sisi… tunataka uhuru wetu. Tunataka tupate mamlaka kamili.”Maalim Seif, ambaye alitamba kuwa ameteuliwa kwa mara ya tano kuwania urais kuwa kuwa anaaminika, alisema mpango wake ni kuboresha Bandari ya Zanzibar ndani ya mwaka mmoja na kuitangaza kuwa huru.

Alisema atahakikisha Zanzibar inakuwa na viwanja viwili vya kimataifa vya ndege.

Alisema ushindi wa chama hicho utakuja na mabadiliko ya kiuchumi yatakayowezesha kuimarishwa bandari huru katika kisiwa cha Pemba katika maeneo ya Mkoani na Wete akifafanua kuwa Pemba imekosa maendeleo tangu wakati wa ukoloni hivyo kuna haja ya kuimarishwa kiuchumi na kuendelezwa ili vijana waweze kufaidika na matunda ya nchi yao kwa kupatiwa ajira.
“Lazima tuwe na meli za kisasa za kasi ili kuimarisha usafiri na miundombinu kuwawezesha wananchi kuvusha biashara zao, alisema Maalim Seif ambaye safari hii anawania urais wa Zanzibar mara ya tano.Katika mkutano huo wanachama 400 walichukua kadi za chama hicho baada ya kuhama kutoka ADC.

Chanzo Mwananchi

No comments:

Post a Comment