TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 Chama Cha Wananchi (CUF) kinalaani vikali kitendo kilichofanywa na kikundi cha watu wapatao 20 wanaosadikiwa kuwa ni askari wa vikosi vya SMZ cha kuvamia kituo cha redio cha COCONUT FM kilichopo Kilimani, mjini Zanzibar jana tarehe 29 Juni, 2015 na kumtisha mwandishi Ali Mohamed wa kituo hicho kwa sababu ya kuandaa kipindi maalum kilichokuwa kikijadili hali ya vitisho inayoendelea katika uandikishaji wa wapiga kura.

Tukio hili ambao limefanywa na askari hao wakiwa wamejifunika nyuso zao kwa staili ya NINJA huku wakiwa na silaha za bunduki za SMG, mapanga, marungu, na msumeno wa Chain Saw na wakitumia gari zenye namba za vikosi vya SMZ ni muendelezo wa vitendo vya kukamata, kuwateka nyara, kuwapiga na baadaye kuwatupa kwenye vichaka watu kadhaa ambavyo vilianza pale uandikishaji wa wapiga kura ulipoanza katika kisiwa cha Unguja.

Kitendo cha kuvamia COCONUT FM na kumtisha mwandishi Ali Mohamed na wafanyakazi wengine ni kitendo kinacholenga kuvinyamazisha vyombo vya habari na waandishi wa habari ili waogope kuanika uovu unaofanywa na vikundi hivyo katika jamii.

Kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa na wapenda amani wote, watetezi wa haki za binadamu na kila anayeamini katika Utawala bora.

Inasikitisha zaidi kuona Jeshi la Polisi ambalo ndilo lenye dhamana ya ulinzi wa raia na mali zao linaiona hali hii ikifanyika mbele ya macho yake na halichukui hatua zozote kuzuia.

Badala yake tunawasikia Wakuu wa Jeshi la Polisi wakisema wao hawahusiki na vikundi hivyo. Ni dhahiri kwa hatua hizo na matamshi hayo, Jeshi la Polisi limeamua kukimbia dhamana zake.

Hali hii imeleta taharuki kwa wananchi wa Zanzibar ambao wengi wao wakiwa ni Waislamu wanaendelea na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani huku wakiwa wanakosa amani na utulivu hata wa kufanya ibada zao.

Hatukutegemea katika zama hizi baada ya Maridhiano yaliyofikiwa mwaka 2009 ambayo yalileta siasa mpya za maelewano kwamba Zanzibar ingerudishwa tena katika siasa za hujuma, vipigo, vitisho na uvunjwaji wa haki za binadamu na misingi ya Utawala bora.

Kutokana na hali hii: sisi katika CUF tunasisitiza haja ya kuchukuliwa hatua zifuatazo:

1. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, kuchukua hatua za kukomesha matukio haya na kuirudisha Zanzibar katika hali ya amani, utulivu, umoja na maelewano kama ilivyokuwepo wakati anakabidhiwa madaraka ya kuongoza nchi hii na mtangulizi wake, Dk. Amani Abeid Karume, mwaka 2010.

2. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, achukue hatua za kuhakikisha kuwa vyombo vyenye dhamana ya kusimamia ulinzi wa raia na mali zao vinatekeleza ipasavyo majukumu yake.

3. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, amwajibishe kisiasa Waziri mwenye dhamana ya Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheri, ambaye vikosi vilivyo chini yake ndivyo vinavyofanya uovu huu.

4. Iundwe tume huru ya uchunguzi itakayoshirikisha mashirika ya kimataifa yanayosimamia haki za binadamu ili kuchunguza na kubainisha ni nani wanaohusika na kutoa maagizo haya na utekelezaji wake na watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria.

5. Jumuiya ya kimataifa ifuatilie kwa karibu matukio yanayoendelea Zanzibar kuelekea Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na mwenendo wa mambo kwa ujumla na kuweka kumbukumbu sahihi ili kuona kama matukio haya hayavunji wajibu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa inayohusu haki za binadamu na Utawala bora ukiwemo ule unaohusu wajibu wa Tanzania katika Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

HAKI SAWA KWA WOTE
Ismail Jussa
Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma

No comments:

Post a Comment