Waandishi watishwa mwengine apigwa

Ali Makame Khamis ambaye amekatwa mapanga na watu waliojifunika uso
Ali Mohammed Abdulrahman aliyetishwa na polisi  
Kundi la watu wasiopungua 20 wakiwa wamefunika nyuso zao na kukamata silaha za moto, mapanga, na marungu jana wamevamia kituo cha Radio (Coconut FM) na kumtisha Mwandishi wa kituo hicho Ali Mohammed aliyekuwa akiendesha mjadala kuhusiana na uandikishaji unaoendelea katika Daftari la Kudumu la Wapiga kura Zanzibar na kumpiga vibaya Mpiga picha kwa kumcharanga mapanga.


Tukio hilo limetokea jana majira ya saa mbili asubuhi na kuzusha khofu kubwa wa wafanyakazi wa kituo hicho ambapo watu hao waliojifunika nyuso zao wakirusha mapanga juu na kumtishia kumpiga Mwandishi huyo ambaye alikuwa ndani pamoja na wafanyakazi wenzake.

“Walikuja kunitafuta mimi lakini wakawa wanatoa vitisho huku wamefunika nyuso zao kwa kweli sisi kila mmoja alikuwa anaogopa na mwenzangu mmoja tuliyekuwa tunaandaa kipindi pamoja yeye alizimia kutokana na vitisho na ule mshituko” alisema Ali Mohammed.

Alisema watu hao walikuwa wamebeba silaha hizo na kuchukua msumeno wa moto wa kukatia miti na kuuwasha kwa lengo la kuwatisha huku wakitoa vitisho vikali dhidi ya mwandishi huyo na kituo hicho kinachorusha mijadala ya moja kwa moja na kutoafursa kwa wananchi kupiga simu kutoa maoni yao.

Askari hao wametoa kila aina ya vitisho dhidi ya Mwandishi huyo kwa kukaribisha mjadala kuhusu vitendo vya kundi hilo kuingilia utaratibu wa uandikishaji uchaguzi na kumkosoa Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za mikoa idara maalumu, Haji Omar Kheri anaesimamia Vikosi vya Zanzibar kwa kusimamia hujuma hizo zinazofanywa wazi wazi bila ya kificho.

Mjadala huo ambao uliwashirikisha waandishi wa habari akiwemo Deogratuse Balile, Ali Saleh, Salim Said Salim, wakati kwa upande wa wawakilishi walioshiriki ni Mwakilishi wa CCM Hamza Hassan Juma na Mwakilishi wa CUF Hijja Hassan Hijja.

Katika kipindi hicho ambacho kimerushwa moja kwa moja huku wananchi wakishiriki mjadala huo kwa kupiga simu na kusikitishwa kwa yale walioyashuhudia katika mitaa mbali mbali kwa vikosi hivyo kutembea wakiwa wamefunika nyuso huku wabebeba silaha, huku watu kadhaa wakijeruhiwa na watu wasio na sifa kupelekekwa kuandikishwa katika vituo ambavyo hawana haki kuandikwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Wakati hayo yanatendekea katika tukio jengine Mpiga Picha, Omar Ali Juma ni mpiga amevamiwa  na kupigwa vibaya jana asubuhi wakati akitoka nyumbani kwake akielekea Mjini kufanya kazi zake na kuumizwa vibaya ambaye amelazwa katika hospitali akipatiwa matibabu.

“Nilikamatwa na kuingiza katika gari na watu walovaa Ninja wakanikamata na kunivisha kitambaa usoni wakanipiga sana mpaka nikapoteza fahamu na hapo nilipokuja kupata fahamu zangu najikuta sina chochote wameninyanganya kamera yangu na vitu vyangu vyote kisha wakanitupa ndipo nikapapatua na kufunua uso nikajikuta nipo maeneo ya maisara kituo cha KMKM” alisema.

Tukio jengine Ali Makame Khamis amepigwa vibaya na kukatwa kidole na watu waliojifunika uso na baadae kumtupa sehemu ambayo wasamaria wema walimuokota na kumkimbiza hospitali.

Hivi juzi Kamanda wa polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Mkadam Khamis Mkadam akizungumza na waandishi wa habari alisema jeshi la polisi halivai vitambaa vya kujifunika nyuso na linafanya kazi zake kwa uwazi halina sababu ya kujifunika nyuso katika utekelezaji wa shughuli zake.

“Mimi nimetembea katika vituo sijawaona hao watu mnaosema wamevaa vitambaa vyeusi lakini kama wapo vichochoroni hao mimi sijui” alisema Mkadam.

Hata hivyo katika kikao cha Baraza la wawakilishi Mohammed Aboud aliwahi kuwaambia wajumbe wa baraza hilo kwamba wale ni polisi na wanavaa vile kwa ajili ya usalama wao.

hivi karibuni Chama Cha Wananchi (CUF) waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kulalamikia zoezi linaloendelea la uandikishaji ambapo walisema watu wananyimwa kuandikishwa huku ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu ukifanyika mbele ya macho ya watu wa tume na jeshi la polisi bila ya kuchukuliwa hatua zozote.

CUF walisema vijana wao zaidi ya 20 wamekamatwa na jeshi la polisi huku watu kadhaa wakiwa wakitekwa nyara na kupigwa kisha kutupwa wakiwa taaban ambapo baadhi yao wanapokamatwa hunyanganywa kila kitu ikiwemo simu fedha na vitambulisho vyao.

No comments:

Post a Comment