Amani Karume usikonde, unahishima

Na Mwadini Ali

KILICHOANDIKWA kwenye ubao wa matangazo wa Maskani ya Muembekisonge, inayoendeshwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), ndio uthibitisho hasa wa fikra mgando zilizoganda akilini mwa viongozi wakuu wa chama hichi.


Maskani hii imeandika maneno yanayomlenga Amani Abeid Amani Karume, rais mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar, na kumtambulisha kuwa ni mwanasiasa mtiifu kwa Hisbu – kundi la wanasiasa waliopingana na Chama cha Afro Shirazi (ASP) kilichoongoza Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Chama cha Hisbu au Hisbulwatan, maana yake ikiwa ni “kiongozi,” chama kilichojumuisha wenyewe kuwa ni wanasiasa wa jamii za watu ambao asili ya nasaba zao ni nchi za Uarabuni, wanaojulikana kuwa walihamia visiwani Zanzibar.

Hisbulwatan ndio Zanzibar Nationalist Party (ZNP), waliochukuliwa kama wanasiasa waliokuwa mhimili wa utawala wa Kisultani ulioongozwa na Jemshid Abdalla, utawala ambao ulipata hifadhi ya kiulinzi ya mamlaka ya dola ya Uingereza.

Kwa watu wenye nasaba kindakindaki za Unguja na Pemba, Hisbulwatan wanajulikana kama nguvu iliyopamba utawala wa Kisultani ili kukabiliana na harakati au vuguvugu la Waafrika weusi waliokuwa wakitaka kuondokana na utawala wa wageni.

Tangu yalipofanikiwa mapinduzi ya 1964 ya Zanzibar, na walioyadhamini mapinduzi yale, yaliyosababisha umwagikaji mkubwa wa damu za raia, na ambayo yalitoa chimbuko la kuuliwa kwa mzee Abeid Amani Karume, baba mzazi wa Rais mstaafu Amani Karume, watu hao wameonekana maadui wa Serikali ya Mapinduzi.

Kwa hivyo basi, kwa kumsema Amani Karume kuwa heshi Uhisbu wake, ina maana CCM na hasa hawa wanasiasa wahafidhina wa Zanzibar, wanamtazama kivingine mwanasiasa huyu.
Amani Karume anaonekana asiyefaa kwa sababu haendelezi kaulimbiu ya Mapinduzi Daima, katika namna wanayoiendeleza wao wahafidhina – namna ambayo inaelekeza siasa za fitna, majungu, chuki na hasadi. Hizi ni siasa za uongo na uzandiki.

Hakika kabisa, Amani Karume ameondoka hapo. Amejitenga na siasa “zile” na kuamua kwa makusudi mazima kuendeleza siasa za maridhiano, siasa zinazoelekeza wananchi katika kupendana, kuoneana huruma na kusaidiana.

Amani Karume ameondoka katika kuendeleza siasa ambazo zinaelekeza wananchi kuchukiana, kusingiziana, kusimangana, kuchongeana na kutakiana mabalaa. Huko ameondoka.

Aliondokaje kwenye siasa “zile” wakati yeye ni kiongozi katika chama kinachoziamini kuwa bado ndizo zinazofaa kuendelezwa na kuzitilia nguvu kwa gharama yoyote? Ameondoka kule kwa sababu amebaini hakuna maana yoyote.

Amani Karume amejipima na kujiridhisha kuwa hapikiki tena chungu kimoja na waumini wa siasa “zile” za chuki, fitna na hasada. Aliyaona mengi alipokuwa mtendaji serikalini na akayashuhudia makubwa alipoingia katika siasa.

Lakini aliyafaidi na kuyaishi hasa maisha ya siasa “zile” chafu alipokuwa kiongozi mkuu wa Zanzibar, akiwa mas’uuli wa maslaha, amani na usalama wa wananchi wa Zanzibar – Unguja na Pemba.

Alikumbuka alivyoingia madarakani. Anakumbuka yaliyofanywa na anaowajua hata kujishika Ikulu. Huyu anakumbuka pasina shaka gharama za kufanikiwa kukalia kiti cha ukinara katika nchi anayojinasibu ni pao ingawa huku akikiri damu yake hasa imetokea nchini Malawi.

Anajutia yote hayo. Anajuta kuwa hata hakupaswa kuingia madarakani kimtindo kama ilivyotokea – watu wanyonge kuuliwa kikatili, wanawake wakubwa na kinadada kudhalilishwa, watoto na watu wazima kudhulumiwa kwa namna mbalimbali.

Najua alipo anajuta kwa yale yaliyotokea kukaribia, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka 2010. Wakati ninaoueleza kwamba kiongozi huyu mstaafu anayakumbuka yaliyotokea, ulikuwa wakati mbaya, mchungu kabisa na wakati usiosahaulika kirahisi machoni pa Wazanzibari na mawazoni mwao. Hawatasahau kirahisi hata kama kweli wanaweza kuwa wasamehevu kwa wa le walioyadhamini machafu yale, waliopanga na kusimamia utekelezaji wa dhulma ile.

Angalia namna gani aliyathibitisha ninayoyasema: mstaafu Amani Karume ameshiriki sambamba na viongozi wenzake katika uzinduzi wa kampeni ya   mgombea urais wa Zanzibar, wa chama chao CCM, katika mkutano uliofanyika uwanja wa Demokrasia, uliopo Kibandamaiti, mjini Zanzibar.

Alishiriki kabisa kila mtu ameona. Viongozi walipewa jukwaa pale kuhutubia umma. Na yeye akawa na nafasi yake ya kuhutubia. Wakatangulia wenzake, ikafika zamu yake. Huyo kiongozi akapanda jukwaa la kuhutubia.

Hutuba yake sasa ndiyo ikamuonesha Amani Karume anajuta. Amejifunza somo muhimu ambalo kwa bahati mbaya sana, halijaingia akilini mwa viongozi wenzake. Wala halijaingia akilini mwa wanamaskani wa Muembekisonge. Halijawaingia wenzake.

Anahutubia akisema Zanzibar nchi nzuri, yenye watu wazuri, watu wanaopendana, kuoneana huruma na kusaidiana. Zanzibar akasema nchi inayostahili watu wenye maisha mazuri, ya furaha na bashasha. Nchi yenye maendeleo yanayoonekana.

Mstaafu Amani Karume akasema nchi kama hiyo, yenye watu watambuzi, watulivu, wasikivu na wenye kupendana, kuhurumiana na kusaidiana, watu walio ndugu sana, haihimili siasa chafu “zile.” Niliwaeleza awali.

Kiongozi huyu aliyejifunza vizuri somo muhimu kuliko wenzake wanaomlaumu sasa, na hasa zaidi baada ya kuhutubia uzinduzi wa kampeni ya Dk. Ali Mohamed Shein anayetaka uongozi mara nyingine, akaonesha palepale alivyo tofauti na wenzake hao.

Alilalamika na akaonya wenzake waache siasa za majitaka (hakutaja neno ‘majitaka’) kwa sababu hazina manufaa yoyote kwa maisha ya wananchi wanyonge wa Zanzibar. Alionesha kuguswa na kauli za ovyo walizotoa viongozi wenzake waliomtangulia kuhutubia.

Borafiya Mtumwa Silima, mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini Magharibi, na Hamza Hassan Juma ambae wakati Amani Karume akiongoza alimteua waziri, na sasa mgombeaji tena kiti cha uwakilishi, walitapika matusi ya nguoni jukwaani pale.

Matusi na masimango waliyoyatoa jukwaani mchana kweupe, waliyalenga yawadhalilishe Maalim Seif Shariff Hamad, mgombea urais kama alivyo Dk. Shein, na Juma Duni Haji, anayempamba mgombea urais wa Jamhuri kupitia Chadema, Edward Lowassa.

Amani Karume akasihi kwamba maatusi na masimango yale hayana maana na hayafai katika siasa za kistaarabu Zanzibar. Maskini roho yake nzuri, hakujua kuwa siasa za maridhiano au za kistaarabu hizo anazitambua yeye sio hao wenzake na hasa waliokuwa palepale wakiyasikia matusi yale ya nguoni wasiwakataze.

Siasa za maridhiano anaziamini Amani Karume, hawaziamini Borafiya na Hamza, kama vile wasivyoziamini viongozi wakubwa wengine walokuwa uwanjani wakiwemo waliofuata baadaye pale nao wakatema matusi, masimango na kauli za uongo na upotoshaji.

Tofauti kubwa iliyopo kwa Amani Karume na wenzake hao ndiyo inamtambulisha yeye kama kiongozi mstaafu mzalendo wa kweli, mwenye huruma na ustahamilivu, na aliyejaa busara na hekima.

Rais mstaafu Amani Karume wala asihofu wajinga na wanaoshupaa kwa kujiona majemedari wa siasa Zanzibar. Wala asisumbuke kudhani hayuko kwenye stara, hata kidogo. Akae akijua amestirika na anahishimika kama kiongozi mkubwa mzalendo wa kweli kwa nchi na watu wake.

Amani Karume ametoa mchango muhimu katika nchi. Historia inamjali kama anavyochukuliwa na wananchi wema wanaopenda ukweli, uwazi, haki na siasa njema na zenye staha.

Ukishasoma hapa, mpelekee salamu Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita Zanzibar, mheshimiwa Amani Abeid Amani Karume kwamba namuwaidhi atulie wala asikonde, umma wa Wazanzibari unampenda na unamheshimu sana.

Mwambieni kuwa asisikitike kwa hayo anayoyaona yanatendwa na wenzake, kwa sababu hao wanaoyatenda, wanatafuta mambo yao binafsi, yaliyo tofauti kabisa na aliyoyalenga yeye yapatikane alipoakisi siasa za maridhiano akimshirikisha kiongozi mwema kama yeye, Maalim Seif Shariff Hamad.

Yeye Amani Karume na Maalim Seif ndio wenye moyo wa kujisikia fakhari kutandika mfumo wa uongozi unaoelekeza ujenzi wa siasa njema na zilizojaa staha kwa lengo la kuwapatia wananchi manufaa.

Wao wawili wanaamini na wangependa iendelee hivyo imani yao kwamba uongozi unaotenda mambo mazuri unatii matarajio na matakwa ya wananchi wanyonge, wale ambao kwao wahishimiwa wawili, ni nguzo na nguvu kubwa ya umoja wa kujenga Zanzibar ya maendeleo kama ya Singapore kwa ajili ya leo, kesho na uchao.

No comments:

Post a Comment