Jecha ni wa Kushtakiwa sio wa Kupongezwa

Image result for picha ya jecha na Magufuli
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetoa tamko la kumshangaa Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli kwa kutaka Jecha Salim Jecha, Mwenyekiti wa tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), atunukiwe tuzo kwa utendaji uliotukuka,.Chama hicho kimesema kwamba mshangao uliopo unahusu kitendo cha rais Magufuli kumsifia Jecha ambaye anajulikana dunia nzima kuwa amevuruga uchaguzi mkuu wa Zanzibar.
“Ni jambo la kushangaza Rais anamsifia hadharani Jecha kuwa amefanya kazi nzuri asilimia 100 wakati waangalizi wa ndani na nje wa uchaguzi walijiridhisha kuwa uchaguzi ulikuwa huru, wa haki na uliofanyika kwa amani,” amesema Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF.
Mtatiro ametoa taarifa hiyo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo ni majibu ya chama hicho kwa kauli alizotoa Rais Magufuli katika hotuba zake mbili alipokuwa katika ziara ya kushukuru wananchi wa Zanzibar. Alifanya mikutano Gombani ya Kale, Chake Chake Pemba Ijumaa na Kibandamaiti, mjini Zanzibar jana.
Katika mikutano yake alimsifia Jecha kuwa alifanya kazi kwa ufanisi na jana alipokuwa uwanja wa Demokrasia Kibandamaiti, alipendekeza apewe tuzo na Rais wa Zanzibar.
Mtatiro katika kauli yake amesema kwamba Jecha alipofuta uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015 alijifanyia tu bila ya kuwa na mamlaka yoyote ya kisheria ya kufanya hivyo.
Kwa kufuta uchaguzi, katika siku aliyotarajiwa kutangaza matokeo ya mwisho ya kura za urais, Jecha alivunja sheria na kusababisha tafrani hivyo kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kilichoitwa “uchaguzi wa marudio” uliofanyika 20 Machi 2016.
Ni katika uchaguzi huo wa marudio, Jecha alimtangaza Dk. Ali Mohamed Shein kuwa mshindi, utangazaji uliofanyika siku hiyohiyo ya uchaguzi. Tofauti na ilivyokuwa Oktoba 2015 ambako kwa siku nne Jecha alishindwa kutangaza ushindi wa CUF kilichomsimamisha katibu mkuu wake, Maalim Seif Shariff Hamad.
“Ni jambo lisilokubalika hata kidogo kujisifia ushindi wa kupora katika uchaguzi kutokana na kupendelewa na Tume ya Uchaguzi ikishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama,” amesema Mtatiro katika tamko lake.
Mapema kabala ya mkutano wa Mtatiro na waandishi wa habari kulitokea tafrani kati ya walinzi wa CUF na walioaminika wafuasi wa Mwenyekiti aliyejiuzulu na baadae kusimamishwa uanachama Prof. Ibrahim Lipumba waliotaka kulazimisha kuingia ndani ya makao makuu Buguluni.

No comments:

Post a Comment