KATIBU MKUU WA CUF AWEKA WAZI MSIMAMO WA CHAMA CHA CUF


Mazungumzo ya Katibu Mkuu WA CUF Maalim Seif  na Club ya Waandishi wa Habari Mwanza leo aeleza msimamo na wapi tunaelekea kama chama cha CUF pamoja na umoja wa UKAWA anasema  UKAWA upo hakuna wa kuuvunjani matakwa ya Watanzania Image may contain: 10 people, people standing



Dondoo za aliyoyasema Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad katika mazungumzo yake na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (Union of Press Clubs of Tanzania) wenye makao makuu Mwanza, leo tarehe 24 Mei, 2018

● Serikali iheshimu mawazo ya wananchi, waachwe huru kutoa mawazo yao.

● Katika maandamano ya mwaka 2001 wananchi wengi sana waliuawa na vyombo vya dola tofauti na idadi ya watu 45 waliotangazwa na tume iliyochunguza.

● Maridhiano ya mwaka 2010 hayakuwa ya Maalim Seif na Karume, yalikuwa ya Wazanzibari wote na ndiyo maana yalithibitishwa na Baraza la Wawakilishi na Wananchi wote kupitia kura ya maoni.

● Wapo viongozi wa CCM wenye nia mbaya ambao hawataki maridhiano, wanaona maridhiano yanazuia mipango yao binafsi ya uongozi, hao ndiyo wanatukwamisha.

● Zanzibar itajengwa na vijana waliofundishwa upendo na siyo chuki, wapo viongozi wanawaaminisha vijana wa vyama vyao kuwa hawa wakiingia madarakani watawaleta masultani, watapinga mapinduzi, watapinga maendeleo. Vijana hao wanapotoshwa.

● Uchaguzi wa Oktoba 2015 ulikuwa huru na wa haki na waangalizi wote wa ndani na nje ya nchi walithibitisha kwamba Zanzibar ilikuwa imefanya uchaguzi wa kwanza huru na wa haki.

● CUF ilishinda uchaguzi wa Oktoba 2015 kwa uwazi na bila ubishi, tulikuwa na matokeo kutoka kwenye kila kituo "polling station". Tulipojumuisha yote tukakuta nimemshinda Dk. Shein kwa kura zaidi ya 20,000.

● Wenzetu walipoona CUF tumeshinda, wakamwamrisha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC) afute matokeo, ndugu waandishi, Mwenyekiti huyo wa ZEC hana mamlaka ya kikatiba wala ya kisheria ya kufuta uchaguzi.

● Mimi ni mtu nisiyependa kabisa vurugu, baada ya hatua ile ya ZEC nikamwandikia barua Dk. Shein kumuomba tukutane, akanijibu tukutane na wajumbe wengine, nikakubali, tukakutana.

● Wakati tumeanza kukutana ili kujadiliana, wenzetu wakatuzunguka wakajitangazia uchaguzi mwingine mpya bila kujali kuwa Katiba ya Zanzibar haina kipengele kinachoruhusu kurudiwa kwa uchaguzi.

● Kama CUF ingeshiriki kwenye uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi 2016 ulioitishwa kinyume cha katiba ingekuwa inashiriki kuvunja katiba na sheria za nchi.

● Pia, chama chetu kilitoa wito kwa Wazanzibari wote wasiende kupiga kura, ndiyo maana kati ya wapiga kura wote 350,000 walioenda kupiga kura hawafiki 25,000.

● Baada ya kuwa nje ya serikali chama chetu kimezidi kuimarika, jambo msilolijua ni kuwa uamuzi wowote wa CUF huwa unaenda na wanachama na wafuasi wake, hata uamuzi wa kukataa kushiriki uchaguzi haramu umeungwa mkono na wanachama wetu wote.

● Hatujutii kabisa kuwa nje ya serikali, hatukuwa tunamtafutia cheo Maalim Seif, tulikuwa tunataka kuifanya Zanzibar iwe na maendeleo, iwe Singapore ya Afrika. Tulichokitaka ni kuongoza serikali siyo kuwa na Makamu wa Rais, tulikuwa na malengo makubwa sana.

● Wito wangu kwa Rais Magufuli tukae na tujadiliane kuhusu masuala muhimu ya Zanzibar.
[5/25, 12:32 AM] Philips: SEHEMU YA PILI:

Dondoo za aliyoyasema Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad katika mazungumzo yake na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari (Union of Press Clubs of Tanzania), Mwanza, Alkhamis, 24 Mei, 2018:

● Kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Uchaguzi ni tatizo kubwa sana. Wajumbe wa Tu  me wanateuliwa na Rais wa nchi ambaye ni mwenyekiti wa chama. Tunalazimika kushiriki uchaguzi kwenye tume hizi kwa sababu haya ni mapambano.

● Sisi Zanzibar tunaingia kwenye tume hiyo hiyo na tumekuwa tunashinda maeneo mengi sana na lengo la kushiriki ni kuchukua serikali ili tuwe na uwezo wa kuunda tume ambayo itakuwa inatenda haki kwa vyama vyote.

● Nawahakikishia Watanzania wote kwamba mimi ni mtu ambaye sikati tamaa.

● Niliahidi kwamba ndani ya miezi mitatu tungekabidhiwa serikali kwa sababu kulikuwa na dalili hizo katika mchakato, lakini kwa sababu miongoni mwa wenzetu wamo ambao hawana nia njema ndiyo mkwamo unaanzia hapo lakini nina uhakika kwamba Dk. Shein hafiki 2020.

● Hata ubaguzi wa rangi wa Afrika ya Kusini ulidhaniwa utadumu milele, lakini uliondoka haraka na wananchi wakapata serikali yao, hata ubabe wa CCM Zanzibar una mwisho wake, na mwisho wake hauko mbali, hautaendelea hivi hivi.

● Sioni kama 2020 kutakuwa na uchaguzi Zanzibar ikiwa hali itabakia kama hivi ilivyo. Tumewapa CCM muda mrefu sana wa kushughulikia masuala haya, wasidhani kuwa wataendelea kutuhadaa, sisi siyo watoto wadogo, haitawezekana.

● Shein hana uwezo wowote, maamuzi yanafanywa na Magufuli, Shein anaamrishwa na kuambiwa tu. Magufuli ndiye mwenye ufunguo. Kwa hiyo siwezi kukaa na kuzungumza na Shein, hata mkono nilimnyima, siwezi kuzungumza na mtu asiye na mamlaka yoyote.



● Mwandishi; Kwa nini huzungumzi na Magufuli? Maalim Seif: Nimeshafanya juhudi mara kadhaa, Magufuli hataki, nimemuandikia hawajibu hata barua. Kwa hiyo Dk.Shein siyo chochote pale Zanzibar, yeye ni kibaraka tu aliyewekwa.

● Mwandishi: Lakini mbona mazungumzo yako na Karume yaliwezekana na kwa nini kwa Shein yanashindikana?
Maalim Seif: Karume si Shein, Karume akifanya maamuzi anayasimamia, anao uwezo wa kufanya maamuzi. Dk. Shein anaendeshwa, hana maamuzi yake.

● Kinachoendelea ndani ya CUF siyo mgogoro. Tatizo ni Lipumba peke yake kama mtu wala siyo tatizo la kitaasisi. Kwa hiyo CUF hakuna mgogoro ili kuna mtu ametumwa na CCM na dola kuja kuivuruga CUF.
● Muungano nauunga mkono, lakini muundo ndiyo unawapa shida Wazanzibari ambapo wanajihisi kuwa koloni la Watanganyika. Watanganyika wamejivika koti la Muungano, Zanzibar haishirikishwi kwenye Muungano kwa maana halisi na malengo ya kuuunda.

● Wakati wa Mchakato wa Katiba, mimi binafsi nilitoa maoni yangu kuunga mkono Muungano wa Mkataba na haya ni maoni ya Wazanzibari. Ziko nchi nyingi zinafuata mfumo huo.

● Lakini baada ya Tume ya Warioba kuja na maoni ya Serikali Tatu, sisi wa Mkataba tukasema tuache msimamo wetu ili tuunge mkono muundo uliopendekezwa na wananchi wa Serikali tatu. Kama Kikwete angesimamia mchakato wa katiba jambo hilo lingekwisha.

● Hali ya Zanzibar ni mbaya mno kiuchumi, serikali haramu ya Dk. Shein haina maono wala vision (dira). Mpango wa maendeleo wa 2020 umebaki kwenye makaratasi, kwenye utekelezaji hakuna kitu. Serikali imeshindwa kuwapa fursa vijana wa Zanzibar.

● Zanzibar ina fursa nyingi sana lakini kwenye miti hakuna wajenzi. Zanzibar inaweza kuwekeza kwenye viwanda vya huduma pamoja na utalii. Wanikabidhi serikali mwaka mmoja tu mtaiona Zanzibar ikiwa Singapore ya Afrika Mashariki.

● James Mapalala alitugeuka baada ya kudanganywa na dola kuwa Maalim Seif anawasiliana na serikali za Uarabuni na wana mpango wa kuchukua serikali na kuwaondoa Wakristo wote, alihadaiwa kupitia barua za kughushi zikionesha zimeandikwa na mimi.

● Mapalala alianza  kuwapiga marufuku viongozi wa Zanzibar wasiingie bara na bara akaanza kuwafukuza viongozi mbalimbali bila kufuata utaratibu. Tukamwambia NO!, mambo haya yanafanywa kwa taratibu za vikao vya chama, siyo kwa maamuzi yako tu.

● Vikao vikamwita Mapalala akakataa. Tukaenda kwa Msajili Liundi. Liundi akatuambia itisheni Mkutano Mkuu wa Taifa mtatue matatizo yenu. Mapalala akakataa kuja kwenye Mkutano Mkuu, bahati nzuri Liundi alikuja na Mkutano ukachukua hatua zake.

● Hamad Rashid  alikuwa anataka Ukatibu Mkuu wa chama, ni haki yake, akaambiwa subiri wakati wa uchaguzi, omba ukatibu mkuu. Badala yake akaanza kuzunguka mikoani kupiga kampeni za wazi za kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wakati uchaguzi haujatangazwa.

● Kwenye ziara zake hizo Hamad Rashid akawa anamchafua Katibu Mkuu aliyepo. Akaitwa kwenye Kamati ya Utendaji ya Taifa kujieleza akakataa, akaitwa kwenye Baraza Kuu la Uongozi la Taifa akakataa, kwa hiyo vikao vikamchukulia hatua.

● Mgogoro huu wa Lipumba ni wa kupandikizwa. Bila kumung’unya maneno nasema katusaliti. Na bahati nzuri muasisi wa UKAWA ni Lipumba, UKAWA iliasisiwa Dodoma wakati wa Bunge la Katiba, Maalim Seif hakuwa mjumbe wa Bunge la Katiba.

● Viongozi wa vyama vyetu walikaa peke yao Dodoma wakasema lazima tushirikiane, hilo jina lenyewe la UKAWA kalipendekeza Prof. Lipumba na yeye ndiye alikuwa msemaji wa UKAWA.

● Mimi Katibu Mkuu wake hakunishirikisha hata kuiunda UKAWA lakini kwa sababu niliona ni jambo zuri nikaliunga mkono na kulisimamia, sikumlaumu mwenyekiti wangu kwa nini hukunishirikisha, baadaye akatugeuka.

● Ghafla Lipumba anakuja kutueleza kwenye Kamati ya Utendaji ya Taifa kuwa yeye anaacha Uenyekiti bila kujali kuwa tumo kwenye uchaguzi. Kapteni yumo kwenye mkondo wa maji, anaikimbia meli.

● Tukamuomba Lipumba aache kujiuzulu, wazee wakaja, viongozi wa dini zote wakaja kumuomba, kina mama, vijana, akashikilia msimamo wake kuwa anaacha uenyekiti.

● Lipumba aliposhikilia msimamo wake, Mimi nikawasihi wanachama kwamba huo ni uamuzi wake ni haki yake kwa hiyo msimtukane, mheshimuni. Huyu alikuwa Mwenyekiti wetu na kweli wanachama wakanisikiliza.

● Pamoja na Lipumba kujiuzulu bado tulimheshimu sana. Hata alipokuwa na Press Conference zake mimi nilikuwa natoa ruhusa atumie ukumbi wa chama. Vikao vingine muhimu vya Baraza Kuu la Uongozi tulikuwa tunamualika.

● Lengo la CCM lilikuwa ni kuisambaratisha UKAWA, UKAWA ni tishio kwa CCM na walidhani kuwa wakipata kiongozi mmoja wa juu wa UKAWA akajiuzulu na kutoka basi UKAWA itayumba na CUF itayumba. Halikutokea.

● Kuondoka kwa Lipumba hakukuiathiri CUF, kipindi Lipumba ni mwenyekiti wetu tulikuwa na Wabunge 2 au 0 upande wa Bara, hatukutwa na halmashauri hata moja na tulikuwa na madiwani wasiozidi 100.

● Baada ya Lipumba kutukimbia na kushiriki uchaguzi bila yeye CUF ikapata wabunge 10 bara, madiwani zaidi ya 300 na halmashauri zaidi ya 6.

● CCM na Dola wakaona kuondoka kwake hakukuiathiri CUF, ndipo wakamshawishi arejee, akaandika barua ya kutaka kurudi. Ni wapi duniani mliwahi kuona mtu anajiuzulu anakaa nje ya uongozi kwa mwaka mzima kisha anarejea uongozini, tena kwa nguvu?

● Serikali na CCM ndio wanamtumia Lipumba. Kwenye Uchaguzi wa wabunge wa EALA alipeleka mtu wake. Kamati ya Uongozi ya Bunge ikakaa ikaamua uchaguzi usifanywe kwa nafasi ya CUF. Spika akapigiwa simu na Ikulu na kuamrishwa kufanya uchaguzi.

● Lipumba amewafukuza wabunge 8 halali wa Viti Maalum wa CUF na kuweka wabunge wake kinyume na Katiba ya CUF na sheria za nchi. Haraka haraka wabunge wa Lipumba wakapokelewa na kukubaliwa na bunge. Kwa hiyo serikali na CCM wanamtumia.

● Lakini pia ili kujua kuwa wanamtumia, tazameni kuwa Lipumba anakwenda mikoani kufanya ziara na analindwa na Polisi. Katibu Mkuu halali anakwenda kufanya ziara kwenye mikoa ile ile anazuiwa na polisi wale wale. Tunahitaji ushahidi gani zaidi?

● Hoja kuwa tunapaswa kukaa meza moja na Lipumba haiwezekani. Lipumba ni msaliti. Adhabu ya Msaliti ni kubwa, huwezi kukaa naye meza moja. Katusaliti watanzania, katusaliti CUF, katusaliti UKAWA. Msaliti ni mtu hatari sana, siyo wa kumsogelea.

● Lipumba ameanza kufanyisha chaguzi feki za ndani ya chama bila kuheshimu kuwa kuna kesi mahakamani ili baadaye apate Mkutano Mkuu feki wamfukuze Katibu Mkuu. Katibu Mkuu huyu hafukuziki mpaka pale ambapo Mkutano Mkuu halali utaitishwa na CUF halisi.

● Lipumba amevamia Mkutano Mkuu wa CUF Ubungo bila kualikwa akisindikizwa na Polisi. Amevamia Ofisi Kuu za CUF Buguruni akisindikizwa na Polisi. Halafu nani anasema kuwa Lipumba hatumiwi na dola na CCM? Magufuli kajaa tele katika vurugu hili.

● Hoja kuwa Lipumba alijitoa kwa sababu hakukubaliana na mgombea Urais siyo ya kweli. Wakati ule Lipumba alishiriki kwenye mchakato wote wa kumpata mgombea wa UKAWA. Mwisho wakabakia wagombea wawili tu, yeye Lipumba na Dk. Slaa.

● Lipumba na Slaa wakaambiwa wakae chini waamue nani atasimama, wakashindwa kuelewana. Bahati nzuri Lowassa akaachwa na CCM, Lipumba mwenyewe ndiye alimfuata Lowassa, akamwambia inabidi uje kwenye UKAWA.

● Lipumba alimuomba James Mbatia amkutanishe na Lowassa. Aliyempeleka Lipumba hadi kwa  Lowassa ni dereva wa Mbatia. Lipumba akamuomba Lowassa akijiunga UKAWA aingie kwenye chama kidogo kama NCCR.

● Hata katika kumkaribisha Lowassa kwenye UKAWA hadharani, Mkutano wa waandishi wa habari juu ya ajenda hiyo uliongozwa na Lipumba mwenyewe na ukafanyikia Ofisi Kuu ya CUF Buguruni.

● Kwenye mkutano ule wa kumtambulisha Lowassa waandishi mlimuuliza Lipumba, "huyu mnasema ni fisadi kwa nini mnampokea?" Lipumba akawajibu Lowassa siyo fisadi, ufisadi ni mfumo na akawauliza tangu Lowassa aache uwaziri Mkuu mwaka 2008 ufisadi umekwisha?

● Hoja ya kuwa Lipumba alichukizwa na Lowassa kuwa mgombea urais ni ya uongo. Lowassa alipojiunga UKAWA alionekana ana nguvu kubwa kwa wananchi kuliko wagombea wengine wote akiwemo Lipumba na automatically akawa na nafasi ya kugombea urais.

● Hata hivyo Lipumba angegombeaje Urais wakati kila uchaguzi kura zake zinashuka na mwaka 2010 alipata kura laki 6? Lipumba hakuwa anauzika tena. Tumekwenda mahakamani kwani tumeona ndiyo suluhisho la pekee. Na maamuzi ya mahakama sisi tutayapokea kama yalivyo.

● Tuliwezaje kuzungumza na adui mkubwa CCM na sasa tunashindwa kwa Lipumba? Lipumba ni adui na msaliti wa ndani. CCM ni adui ya nje. Ni rahisi sana kuzungumza na adui wa nje kuliko wa ndani. Adui wa ndani ni msaliti.

● Swali la uhitimu wangu Chuo Kikuu cha DSM mwaka 1975 na kufaulu kwa kiwango cha juu sana na kuombwa na Chuo kubakia kufundisha ni la kweli. Lakini siyo kwamba nilikataa kubaki Chuo kama nilivyoombwa.

● Nilipenda kubaki chuo kikuu nifundishe lakini Serikali yangu ya Zanzibar ambayo ndiyo ilinipeleka chuoni ilileta barua chuoni na kueleza menejimenti kwamba natakiwa kurudi Zanzibar, nikawa sina chaguo zaidi ya kutekeleza matakwa ya serikali.

● Katika CUF Maalim Seif ni kama alama tu, lakini kuna viongozi wengi wenye uwezo mkubwa sana. Viongozi hao ukiwaambia chukua nafasi ya Maalim yeye apumzike wanakwambia hatuwezi kuvaa viatu vyake lakini mimi nawaambia utafika wakati watavivaa tu.

● Hata kama Mungu atanichukua leo hii. Nawahakikishia kuwa CUF inao watu ambao watakichukua chama na kukipeleka mbele kikiwa imara. Lakini tuna programu maalumu za kuwapa  mafunzo vijana wetu na wanawake.

● Kuhusu Serikali ya Magufuli, mimi nilikuwa na matumaini makubwa sana na serikali yake. Lakini kwa kadri siku zinavyokwenda navunjika moyo. Naweza kusapoti hatua za Magufuli kwenye maeneo machache sana moja kupambana na Ufisadi.

● Lakini juzi Rais Magufuli kanishangaza alipokuwa anapokea taarifa ya Kamati ya Dk. Bashiru Ally ya Mali za CCM akisema hatafukua makaburi wakati ripoti ile imejaa taarifa za ufisadi na mafisadi, amenishangaza sana. Hiyo ni dalili kuwa ameanza kuchoka.

● La pili nalomuunga mkono Magufuli ni kurejesha nidhamu serikalini, ingawa nidhamu yenyewe ni nidhamu ya woga. Lakini sasa naona anaanza kuchoka kidogo.

● Maeneo ambayo nadhani Magufuli na serikali yake hawafanyi vizuri ni mengi sana. Mojawapo ni Uchumi. Takwimu zao zinaonesha uchumi unakua kwa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka, lakini ukija katika maisha ya Mtanzania ni magumu mno.

● Tangu Magufuli aingie madarakani, sarafu ya Tanzania inaporomoka. Deni la Taifa linakua kwa kasi, sasa limefikia Shilingi Trilioni 60, ndani ya miezi mitatu Januari – Machi 2018 deni hilo limeongezeka kwa trilioni 3 kwa mujibu wa Benki Kuu.

● 75% ya Watanzania ni Wakulima ukijumuisha wafugaji na wakulima, lakini serikali ya Magufuli imepeleka Shs 170 Bilioni tu ambazo ni chini ya asilimia 3 ya bajeti nzima. Is he serious? Huwezi kupata Tanzania ya viwanda kama unadharau kilimo.

 ● Katika awamu zote CCM wanabadilisha kaulimbiu za kilimo; Kilimo cha Kufa na kupona, Kilimo ni Uti wa Mgongo, Kilimo Kwanza..... Kwa Magufuli yeye mambo ya kilimo kayatupa huko kabisa, kaja na kauli mbiu mpya ya viwanda visivyo na mipango.

No comments:

Post a Comment