Njama za CCM kuitia CUF mtegoni

Na Ahmed Rajab

WENYEWE watakataa, lakini sidhani kama ilikuwa ni jambo la busara kwa mawaziri wa Chama cha Wananchi (CUF) walio katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Zanzibar, kulisusia Baraza la Wawakilishi na kuacha kupitisha bajeti za wizara zao wenyewe.
Kufanya hivyo kumewapa CCM/Zanzibar, hususan wale wasioitakia mema SUK, fursa ya kuzidi kuchafua mambo.

Inafahamika kwanini wajumbe wa CUF waliamua kuchukua hatua waliyoichukuwa. Hata hivyo, nafikiri uamuzi wao uliongozwa zaidi na jazba badala ya tafakuri za kina.

Ni wazi kwamba CUF wametafishika na wamechoka na vitimbi wanavyoendelewa kufanyiwa kila siku na mahasimu wao wa CCM, hususan wale walioazimia kwamba lazima CCM ishinde uchaguzi ujao hata ikiwa ni kwa kutumia njia zilizo haramu.

Wajumbe wote wa CUF waliamua kulisusia Baraza baada ya kuwasilisha hoja ya dharura ya kutaka vijadiliwe vitimbi ambavyo wanasema vinawakuta wafuasi wao wanapokwenda vituoni kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Miongoni mwa vituko walivyovitaja ni urasimu katika utoaji vitambulisho vya ukazi wa Zanzibar na uandikishaji wa wapigakura.

Isitoshe, wameshutumu pia kuwa baadhi ya masheha wamekuwa wakikataa kuwaandikisha watu wanaowajuwa kuwa ni wafuasi wa CUF. Lalamiko jengine ni kuwako kwa wanajeshi na askari polisi wenye silaha katika vituo vya kuandikisha wapigakura, baadhi yao wakiwa wamevaa “ninja”.

Nimearifiwa wiki iliyopita kwamba katika eneo la Kombeni, katika mkoa wa Maghrib, wanajeshi waliovaa “ninja” walitawanyika katika vituo vya uandikishaji wapiga kura. Nasikia kwamba hayo yalionekana katika sehemu nyingine pia.

Kadhalika, CUF wameshutumu kwamba wanajeshi na polisi wametumiwa kulazimisha watu wasio na sifa zinazohitajika waandikishwe katika Daftari la Wapigakura. Picha zimekuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii zikionyesha wanaodaiwa kuwa “mamluki” wakisafirishwa kwenye magari na kupelekwa kwenye kambi za kijeshi kupewa vitambulisho vya Mzanzibari mkazi.

Hali hizo zimezusha vurugu katika vituo kadhaa vya uandikishaji wapigakura.
Njama hizo hazijajitokeza leo. Kwa wiki kadhaa sasa, viongozi wa CUF wamekuwa wakizigusia kwa kupiga vijembe na waziwazi katika mikutano ya hadhara. Maalim Seif Sharif Hamadi, Katibu Mkuu wa CUF na makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, alikwisha watahadharisha wenzake serikalini lakini mambo yamekuwa yakiendelea vilevile.

Mwishowe, Mei alikutana na Rais wa Zanzibar, Dr Ali Mohamed Shein, na mwezi huohuo alikutana na Rais Jakaya Kikwete, Dodoma na Dar es Salaam, kuhusu suala hilo. Hakuna lililobadilika.

Fujo hizo kwenye vituo vya uandikishaji wa wapigakura ni ishara mbaya kwa uchaguzi ujao.

Kwa hivyo, wana CUF walifanya ndivyo kuwasilisha hoja ya dharura kuyajadili mambo hayo.

Lakini Spika wa Baraza, Pandu Ameir Kificho, kwa sababu azijuazo mwenyewe, aliitupilia mbali hoja hiyo, tena kwa dharau.

Hatua ya Kificho ni ya kushangaza kwa sababu ilikuwa ni mahala pake Baraza lake kuijadili hoja hiyo ya dharura.

Inasikitisha kwa mtu mwenye kuheshimika na mwenye wadhifa muhimu kama wa Uspika kujiachia akaonekana kama anatumiwa na wanasiasa wenye dhamiri ovu.

Ilisikitisha kuona namna Kificho alivyokuwa akiwaridhisha wajumbe wa CCM kwenye Baraza walipokuwa wakikataa Maalim Seif na wasaidizi wake wasialikwe kwenye kikao cha kulifunga Baraza.

Alichofanya si kumdhalilisha Maalim Seif binafsi bali ni kukidhalilisha cheo cha umakamu wa kwanza wa Rais katika serikali ya ubia. Cheo hicho ni chenye kuwakilisha taasisi muhimu inayotegemewa na Rais katika serikali yenye muundo kama wa SUK.

Kwa upande mmoja, unaweza kusema kuwa aliyoyafanya Kificho kwa kejeli yalikuwa mambo ya kitoto yasiyolingana na hadhi ya wadhifa alionao.

Kwa upande mwingine, aliyoyafanya yanaweza kutafsiriwa kuwa ni dhihirisho la nia yake na ya wenzake ya kuivuruga SUK na kuitumbukiza nchi katika mazingira ya machafuko yanayoweza kusababisha umwagaji wa damu.

Sidhani kama nitakosea nikisema kwamba Spika kachafuka kwani kwa muda sasa amekuwa akifanya mambo ya kushangaza kabisa.

Kuna wasemao kwamba labda kuchafuka huko ni ishara ya kutapatapa kwake kwa vile kuna wahafidhina wa CCM/Zanzibar wenye kumtilia shaka. Kwa hivyo, lazima ajioneshe kwamba hajauvuka mstari na ni mwenye kuaminika.

Njia rahisi ya kufanya hivyo ni kufanya kama alivyofanya hivi karibuni kwenye mkutano wa hadhara wa Magogoni, Unguja, alipomtukana Maalim Seif, hata ikiwa kufanya hivyo kulimvunjia yeye heshima yake.

Hatua ya wajumbe wa CUF kulisusia Baraza la Wawakilishi imempa fursa yeye na wenzake wazidi kuikorofesha SUK ambayo kuwako kwake kulisaidia, kwa kiwango kikubwa, kuishusha homa kali ya kisiasa visiwani humo.

Mwenzake mwengine aliyepata fursa hiyo ni Vuai Ali Vuai, naibu katibu wa CCM, aliyetoa shutuma zisizoingia akilini dhidi ya viongozi wa CUF. Vuai aliwaambia waandishi wa habari kwamba CUF ilikuwa na mpango wa kuwazuia wafuasi wa CCM wasiandikishwe kwenye daftari la uchaguzi. Vipi walipanga kuutekeleza mpango huo, hakusema.

Ni wazi kwamba CCM wanafanya kusudi kuwachokoza, kuwabughudhi na kujaribu kuwatia kwenye mtego wana CUF. Ni wazi pia kwamba kwa namna zoezi la uandikishaji wapigakura linavyoendeshwa, CCM haijali kufanya mambo yasiyo halali.

Kwa hali hii CCM, na hasa CCM/Zanzibar, haitokamatika. Yanayojiri siku hizi tunapozidi kuukaribia uchaguzi mkuu, yanayathibitisha niliyowahi kuyaandika Julai mwaka jana kwenye makala chini ya kichwa cha maneno: “Lazima tushinde 2015 hata kama tutaua” [Raia Mwema, Toleo la 361].

Katika makala hayo nilieleza yaliyotokea kwenye kikao kimoja cha ndani cha viongozi wa CCM/Zanzibar pale kiongozi mmoja mzito aliposimama na kutamka kwa hamasa: “Lazima tushinde uchaguzi wa 2015 hata kama tutaua.”

Kwa mujibu wa aliyenipasha habari hizo wengi waliokuwa kwenye kikao hicho walishtushwa na matamshi hayo. Kwa bahati nzuri, juu ya uzito wake, kiongozi huyo alikemewa na mwenzake aliyekuwa na ujasiri wa kumuuliza atawaua kina nani? Swali hilo lilimyamazisha.

Wiki kadhaa baadaye niliandika makala mengine chini ya kichwa cha maneno: “Kwa mpigo huu CCM haishindwi, haishindiki.” [Raia Mwema, Toleo la 374].

Ukiyachukuwa yaliyogusiwa kwenye makala yote hayo mawili na yanayojiri sasa na ukayajumlisha na kauli za mara kwa mara za wahafidhina wa CCM/Zanzibar kwamba hawatoitoa serikali kwa karatasi (yaani kwa kura) ila labda kwa mtutu wa bunduki ni wazi kwamba viongozi hao wana dhamira ovu.

Wameazimia kuzipalilia moto siasa za chuki na wamedhamiria kuvirejesha visiwa vya Zanzibar katika siku zake za giza. Hawajali iwapo damu itamwagika, ilimradi madaraka yasiwaponyoke.

Inazidi kudhihirika kwamba kuna njama zilizokwishapangwa ambazo ni sehemu ya mkakati wa CCM wa kuhakikisha kwamba uchaguzi mkuu ujao hautopelekea pakapatikana mabadiliko yoyote Zanzibar.

Cha kushangaza zaidi ni kumsikia katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye,naye akitoa kauli ya kutisha aliponukuliwa kusema kwamba “CCM itashinda tu hata kwa goli la mkono.”

Tafsiri ya maneno hayo ni kwamba CCM lazima ishinde tu, ikibidi hata kama ni kwa kutumia ghiliba na udanganyifu. Tafsiri hiyo haiko mbali na maneno ya yule kigogo wa Zanzibar aliyenukuliwa kusema kwamba lazima CCM ishinde hata kama wataua.

Baada ya ripoti ya kauli yake kuchapishwa, Nnauye hakusema kama alinukuliwa vibaya. Hakutaka radhi wala hajakemewa — si na wakubwa zake, si na viongozi wenzake na wala si na hata mmoja wa wana CCM 41 wanaowania nafasi ya kuwa mgombea wa Urais kwa niaba ya chama chao.

Hakuna hata mmojawao aliyejitokeza kumkosoa. Tuseme wanamuogopa? Au ndo wamenasa katika utamaduni wa kulindana na wa kufunikiana kombe wanaharamu wapite?
Yote hayo ni ishara nyingine kwamba kuna kazi kubwa mbele ya safari katika medani ya uchaguzi mkuu wa Oktoba. Viongozi wasio na nidhamu wenye kutoa matamshi yanayogongana na misingi ya demokrasia ni viongozi wanaoweza kuuhatarisha mustakbali wa taifa, maendeleo ya watu wake na hata amani na utulivu wao.

Kwa upande wa CCM/Zanzibar, vitimbi vinavyofanywa na vigogo kadhaa wa huko, kwa upande mmoja, ni matokeo ya mahusiano mabaya ya kutoaminiana baina yao na vigogo wa CCM/Taifa huko Dodoma.  Hii ndiyo sababu iliyowafanya baadhi ya vigogo wa CCM/Zanzibar wapigwe na bumbuwazi pale Jaji Agostino Ramadhani alipojitokeza kuchukua fomu ya kutaka achaguliwe awe mgombea wa Urais kwa kupeperusha bendera ya CCM.

Wazanzibari hao wanaamini kwamba Ramadhani katomezwa na wenzao wa Bara ili kumvunja nguvu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.

Kwa ufupi, wanamuona Ramadhani kuwa si wao; na, kwa hakika, yeye siye wamtakaye.

Wenye kuyasikia yasemwayo kwenye vikao vya ndani vya CCM/Zanzibar wanaripoti kwamba ingawa baadhi ya hao vigogo wa Zanzibar wamekuwa wakizila fedha za Lowassa lakini hata naye siye wao.

Wamtakaye ni mwengine kabisa, na wala si miongoni mwa Wazanzibari waliojitokeza kuwania nafasi hiyo. Ala kuli hali kwa mambo yalivyo, haielekei kwamba CCM/Zanzibar itakuwa na usemi mkubwa kuhusu suala hili. Kama kawaida, uamuzi utakatwa Dodoma na wataokuwa na usemi mkubwa ni vigogo wa CCM watokao Bara.

Hili ni moja linalowaudhi CCM/Zanzibar kwamba huwa hawana ubavu wa kuzuia maamuzi yao yasitenguliwe Dodoma. Wanatambua kwamba wanadharauliwa na wenzao wa Bara lakini badala ya kuzielekeza hamaki zao Dodoma wanazielekeza dhidi ya CUF.

Jinsi wanavyojiona kuwa wanadharauliwa Bara ndivyo na wao wanavyozidi kuwaonyesha ubabe mahasimu wao wa CUF.

Jengine linalowakera wahafidhina wa CCM/Zanzibar ni namna Maalim Seif anavyoheshimiwa na viongozi wenzao wa Bara zaidi ya wao. Matokeo ya yote haya ni ukakamavu wa viogozi wa CCM/Zanzibar wa kuhakikisha kwamba hakuna kitachoweza kuwaondosha kwenye madaraka baada ya uchaguzi wa Oktoba 25, hata ikiwa watalazimika kutumia nguvu.

Juni 26 wakati wa kulifunga Baraza la Wawakilishi, Rais Shein alisema jambo moja lenye maana sana kuhusu uchaguzi ujao analopaswa yeye mwenyewe na wenzake walizingatie kwa makini. Alisema: “Kuanzia sasa macho ya ulimwengu yanatuangalia.”

Kusema kweli, macho ya ulimwengu yamekuwa yakiangalia Zanzibar kwa muda sasa. Mpaka sasa hayakufurahishwa na yaliyoyaona.

Yameshuhudia wahafidhina wa CCM wakiwatukana matusi ya nguoni wapinzani wao, wakitamka maneno yanayoashiria utumizi wa nguvu na yameshuhudia vyombo vya dola vikitumiwa dhidi ya wapinzani, kinyume na sheria. Wanawachochea wafuasi wa CUF waingiwe na jazba ya kulipiza kisasi kisha watiwe nguvuni kuwa ndio walioanzisha vurugu.

Kinachovunja moyo ni kuwaona wale wazuri wa CCM, wenye busara na wenye kuona mbele, wakikaa kimya. Hawayasemi hadharani wanayotunongoneza faraghani.

Baruapepe: ahmed@ahmedrajab.com
CHANZO: RAIA MWEMA

No comments:

Post a Comment