Headlines News :
KARIBU CUF DIASPORA NETWORK - CUF HAKI SAWA KWA WOTE...TEGEMEA KILA JIPYA NA ZURI KUTOKA KWETU...LIKE PAGE YETU KWENYE FACEBOOK
Home » » CUF kuigeuza Z’bar kituo kikuu cha biashara

CUF kuigeuza Z’bar kituo kikuu cha biashara

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema anakusudia kuifanya Zanzibar kuwa visiwa vya fursa za biashara na ajira kwa wananchi.

Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba (kulia), akimtambulisha rasmi mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa wananchi wa Zanzibar.

Maalim Seif ambaye tayari Chama chake kimeshamteua rasmi kuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, ameeleza hayo katika viwanja vya Kibandamaiti, wakati akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho kwa ajili ya mapokezi ya mgombea huyo.

Amesema Zanzibar inazo fursa nyingi za kuweza kunyanyua kipato cha wananchi, na kwamba ataweka kipaumbele katika kuziibua na kuziendeleza fursa hizo.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema katika kujenga mazingira bora ya uwekezaji, ataisimamia ipasavyo Mamlaka ya vitega uchumi, ili kuondosha vizingiti vinavyokwamisha uwekezaji nchini.
Amefahamisha kuwa wapo wafanyabiashara wengi wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kuwekeza miradi mikubwa ya kiuchumi, lakini wamekuwa wakipata usumbufu, jambo ambalo ameahidi kulishughulikia muda mfupi baada ya kuingia madarakani.
Sambamba na hilo, Maalim Seif amesema iwapo atachaguliwa kuiongoza Zanzibar, atahakikisha kuwa Zanzibar inakuwa na shirika lake la ndege ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, ili kurahisisha shughuli za kibiashara ikiwemo Utalii.
Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na wananchi.
 Amesema hatua hiyo itakwenda sambamba na uboreshaji wa huduma za viwanja vya ndege, ambavyo vitaweza kutoa huduma bora kitaifa na kimataifa.

Aidha amesema chini ya uongozi wake iwapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015, ataitangaza Zanzibar kuwa bandari huru, sambamba na kujenga bandari mpya itakayotoa huduma bora kwa mwambao wa Afrika Mashariki.
Katika hatua nyengine Maalim Seif amesema anakusudia kuongeza viwango vya mishahara kwa wafanyakazi wote, pamoja na kuzingatia maslahi ya wastaafu na wazee wasiojiweza.
Akizungumzia kuhusu mafuta, Maalim Seif amesema anakusudia kuanzisha Wizara ya Mafuta na Gesi ili kurahisisha uchimbaji wa nishati hiyo, itakayoondosha hali ya umasikini katika visiwa vya Zanzibar.
Maalim Seif pia alizungumzia hali ya amani na utulivu nchini, na kueleza kuwa amani ya kweli itapatikana iwapo vyombo vinavyohusika vitatoa haki kwa wananchi wote.
Mapema akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba, amesema Baraza Kuu la Uongozi la CUF limeshawika kumuidhinisha Maalim Seif kuwa mgombea Urais wa Zanzibar, kutokana na uwezo na nia ya dhati ya kuwatumikia wazanzibari.

Amesema viongozi waliopo madarakani wana dhamana na wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao unafanyika katika hali ya amani, sambamba na kuheshimu maamuzi ya wananchi katika uchaguzi huo.
Chanzo: Haki na Umma

Share this article :

No comments:

Post a Comment

 
Support : ZENJIBARZA
Copyright © 2011. ACT WAZALENDO DIASPORA NETWORK - All Rights Reserved