Na Ahmed Rajab
WIKI iliyopita nilipata baruapepe kutoka kwa rafiki yangu mmoja wa Burkina Faso ambaye kwa muda mrefu sasa amekuwa chanda na pete na Blaise Compaoré, Rais wa nchi hiyo aliyepinduliwa kwa ghadhabu ya umma mwishoni mwa Oktoba 2014.
Wanavyoamini wao ni kwamba Chama cha Wananchi (CUF) kikiushika uongozi wa Zanzibar kitauvunja Muungano.
Sasa tuseme Kitine, na usomi wake wote, hatambui kwamba Zanzibar
ilipata uhuru wake kamili Desemba 10, 1963? Na kwamba uhuru huo,
haukupatikana kwa umwagaji wa damu bali kwa mazungumzo yaliyofanywa
kwenye meza katika jumba la Lancaster House, London?
Aidha, Msangi asisahau kwamba kabla na wakati wa kampeni za uchaguzi
umma ulishtushwa kwa matusi ya nguoni ya baadhi ya wanasiasa kwenye
majukwaa yao. Jeshi la Polisi lioneshe kwamba halina upendeleo kwa
kuwashughulikia watuhumiwa wote bila ya kujali ni wa chama gani cha
siasa. Kanda za video zenye ushahidi wa tuhuma wanazotuhumiwa zipo.
WIKI iliyopita nilipata baruapepe kutoka kwa rafiki yangu mmoja wa Burkina Faso ambaye kwa muda mrefu sasa amekuwa chanda na pete na Blaise Compaoré, Rais wa nchi hiyo aliyepinduliwa kwa ghadhabu ya umma mwishoni mwa Oktoba 2014.
Waburkinabé, wananchi wa Burkina
Faso, walikuwa wamekwishamchoka Compaoré aliyekuwa madarakani kwa miaka
27. Alipoamua kuibadili Katiba ili aendelee kutawala zaidi waliona
anawageuza mafala (malofa), ndipo walipoghadhibika wakaingia mitaani na
kumpindua. Compaoré hakuwa na hila ila kuikimbia nchi na kwenda kutafuta
hifadhi Côted’Ivoire.
Katika baruapepe yake rafiki
yangu hakuyadhukuru hayo ya sahibu yake ambayo lazima akiyakumbuka kwani
yamemjaa kichwani. Lakini aliyagusia kwa mbali kwa kutoa mfano wa hii
aibu ya watawala wetu inayowafanya wawe kichekesho duniani kwa kuufuta
uchaguzi uliokamilika walipoona chama chao kinaelekea kushindwa katika
mchuano wa urais wa Zanzibar.
Yafuatayo ni tafsiri ya
aliyoniandikia rafiki yangu: “Tanzania imepoteza fursa ya kuuthibitishia
ulimwengu kwamba sisi (Waafrika) tuko tayari kufuata utawala wa sheria,
utawala bora na utawala wa kidemokrasia. Bado demokrasia halisi na moyo
wa kukubali kushindwa katika uchaguzi haukutia mizizi katika Bara letu
ambalo lingali la giza. Walio madarakani wangali wakiwazuia wengine
walioshinda uchaguzi wasiweze kuwatumikia wananchi.”
Halafu akanikumbusha yaliyotokea
Côted’ivoire baada ya kufanywa duru ya pili ya uchaguzi wa urais
Novemba 28, 2010 ambapo Alassane Ouattara aliibuka mshindi kwa kupata
asilimia 54.1 ya kura zote zilizopigwa. Ushindi huo ulitangazwa na Tume
ya Uchaguzi ya nchi hiyo.
Chama cha Rais Laurent Gbagbo
kilikataa kuyakubali matokeo hayo. Kama kisemavyo Chama cha Mapinduzi
(CCM) kuhusu kura za Pemba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, chama cha
Gbagbo nacho kilisema kwamba kulitokea ghiliba katika kura hizo za
kaskazini mwa Côted’Ivoire. Tume ya Uchaguzi ilikataa na kusema hayo
hayakuwa kweli, waangalizi wa kimataifa nao pia walisema uchaguzi mzima
ulikuwa wa haki.
Lakini Gbagbo aliushikilia uzi
ule ule wa chama chake na akalazimisha Mahakama ya Kikatiba yazifute
kura zipatazo 600,000 zilizopigwa katika majimbo tisa ya kaskazini,
ambako ni ngome ya Ouattara. Mahakama yakaitika “hewala bwana”,
yakayafuta matokeo ya kaskazini na yakasema kwamba kwa kuondolewa kura
hizo za kaskazini Gbagbo alishinda kwa asilimia 51.
Katika baruapepe yake rafiki
yangu alinikumbusha kwamba “hatimaye Gbagbo aliondoshwa madarakani kwa
nguvu na hii leo yuko Hague anafanyiwa kesi ya aibu.”
Alimaliza kwa kuandika: “Bado
tumo tu tunayashutumu madola ya Magharibi kwa ukoloni mamboleo lakini
viongozi wetu wa Kiafrika nao hawayajali maslahi ya raia zao…Inavunja
moyo…Tunafuata njia mbaya.”
Kwa Zanzibar hiyo “njia mbaya”
ndiyo iliyotufikisha hapa tulipo. Kwa ilivyo hivi sasa, zaidi ya nusu ya
wananchi wa Zanzibar wamepokonywa haki yao ya kimsingi ya kuongozwa na
Rais wamtakaye. Wamebakishiwa uhuru wa kuzitii amri za CCM, chama chenye
kushika mpini wa utawala.
Jamii isiyokubali mabadiliko ni
jamii iliyochakaa. Haitaki mambo mapya, inayashikilia yaleyale ya kale.
Vivyo hivyo kwa watawala. Chama chochote kinachotawala kisipokubali
kuondoka madarakani wananchi wanapokitaka kiondoke, huwa pia kimechakaa.
Ukaidi wa kukataa kupumzika kwa miaka mitano mpaka uchaguzi ujao ni
dalili moja tu ya kuchakaa kwake.
Pamoja na kuchakaa, bila ya
shaka zipo sababu nyingine za kwa nini CCM kinakataa kuyaachia madaraka
Zanzibar licha ya kujuwa kwamba kilishindwa katika uchaguzi wa urais wa
Zanzibar mwaka jana. Moja ni haja ya kuyalinda maslahi ya kibinafsi ya
baadhi ya viongozi wake wakuu, lakini sababu kubwa au tuseme kisingizio
kikubwa nadhani ni kile cha kuuhifadhi Muungano.
Kuna vizingiti viwili vikubwa
alivyovikuta Rais John Magufuli aliposhika uongozi wa taifa, na vyote
vimewekwa na sera za chama chake; navyo ni vizingiti vya demokrasia na
Zanzibar. Vizingiti hivyo vinafungamana.
Kwa vitendo na matamshi yao
watawala wa Zanzibar pamoja na wa CCM-Taifa ni wazi kwamba hawaiamini
kwa dhati dhana ya demokrasia na wala hawakubali Zanzibar iwe
inajiamulia mambo yake yenyewe. Kila siku zikisonga mbele tangu Muungano
uundwe Aprili 1964 majaaliwa ya Zanzibar ndipo yanapozidi kuamuliwa
Dodoma, kwenye makao makuu ya CCM.
Ndio maana haikustaajabisha,
ingawa ilisikitisha, kusoma kwenye gazeti moja karibuni Dk. Hassy
Kitine, mkurungenzi wa zamani wa Usalama wa Taifa, akinukuliwa akitamka
kwamba Maalim Seif Sharif Hamadi, aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar
katika uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, anaota akidhani kwamba ataiongoza
Zanzibar. Hatoruhusiwa kamwe.
Miongoni mwa mengine
aliyonukuliwa Kitine kusema ni haya: “Wenzetu wamepata uhuru wao kwa
kumwaga damu, tofauti na sisi huku, ambako Mwalimu Nyerere alitumia meza
ya mazungumzo kusaka uhuru, kwa wenzetu siyo”.
Mazungumzo yalikuwa baina ya
Serikali ya Uingereza na wanasiasa kutoka Zanzibar, akiwemo Sheikh Abeid
Amani Karume, kiongozi wa Afro-Shirazi Party (ASP).
Damu ilimwagwa na Mapinduzi ya
Januari 12, 1964, mapinduzi ambayo hayakuupindua utawala wa Uingereza
bali yaliipindua serikali huru ya Zanzibar iliyokuwa ikiongozwa na
Waziri Mkuu Sheikh Mohamed Shamte Hamadi.
Kitine alitoa kauli nyingine
yenye kusikitisha na usiyoitarajia kwa mtu kama yeye. Hakuona aibu
kutamka kwamba watu wanahangaika kutafuta uongozi wa Zanzibar “jambo
ambalo haliwezekani kwa sababu nchi hiyo haikukombolewa kwa makaratasi,”
yaani kwa kura.
Sasa angelitueleza kwa nini
matrilioni ya fedha za umma zinatumiwa kwa udanganyifu wa kujidai tuna
demokrasia ilhali imekwishaamuliwa kwamba CCM kikishinda kisishinde
katika uchaguzi kitaendelea tu kutawala naiwe iwavyo?
Huo ni uamuzi wa wale wanaoamini
kwamba ni wao pekee wenye haki ya kuziongoza serikali mbili za
Tanzania, ya Muungano na ile ya Zanzibar. Niliwahi kuandika mwaka jana
katika sahafu hii kuhusu lile nililoliita “dubwasha” na ambao wengi
nchini wanaliita “the system”.
Huu ni mfumo usio rasmi wenye
kuwaunganisha walio kwenye Usalama wa Taifa na vyombo vingine vya
usalama na ulinzi pamoja na wahafidhina wa CCM. Waliomo humo ndio
wanaojiona kuwa ni wao wenye haki na dhamana ya kuiendesha, na kwa dhana
yao, kuilinda Tanzania. Huo ndio undani wa siasa za kwetu.
Mantiki inatuambia kwamba ikiwa
“system” imeamua kuwa haitokubali CCM kishindwe katika uchaguzi
Zanzibar, basi pia haitokubali CCM ishindwe Bara. Haitokubali kwa sababu
ya kuhofia kwamba upinzani ukishinda na ukaruhusiwa ushike madaraka ya
taifa zima hautozivumilia siasa za kijinga zinazoendeshwa Zanzibar na
wenye kutumia nguvu za dola kubakia madarakani.
Tutaziona nguvu hizo zikizidi
kutumika tunapoukaribia ule uitwao uchaguzi wa marudio unaotarajiwa
kufanywa Machi 20. Kuna ishara mbaya. Wale waitwao “mazombi” wanaendelea
na mashambulizi yao kwa raha zao na wapinzani wanatishwa.
Ninavyoandika haya kuna mpinzani
mmoja aliye nje kwa dhamana baada ya kushikiliwa na polisi. Anatuhumiwa
kutoa video yenye kumtukana Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein. Kamishna Msaidizi wa Polisi Zanzibar, Salum Msangi, wiki
iliyopita alisema kuwa Jeshi la Polisi linakusudia kuwahoji watu 34, kwa
kuitumia mitandao ya kijamii kuwatukana viongozi wa kitaifa, jambo
ambalo ni kinyume cha sheria na maadili ya Wazanzibari.
Aliyoyasema Msangi ni sawa sawa.
Matusi ni kinyume cha ustaarabu wetu, akitukanwa kiongozi au mwananchi
wa kawaida. Na hatua ya kuwafikisha watuhumiwa mbele ya mahakama ni sawa
ilimradi isiwe kisingizio cha kuwatia adabu wapinzani.
Kadhalika asilisahau lile bao
jeusi kwenye maskani maarufu ya CCM ya Kisonge ambalo mara kadha wa
kadha limekuwa na maandishi ya uchochezi, chuki na matusi dhidi ya
viongozi wa CUF na hata wa CCM.
Kwa muda mrefu, kumekuwa na
shutuma kwamba CCM, kupitia serikali zake, kimekuwa kikilitumia jeshi
kuwatishia wakazi wa Zanzibar. Hii ndiyo sababu inayowapa watawala wetu
jeuri ya kuthubutu kufanya walitakalo na ndiyo inayowafanya wawe na
kibri. Wanatambua kwamba wanao wa kuwalinda.
Labda wenyewe hawajui kuwa
matamshi yao na lugha wanayoitumia ni ya vitisho. Hamna shaka kuwani ya
vitisho ela safari hii, kwa nionavyo, wananchi wamekuwa sugu,
hawatishiki tena. Na hapo ndipo penye hatari.
Na hatari inazidi kuwa kubwa kwa
vile watawala wetu hawaoneshi kama wamejifunza kitu. Wanajifanyia mambo
utadhani wao ni watoto wa kambo wa Adolf Hitler, yule dikteta wa
Ujerumani aliyekuwa na sera za kibaguzi, aliyetawala kwa mabavu na
aliyesababisha vifo visivyosemeka.
Kwa hali hiyo wapinzani wa Bara
wasihadaike wakafikiri kwamba viongozi wa CCM wa huko kwao ni tofauti na
wale wa Zanzibar. Wote ni “dugu moja”. Kwa hivyo, kuna haja ya
wapinzani wa Bara kuyaangalia yanayojiri Zanzibar kwa makini, wayaone
kuwa kama ni somo kwao, tena somo kubwa, katika harakati zao za kuleta
mabadiliko.
Hii huzuni iliyotanda sasa
Zanzibar inaweza ghafla tukashtukia imehamia Bara. Watawala ndio
walewale, mbinu zao ndizo zilezile na maadui zao ndio walewale — haki,
uwazi na ukweli.
CHANZO: RAIA MWEMA
No comments:
Post a Comment