Headlines News :
KARIBU CUF DIASPORA NETWORK - CUF HAKI SAWA KWA WOTE...TEGEMEA KILA JIPYA NA ZURI KUTOKA KWETU...LIKE PAGE YETU KWENYE FACEBOOK
Home » » Kituko cha Sheha na dada yangu

Kituko cha Sheha na dada yangu

Na Rashid Abdallah

Muda ukifika katika makala hii, nitakueleza kisa kimoja kilichotokea wakati watu wanajiandaa kuingia katika uchaguzi wa mwaka 2000, kinachomuhusu Sheha wa shehia yetu na dada yangu, ni kisa, kituko, tukio la kustaajabisha.

Alhamisi ya wiki hii, chama cha Conservatives kilikua na upinzani mkali dhidi ya Labour lakini mwisho wa siku Waziri mkuu wa nchi hiyo David Cameron akawa mshindi wa kiti cha kuongoza taifa la Uingereza kupitia chama chake cha Conservatives. David Cameron amechaguliwa kwa awamu ya pili na ushindi huo umekuja baada ya kushinda viti 323 alivyohitajika kushinda.


Wakati uchaguzi mkuu wa Uingereza unafanyika, wale ambao walizoea sheha na janjaweed , kwani watu wanaotoka nchi za jumuia ya madola nao walipata bahati ya kupiga kura, Wazanzibari waiwemo kwa jina la Watanzania, yupo Mzanzibari mmoja anayeishi Uingereza aliandika kupitia mtandao wake wa kijamii kuwa hakuwaona Masheha wala janjaweed, yaani anakusudia kuwa hakuna usumbufu kabisa wa masheha wala janjaweed wanaopiga kura zaidi ya mara moja tena katika vituo tofauti.

Si-chochote kwangu David Cameron kushinda, huenda hakunisaidii lolote mimi kushindwa au kushinda kwake! Kinachonipendeza ni mifumo yao ya upigaji kura, kuanzia mwanzo hadi mwisho. Yaani hakuna usumbufu wakati na hata kabla ya kupiga kura, hakuna wizi, hakuna watu kupigwa na udanganyifu, hicho ndicho kinachonipendeza.

Kwani ndio tofauti kubwa yetu sisi na wao, kwetu sisi si hivyo, hakufanyiki uchanguzi kwa salalama na amani, kukifanyika uchaguzi kwetu sisi basi jeshi linatolewa kwenye kambi na kuja uraiani, na askari wenye likizo wanarudishwa kwenye vituo ili waje wawashugulilike raia, kama vile kuna vita Zanzibar, kumbe ni uchaguzi tu.

Hilo halitoshi, kunaanzishwa pia makundi ya vijana wafanya uhalifu, hao hupiga kura hata mara sita wanapiga kura kituo hichi wanaondoka wanaenda kupiga kura kituo chengine, pia niwachafuzi wazuri wa amani, wanapora, kuiba, kuharibu kisha wanatoweka, kinachofuata vyombo vya dola vinakuja kuumiza raia wa eneo lile.

Historia ya chaguzi Zanzibar ni mbaya sana, ni kama vile nchi imeingia katika vita na wala si uchaguzi wa siku kidogo ukamaliza, wanaoshika dola hawakubali hadi wamwage damu, hili linakuja pale ambapo wameshindwa, wanachofanya ni kutumia nguvu kwa kuvitumia vyombo vya dola kubaki madarakani.

Vipindi vyote vya uchaguzi huwa vinagubikwa na ushenzi, wizi, vitendo vya uvunjifu wa amani na mambo mengine mengi, wizi si ule tu wa kupora maduka ya watu, lakini wizi mkubwa ni ule wa kura ambao hufanyika, yaani aliyeshindwa huwekwa kuwa ndio mshindwa na mshindwa akawa mshindi.

Uchaguzi wa Nigeria ulitoa funzo zuri sana kwa chaguzi nyingi za Afrika, nazungumzia hasa nyumbani Zanzibar nikujuako, ukweli wa mambo ni kuwa kila muhula wa chaguzi, chama cha CCM kinashindwa lakini hakijwahi kukubali kama tumeshindwa na kuwaachia nchi walioshinda.

Kwangu mimi haki ndio jambo la msingi, chama chochote ambacho kitashinda hata kiwe CCM basi ndio kiwe na haki kuwepo madarakani, lakini sio kubaki madarakani kwa njia za udanganyifu. CCM wanabaki madarakani kwa njia za udanganyifu, ubabe, wizi, ulaghai na mengine mengi wanayoyafanya ili kubaki madarakani.

Hayo yanathibitishwa na wana-CCM ambao walikuwa katika chama hicho, mwisho wakakihama kutokana na sera zake mbovu, wakikiacha chama hicho basi mbarika hualika, kwani husema ukweli juu ya jinsi gani CCM inapata ushindi wa kupora. Wana-CCM hao wakongwe wanakiri kuwa kura zinaibiwa, tena nyingi sana, hadi CCM ikapata ushindi wa kupora.

Hata Maalim Seif mwenyewe anajua kuwa uraisi anaporwa, amedhihirsha hilo juzi na kunukuliwa na vyombo mbali mbali vya habari kuwa , safari hii hatokubali kunyang’anywa urais wa Zanzibar kama ilivyozoeleka katika chaguzi zilizopita.

Maalim amenukuliwa akisema kuwa, Chama cha Wananchi CUF kimekuwa kikishiriki uchaguzi mkuu tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa na kushinda chaguzi hizo zilizopita, lakini hakipewi ushindi

Kazi ya kuhakikisha CCM inabaki madarakani huanza chini kabisa, huenda hadi katika tume ya uchaguzi mwisho hutangazwa ndiye aliye siye, kila hatua hutumika mbinu zisizo halali za kuhakikisha CCM inabaki madarakani, mbinu zipo hadi hata kabla ya uchaguzi.

Ninaye Dada yangu ambaye si wakuzaliwa ni mtoto tu wa Shangazi yangu, katika mtaa wetu kabla hajaondoka, alipokuwa anaamka asubuhi na kushika ufagio kwa ajili ya kufanya usafi, basi hufagia pia uwanja wa nje wa nyumba yao, wakati anapofagia uwanja huo pia hufagia uwanja wa nyumba ya Sheha. Nyumba ya Sheha na yoa ni jirani kiasi ambacho hata viwanja vya nyumba zao vimeingiliana.

Lakustaajabisha ilipofika wakati wa kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa October mwaka 2000, dada yule alipokwenda kwenye kituo cha kujiandikisha, Wallah Sheha yule yule alisema kuwa hamfahamu, yaani hamjui kabisa, wakati kila siku akimka anamuona akifagia hadi uwanja wake yeye Sheha, mwisho wa siku akakosa kujiandikisha kwa awamu ile.

Hilo ni moja tu kati ya mengi ambayo hutokea, lengo la mambo haya ni kukwamisha watu wasipate haki yao ya kupiga kura, kwakuwa Sheha anakujua tu wewe si wa chama chake basi hata kupata haki ya kupiga kura anaweza kukukosesha ama ukapata usumbufu wa kutosha, mambo hayo bado yanaendelea hadi kesho Zanzibar.

Ukitafsiri uchaguzi huru na haki au uchaguzi wa kidemokrasia, kwa mfano wa matukio kama haya, kunaingia doa jeusi juu ya demokrasia iliyopo katika uchaguzi wa namna kama hii, kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Miaka yote uchaguzi unalalamikiwa kuwa hauko huru na wala si wahaki, hauko huru kwani baadhi ya watu yanawakumba kama yale yaliyomkumba dada yangu, sheha unayeishi kijiji kimoja ukienda kwenye kituo cha kupiga kura au kujiandikisha anakukataa, lakini anaweza kuwa hana pingamizi kwa mtu ambaye ameletwa kutoka mbali na Chama tawala ili aje aongezee idadi ya kura.

Lakusikitisha ni kwamba hata wale waangalizi wa kimataifa, sijui hawajui kuwa haki haitendeki au wanavaa miwani ya mbao ili wasione kusudu, mara nyingi wanaoletwa ni wale wale, ukimleta Mkurunzinza aangalie uchaguzi kweli atapeleka ripoti ya kuwa uchaguzi haukiwa huru na haki?

Nimealizie kwa kusema kuwa uchaguzi ukiwa unakaribia, basi serekali yetu ijitahidi kuweka haki kwa wote na kuhakikisha kila anayestahiki kuwa na haki basi anaipata, tusiendeshane kwa chuki za vyama, tuendeshane kwa haki. Hasara ya kuunyima haki umma huenda ikawa ni kubwa na mbaya kuliko ile faida ya kukaa Ikulu.

Uchaguzi wa Uingereza, usitufurahishe tu kuwa umeenda vizuri, lakini ni lazima serekali zetu ziige kutoka kwao, Waingereza wanaporidhika na uchaguzi walioufanya basi na hata Wazanzibari wanastahiki kuridhika na uchaguzi wanaoufanya sio kuleteana magumashi. Ni hatari!

Chanzo: Mzalendo
Share this article :

No comments:

Post a Comment

 
Support : ZENJIBARZA
Copyright © 2011. ACT WAZALENDO DIASPORA NETWORK - All Rights Reserved