Wakati sintofahamu ya hali ya kisiasa Zanzibar ikiendelea, aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amejitoa kwenye mazungumzo ya maridhiano yaliyokuwa yakiendelea visiwani humo, Nipashe inaripoti.
Mpaka sasa Maalimu Seif, Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein, marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Dk. Salmin Amour Juma, Amani Abeid Karume na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, wameshakutana mara tisa kwa nyakati tofauti katika vikao hivyo ambavyo vilikuwa vimetawaliwa na usiri mkubwa.
Itakumbukwa pia kuwa, hivi karibuni Maalimu Seif alikutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kueleza kutoridhishwa na namna ambavyo mazungumzo hayo yalikuwa yakiendelea na badala yake kumtaka Rais John Magufuli kuingilia kati mzozo huo wa kisiasa ulioibuka baada ya uchaguzi mkuu Zanzibar uliofanyika mwaka jana kufutwa na matokeo yake.
AKUTANA NA LOWASSA, VIONGOZI UKAWA
Taarifa ambazo Nipashe ilizipata jana zilieleza kuwa, Maalimu Seif alisafiri kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam na kukutana na viongozi wakuu wa Ukawa wakiongozwa na aliyekuwa mgombea wa urais wa umoja huo kupitia Chadema, Edward Lowassa na kuweka msimamo wa kutoendelea na mazungumzo hayo kwa madai kuwa hayana nia njema ya kumaliza mzozo uliopo visiwani humo.
Habari ambazo gazeti hili ilizipata zilisema, viongozi hao walikutana kwenye ofisi za umoja huo (Ngome), zilizoko Kawe, wilayani Kinondoni.
Viongozi wengine walioshiriki kwenye kikao hicho ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Kaimu Mwenyekiti wa CUF Taifa, Twaha Taslima na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), Prof. Mwesiga Baregu.
Chanzo chetu kutoka ndani ya kikao hicho kilisema: “Maalimu Seif aliwaeleza wenzake kwamba kwa sasa hataendelea na mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea Zanzibar kwa sababu ameona hayana tija.”
WAPANGA MIKAKATI
Chanzo hicho kilieleza kuwa, baada ya Maalimu Seif kutangaza kujiweka kando na mazungumzo hayo, iliamuliwa njia iliyobaki ni kuweka shinikizo la kitaifa na kimataifa ili mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana atangazwe.
“Siku yoyote kabla ya Bunge kuanza, Maalimu Seif na viongozi wengine wa Ukawa watasafiri hadi Dodoma kukutana na wabunge wao ili kuwaeleza hali ya Zanzibar ilivyo na namna ya kuingia nayo Bungeni,” kilieleza chanzo hicho.
Kilieleza pia kwamba, katika mkutano na wabunge hao wa Ukawa, watajadili namna ya kuendesha siasa zao ndani ya Bunge na nje ili kujipanga na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Januari 11, mwaka huu, Malimu Seif alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuwaeleza kuwa haridhishwi na mazungumzo hayo, akidai wenzake wanaokana kuendelea kung’ang’ania kurudiwa kwa uchaguzi jambo alilosema haamini kama litaleta suluhu kwenye mgogoro wa Zanzibar na kumtaka Rais Magufuli kuingilia kati.
Wakati Maalimu Seif akionyesha kuwa tumaini lake lililokuwa limebaki ni Rais Magufuli, Januari 12, Rais Shein alilizika pale alipoweka msimamo wa kurudiwa kwa uchaguzi huo mbele ya Rais Magufuli na marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, akiwamo Balozi Seif Idd Ali, ambao pia ni wajumbe wa mazungumzo hayo.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Shein, alisema uchaguzi wa marudio utafanyika chini ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) na kuwataka wananchi kuwa watulivu wakisubiri tume hiyo itangaze tarehe ya kufanyika uchaguzi huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment