HOJA NA MAJIBU: UBATILI WA MKUTANO MKUU WA CUF.
Na. Mtatiro J
1. HOJA:
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF kutoka Zanzibar walikuwa wengi kuliko wale wanaotoka Tanzania bara?
MAJIBU:
(i) Siyo kweli, tangu Chama Cha Wananchi CUF kimeanzishwa, Tanzania Zanzibar haijawahi kuwa na Wajumbe wengi kwenye Mkutano Mkuu au Baraza Kuu kuliko Tanzania Bara. Katika Mkutano Mkuu wa juzi tarehe 21 Agosti 201,6 Wajumbe halali wa Mkutano huo kwa mujibu wa katiba walikuwa ni 804. Kati ya hao, wajumbe 429 sawa na 53.3% walipaswa kutoka Tanzania Bara na wajumbe 375 sawa na 46.7% walipaswa kutoka Zanzibar.
(ii) Wajumbe waliohudhuria mkutanoni PHYSICALLY na kusaini fomu za mahudhurio na za fedha za posho ni wajumbe 327 kutoka Bara ambao ni sawa na asilimia 76.2 ya wajumbe wote wa Bara huku wajumbe wa Zanzibar walikuwa ni 351 sawa na asilimia 93.6 ya wajumbe wote wa Zanzibar. Kwa ujumla Bara + Zanzibar walikuwa wajumbe 678 ambao ni sawa na asilimia 84.3 ya wajumbe wote halali wa Mkutano Mkuu.
(iii) Kwa hiyo, asilimia 23.8 ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kutoka Tanzania Bara hawakuhudhuria mkutanoni kabisa, pamoja na kujulishwa kupitia vyombo vya habari, ujumbe mfupi wa simu, kupigiwa simu na kuandikiwa barua kuwa wanapaswa kufika mkutanoni. Vivyo hivyo, asilimia 6.4 ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kutoka Zanzibar hawakuhudhuria mkutanoni pamoja na kuwa walijulishwa kwa njia zote za mawasiliano ndani ya chama.
2. HOJA
Je, Mkutano Mkuu wa CUF ulifikisha akidi ya kufanya maamuzi?
MAJIBU
(i) Ndiyo, Mkutano Mkuu wa CUF ulifikisha akidi ya kuanza kikao na kufikia maamuzi yoyote. Kwa mujibu wa ibara ya 77 (5) ya Katiba ya CUF toleo la mwaka 1992 na marekebisho ya mwaka 2014 (nanukuu) “Mkutano Mkuu wa Taifa utakuwa halali iwapo zaidi ya nusu ya wajumbe wake kutoka Tanzania bara na zaidi ya nusu ya wajumbe wake kutoka Zanzibar watahudhuria” (mwisho wa kunukuu).
(ii) Wajumbe wote wa Bara ni 429 na kwa hiyo nusu inayohitajika ili kuhalalisha mkutano ni 215, kwa bahati nzuri waliofika mkutanoni kutoka BARA ni wajumbe 327 ambao ni wajumbe 100 zaidi ya nusu inayotakiwa, kwa hiyo akidi ya upande wa bara ilitimia na kuzidi.
(iii) Wajumbe wote wa Zanzibar ni 375 na kwa hiyo nusu inayohitajika ili kuhalalisha mkutano ni 188, kwa bahati nzuri waliofika mkutanoni kutoka Zanzibar ni wajumbe 351 ambao ni wajumbe 100 zaidi ya nusu inayotakiwa, kwa hiyo akidi ya upande wa Zanzibar ilitimia na kuzidi.
3. HOJA
Je, maamuzi yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa CUF wa juzi ya KUKUBALI KUJIUZULU kwa Prof. Lipumba ni halali kikatiba?
MAJIBU
(i) Ndiyo, kwa mujibu wa Ibara ya 77 (6) ya Katiba ya CUF (nanukuu) “Maamuzi yatakayofanywa na Mkutano Mkuu wa Taifa yatahesabiwa kuwa maamuzi halali ikiwa zaidi ya nusu ya wajumbe waliohudhuria watayaunga mkono” (mwisho wa kunukuu).
(ii) Wajumbe waliounga mkono azimio la KUJIUZULU kwa Prof. Lipumba (KUMUONDOA RASMI) ni 476 ambao ni sawa na asilimia 70.2 ya wajumbe wote waliohudhuria. Wajumbe waliokataa kujiuzulu kwa Prof. Lipumba (KUTAKA AENDELEE NA UENYEKITI) ni 14 sawa na asilimia 2.06 ya wajumbe wote waliohudhuria. Wajumbe ambao hawakupiga kura (walikataa kunyoosha mikono) ni 188 ambao ni sawa na asilimia 27.7 ya wajumbe wote waliohudhuria mkutano.
(iii) Kwa mantiki hiyo, kura 476 zilizoamua kuwa LIPUMBA AMEJIUZULU zilitimiza matakwa ya kikatiba ya kutaka yaungwe mkono na zaidi ya nusu ya wajumbe waliohudhuria. Nusu ya wajumbe waliohudhuria (50%) ilipaswa kuwa 339, kwa hiyo kura 476 (70%) zilikidhi masharti ya katiba na kufanya maamuzi ambayo ni halali na hayawezi kupingwa kokote.
4. HOJA
Je, utaratibu uliotumika kufanya uamuzi wa KUMUONDOA au KUMBAKISHA Lipumba ulipaswa kufanywa kwa kura ya siri? Na kwamba kura za kunyoosha mkono zilizotumika ni kinyume na katiba ya CUF?
MAJIBU
(i) Siyo kweli kwamba uamuzi wa kumuondoa Lipumba ulipaswa kufanywa kwa kura ya siri. Wanaosema hivyo aidha hawaijui hawa hawajaisoma katiba ya CUF kabisa. Kwa mujibu wa Katiba ya CUF ibara ya 115 (3) (nainukuu) “Katika shughuli za uchaguzi wowote ule kura zitakuwa za siri”. Ibara hii inamaanisha “Uchaguzi” kwa kiingereza “Election” haiongelei “Uamuzi” kwa kiingereza “Decision”.
(ii) Mkutano Mkuu wa Blue Pearl wa juzi ulikutana kufanya uamuzi wa kukubali au kukataa kujiuzulu kwa Lipumba (hapa nazungumzia ajenda ya KWANZA ya mkutano), mkutano ule katika ajenda hiyo ya kwanza haukuwa na jukumu la kufanya UCHAGUZI (ELECTION). Ajenda ya Uchaguzi “election” ilikuwa ni ya PILI ambayo haikuendelea baada ya mkutano kuahirishwa na kama tungeifikia ajenda hiyo ndipo kura zingefanywa kwa siri.
(iii) Kwa mantiki hiyo, maamuzi yote ya kawaida kama vile kukubali kiongozi kujiuzulu, kupendekeza na kumthibisha mwenyekiti wa muda, kupitisha Katiba ya CUF n.k. yanafanywa aidha kwa kuwahoji wajumbe au kwa kuhesabu wingi au uchache wao wakiwa wamenyoosha mikono juu. Ni jambo la ajabu sana kudhani kuwa “kuthibisha” au “kuazimia” jambo fulani kwenye vikao hufanywa kwa maboksi ya kura na kura za siri. Suala la kukubali au kukataa kujiuzulu kwa Lipumba halikuwa Uchaguzi “election”.
Mtatiro J
#NOTE; Baba yangu amekuwa akinisisitiza, "mwanangu watafute sana ELIMU, MAARIFA, AKILI na UTARATIBU TULIOJIWEKEA". Ikiwa watu hawataongoza na Elimu, Maarifa, Akili na Utaratibu waliojiwekea watu hao ni sawa na vipofu wasiojua wanakokwenda na ipo siku watapigwa kwa fimbo moja na kutawanyika kwa sababu hawana mchungaji mwema na tena wamekata kujiongoza kwa taratibu zao. Huko kwa msajili wa vyama ni kupoteza muda, someni katiba zenu ambazo mnazo, msiongozwe na VIPOFU.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Popular Posts
- CUF wamuandikia barua Mwenyekiti wa ZEC
- TAMKO LA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA JUU YA KUTEKWA KWA MWANDISHI WA HABARI WA SAUTI YA UJERUMANI ( DW ) SALMA SAID.
- Sera ya kunena na Kutenda ya Wana CUF
- (no title)
- Ufungaji wa Kampeni ya uchaguzi mdogo wa Dimani.
- Salam kwa Mkururinza wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment