29 Aprili. 2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nchi yetu Zanzibar imekumbwa na mvua kubwa zinazoendelea kusababisha madhara kwa maeneo mengi ya visiwa vya Unguja na Pemba. Mvua hizo zinazonyesha katika maeneo yote ya nchi yetu zimesababisha athari mbalimbali ikiwemo kupotea kwa baadhi ya roho za wananchi wenzetu kutokana na athari zake. Kwa mfano, mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 17 Aprili, 2016 zilisababisha kifo cha Ndugu Salim Mohamed Ahmed (61) mkaazi wa Migombani kutokana na kuangukiwa na ukuta uliomong’onyolewa na mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia siku hiyo.
Mvua hizo zilizofikia kiwango cha milimita 212.4, kama ilivyotangazwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kanda ya Zanzibar, zimepelekea, mbali na kuharibu kabisa miundombinu ya barabara, kuathirika pia maeneo yanayotumika kwa ajili ya kutolea huduma kwa wananchi. Moja ya maeneo hayo ni hospitali ya wagonjwa wenye matatizo ya akili ya Kidongochekundu ambayo ililazimika kusitisha huduma zake kutokana na kujaa kwa maji ya mvua katika maeneo ya majengo yake kama vile jengo la Block D na Block F.
Aidha, taarifa zinaonesha kuwa zaidi ya nyumba mia tisa (900) ambazo ni makaazi ya watu zimeingiliwa na maji na kusababisha athari mbalimbali ikiwemo kubomoka kwa nyumba hizo na kupelekea wamiliki wa nyumba hizo kuhama na kutafuta hifadhi kwa ndugu na jamaa zao. Miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi ni: Jang’ombe, Nyerere, Sebleni, Sogea, Karakana, Kwahani, Mpendae, Miembeni, Gulioni, Makadara, Meya, Migombani, na Kwaalinato kwa upande wa Wilaya ya Mjini Unguja.
Kwa upande wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ maeneo yaliyoathirika ni pamoja na Mwanyanya kwa Goa, Bububu, Welezo, Mwera, Mtofaani, Mtopepo, Mtoni Kidatu, Kihinani, na Kibweni. Maeneo yaliyoathirika kwa Wilaya ya Magharibi ‘B’ ni Mwanakwerekwe, Tomondo, Mombasa, Fuoni Kibonde Mzungu, Pangawe, Kinuni, Kisauni, Kiembesamaki na Meli nne.
Kiwango hichi kikubwa cha mvua kuwahi kushuhudiwa hapa Zanzibar kimepelekea kutifuka kwa miundo mbinu ya maji machafu na kuathirika vibaya kwa mfumo wa kuhifadhia na kusafirishia maji machafu hasa katika maeneo tuliyoyataja kukumbwa na mvua zinazoendelea. Hadi sasa maeneo tuliyoyataja yamezungukwa na kiasi kikubwa cha maji machafu yaliyochanganyika na mkusanyiko wa takataka za kila aina ikiwemo masalia ya uchafu wa kimaumbile wa viumbe mbalimbali. Hali hii imepelekea kushamiri na kuongezeka kwa kasi kubwa kwa maradhi ya mlipuko ya ugonjwa wa kipindupindu yaliyoanza mwezi Machi, 2016.
Kwa mujibu wa taarifa tulizozipokea hapa katika ofisi zetu za Makao Makuu, kama zilivyotangazwa na Mamlaka mbalimbali za Zanzibar kama vile Mkurugenzi wa Idara ya Kuzuia na Kupambana na Maradhi Zanzibar (Director of Disease Prevention and Control) Muhammed Dahoma, maradhi haya thakili ya kipindupindu yamesababisha vifo vya zaidi ya watu thamanini (80) na wengine zaidi elfu tatu (3,000) wamelazwa katika maeneo maalum ya makambi ya wagonjwa wa maradhi hayo.
Kutokana na maradhi haya, Mamlaka za Zanzibar, ikiwemo viongozi wa kisiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamepiga marufuku uuzwaji wa vyakula na vinywaji vya aina zote katika maeneo ya wazi, kuanzisha makambi katika visiwa vya Unguja na Pemba ambamo wagonjwa wa kipindupindu huwekwa na kutengwa na kufungwa kwa skuli za madarasa ya awali na msingi kwa kipindi kisichojulikana.
Mbali na watendaji wa Malaka zilizopewa jukumu la kusimamia kazi ya kuhakikisha matangazo hayo yanasimamiwa kujinufaisha binafsi na kutekeleza jukumu hilo kwa uonevu na udhalilishaji, taarifa zinaonesha kuwa kumekuwepo na kasi ndogo na utekelezaji usiozingatia vigezo vya kitaalamu katika kutoa huduma kwa wahanga waliokusanywa katika maeneo ya wagonjwa wa kipindupindu kutokana na kukosekana kwa nia njema ya kukabiliana na kupambana na maradhi hayo kwa kuwatibu waathirika kutokana na kukataa kukiri kwa mamlaka hizo kukosa uwezo wa vifaa na utaalamu.
Aidha, uamuzi wa kufungwa kwa skuli za awali na skuli za msingi kama njia ya kukabiliana na maradhi ya kipindupindu unaonekana kuchukuliwa kwa kufuata mawazo yaliyojengwa kwa hamasa na kuamuliwa kwa haraka bila ya kuzingatia athari zake kwa sekta ya elimu Zanzibar. Bila ya chembe ya shaka, maradhi ya kipindupindu ni hatari kwa mustakbali wa wananchi wa rika zote katika nchi yetu, hata hivyo haikubaliki kuchukua hatua ya kufunga skuli na kuwakosesha watoto wetu haki yao ya msingi ya kupata elimu katika kipindi kisichojulikana bila ya kushughulikia msingi wa matatizo na chanzo cha maradhi ya kipindupindu kwa Zanzibar.
Ni busara kwa waliotoa tangazo la kufungwa kwa skuli kuzingatia mustakbali wa sekta ya elimu zanzibar kutokana na tangazo hilo. Katika kufanya hivyo wanapaswa kuzingatia idadi za siku za mapumziko kwa mujibu wa kalenda ya Wizara ya Elimu Zanzibar, urefu wa mitaala ya Elimu, na idadi ya siku za masomo kwa wanafunzi wa Zanzibar. Bila ya shaka, kwa kuzingatia vigezo hivyo watabaini athari za tangazo lao hilo la kufunga skuli za Zanzibar kwa muda usiojulikana kwa mustakbali wa sekta ya elimu Zanzibar bila ya kuwepo mikakati madhubuti miongoni mwa Mamlaka nyengine za kupambana na maradhi ya kipindupindu yanayojirudia kila uchao.
Kwa upande mwengine, tangu kutokea kwa mafuriko ya mvua kwa mwaka huu na kushadidi kwa maradhi ya kipindupindu, kumekuwepo na mlolongo wa ahadi nyingi kutoka kwa wanasiasa wa CCM, akiwemo Dr. Ali Mohamed Shein, Balozi Seif Ali Idd na Mohamed Aboud, kwa wananchi waliopatwa na mitihani ya mafuriko. Sisi katika CUF-Chama Cha Wananchi tunaamini kuwa ahadi hizi za wanasiasa hawa, waliojiweka madarakani bila ya ridhaa ya wananchi, ni ahadi hewa ambazo kimsingi hawana nia wala uwezo wa kuzitekeleza na kwa hakika zimelenga kuwahadaa wananchi hao ili kupunguza ghamidha za wananchi wa Zanzibar dhidi yao kutokana na matendo ya wanasiasa hao kusaliti maamuzi ya wazanzibari na kuzima sauti zao walizozitoa kwa njia za kidemokrasia tarehe 25 Oktoba, 2015.
Kutokana na muktadha wa kukosekana insafu na nia njema ya kukabiliana na kuwaondolea matatizo yanayowakabili wananchi wanyonge wa Zanzibar na mfululizo wa ahdi kemkem za viongozi walioweka mbele maslahi yao binafsi na kuwahadaa wananchi kwa malengo tuliyoyataja hapo juu:
1. CUF-Chama Cha Wananchi Kinaendelea kuwasisitiza wananchi wote wa Zanzibar kuendelea kushikamana na kusaidiana, kwa kuzingatia hali halisi ya zanzibar kwa sasa, kwa kuwasaidia wananchi wenzao waliokumbwa na maafa ya kukosa makaazi kutokana na kuharibikiwa na nyumba na mali zao kwa kuendelea kuwapatia hifadhi katika nyumba zao, na kuendelea kuwa karibu na wanafamilia za wananchi waliopoteza ndugu zao kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha kwa kuwafariji na kuwaombea dua marehemu wetu wote waliotangulia mbele ya haki ili Mwenyezi Mungu mtukufu azilaze roho zao mahali pema peponi na kuwaombea wanafamilia hao kuwa na moyo wa subira.
2. CUF-Chama Cha Wananchi kinatoa wito kwa Mamlaka zinazohusika na maafa, ikiwemo idara ya maafa Zanzibar, kuweka utaratibu mzuri unaoeleweka katika kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali iliyokwishafanyika miaka mingi iliyopita ili kumaliza tatizo la miaka mingi la mafuriko ya maji na mvua katika miji ya Zanzibar linalojirudia kila baada ya kipindi kifupi cha muda. CUF inaamini kuwa kwa kutumia kwa vitendo mipango na mikakati iliyoandaliwa kwa gharama kubwa na iwapo kutakuwa na umakini na utayari wa hali ya juu miongoni mwa watendaji wa idara hizo, tatizo la mafuriko kwa maeneo sugu ya Zanzibar yanayokabiliwa na matatizo hayo litapungua na hatimaye kumalizika kabisa.
3. Kutokana na kuamini na kuthamini maisha ya kila mwananchi wa nchi hii, bila ya kujali uwezo wake wa fedha, asili yake, na itikadi yake ya kisiasa, CUF-Chama Cha Wananchi kinazizindua Mamlaka zilizoaminiwa na kupewa jukumu la kuhami maisha ya wananchi wa nchi hii, ikiwemo Baraza la Manispaa Zanzibar, kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mpango wa kudhibiti maji ya mvua na mfumo wa maji taka kwa azma ya kuwaepusha wanajamii ambao wao ni sehemu yake. CUF inatoa wito wa utekelezaji, kwa vitendo, wa Master Plan kwa mji wa Zanzibar ili kufumua mfumo wa maji taka uliopitwa na wakati na kuweka mfumo wa kisasa wa ukusanyaji, ukaushaji na uhifadhi wa maji taka kwa maeneo yote ya Zanzibar.
4. CUF-Chama Cha Wananchi kinawanasihi wanasiasa wa Zanzibar kuacha mara moja kuwadhihaki wananchi wenye matatizo na kutumia matatizo hayo kuwafanyia tashtiti na kuwapa ahadi kemkem bila ya dhamira ya dhati ya kutekeleza ahadi hizo. CUF inawatanabahisha wanasiasa wote kuwa wananchi wa Zanzibar wameerevuka vya kutosha na katu hawatakubali tena kutumika kuwanufaisha wanasiasa wa hovyo hovyo walioweka mbele maslahi yao na familia zao na kuwasahau wananchi kwa kupuuza na kudharau sauti zao na matakwa yao.
HAKI SAWA KWA WOTE
NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU CUF ZANZIBAR
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Popular Posts
- CUF wamuandikia barua Mwenyekiti wa ZEC
- TAMKO LA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA JUU YA KUTEKWA KWA MWANDISHI WA HABARI WA SAUTI YA UJERUMANI ( DW ) SALMA SAID.
- Sera ya kunena na Kutenda ya Wana CUF
- (no title)
- Toleo la Annur June 23
- Ufungaji wa Kampeni ya uchaguzi mdogo wa Dimani.
- Salam kwa Mkururinza wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment