TAARIFA KWA UMMA
Leo, Alkhamis tarehe 6 Aprili, 2017 Katibu Mkuu wa The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi), Maalim Seif Sharif Hamad, amefanya mahojiano maalum (exclusive interview) na taasisi ya Utangazaji ya Marekani (Voice of America) kupitia vituo inavyovimiliki: kituo cha redio cha sauti ya America (VOA) na kituo cha televisheni cha Voice of America (VOA).
Mahojiano hayo maalum yaliyofanyika nyumbani kwa Maalim Seif Sharif Hamad, Chukwani Mjini Unguja, mapema asubuhi ya leo yalilenga kuangazia mambo mbali mbali katika mwenendo wa siasa na uendeshaji wa Mamlaka za nchi ikiwa ni pamoja na hali ya kisiasa nchini, msimamo wa CUF juu ya utawala wa Zanzibar, na mgogoro wa kiuongozi katika CUF.
Aidha, mahojiano hayo yaliangazia kufanikiwa kwa juhudi za CUF katika kulitafutia ufumbuzi suala la mgogoro wa kisiasa Zanzibar na mipango ya CUF kuwatumikia wananchi muda mfupi baada ya kukabidhiwa hatamu za Dola kufuatia juhudi zinazoendelea za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaotokana na kufutwa isivyo halali kwa Uchaguzi Mkuu wa 25 Oktoba, 2015.
Akijibu maswali kuhusu hali ya kisiasa nchini, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kwamba hali ya kisiasa nchini si shwari kutokana na mzozo uliopo kufuatia kutokuheshimiwa kwa maamuzi ya wananchi waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015.
Maalim ameeleza kuwa kuporwa kwa ushindi wa CUF na kikundi cha watu wachache kujiweka katika Mamlaka za nchi kwa kutumia njia na mbinu za kiharamia, huku wakitoa kauli za kibri na dharau dhidi ya matakwa ya wananchi wanaokabiliwa na hali ngumu ya maisha kunaendelea kuongeza hamasa na kuchochea vuguvugu la mabadiliko miongoni mwa wananchi wa rika zote.
Akielezea kukua na kuongezeka kwa vugu vugu hilo, Maalim Seif Sharif Hamad ametolea mfano wa idadi kubwa ya wananchi, hasa vijana, wanaojitokeza kumpokea katika ziara zake zinazoendelea katika visiwa vya Unguja baada ya kumalizika katika kisiwa cha Pemba huku wakimtaka awaachie wachukue hatua za kudai haki yao iliyoporwa kwa njia wanazozijua wenyewe.
Katika ziara hizo, Maalim Seif Sharif Hamad, akiambatana na Viongozi wenzake wa CUF wamekuwa wakipokelewa na idadi kubwa ya wananchi hali iliyopelekea Jeshi la Polisi kuingilia kati na kujaribu mara kadhaa kuzuia ziara hizo kwa kudai kuwa CUF imekuwa ikifanya mikutano ya hadhara ambayo imepigwa marufuku kufuatia amri ya Rais John Pombe Magufuli.
Mbali na mapokezi hayo, ziara za Maalim Seif Sharif Hamad zimeshuhudia wimbi kubwa la wananchi kuvihama vyama vyao, hasa wanachama wa CCM na kuamua kujiunga na CUF. Katika ziara yake ya jana tu, Jumatano tarehe 5 Aprili, 2017 katika kisiwa kidogo cha Uzi kilichopo Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, Maalim Seif Sharif Hamad alitoa kadi kwa wanachama wapya 216.
Kuhusu msimamo wa CUF kwa utawala uliopo Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesisitiza msimamo wa CUF kama taasisi kuwa haimtabui Ali Mohamed Shein na yeye binafsi akiwa ni mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia CUF, na kupewa ridhaa na wananchi wa Zanzibar kwa ushindi wa kura zaidi ya 25,000 anamchukulia Ali Mohamed Shein kuwa ni mtu aliyejiweka madarakani kwa kutumia njia haramu na nguvu za makundi ya maharamia kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji katika vyombo vya Ulinzi na Usalama, kinyume na matakwa ya Sheria na Katiba ya nchi.
Kwa upande wa mgogoro wa kiuongozi unaoikabili CUF na taswira inayojengwa kutokana na mgogoro huo kuwa CUF imegawanyika pande mbili: ile inayomuunga mkono aliyekuwa Mwenyekiti Ibrahim Lipumba na ile inayomuunga mkono yeye Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza kuwa CUF ni taasisi moja iliyochini ya Kamati ya Uongozi inayoundwa na Mwenyekiti wake Julius Mtatiro na wajumbe wake ni Severina Mwijage na Katani Ahmed Katani.
Tafauti na maadui wa CUF wanaojaribu kuonesha kuwa CUF imegawanyika sehemu mbili, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa CUF ni moja kwa kutoa mfano wa utendaji kamili wa kitaasisi uliopo baina ya Mamlaka mbali mbali za CUF kuanzia Bodi ya WADHAMINI, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ambazo zinaundwa na wajumbe kutoka sehemu mbalimbali za pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba Mamlaka zote hizo zinakutana kwa mujibu wa Katiba ya CUF, zinatekeleza wajibu wake na kusimamia maamuzi yake.
Akifafanua hoja kuwa CUF imegawika pande mbili kulingana na madai ya Utanganyika na Uzanzibari, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kwamba hoja hiyo inatolewa na maadui wa chama ili kuwaziba macho na kuwazuga baadhi ya watu na wanachama ili iwe rahisi kuwatumia kufikia malengo ya kuisambaratisha CUF, hata hivyo Maalim alisema kwamba njama hizo hazitafanikiwa kwani wanachama wa CUF nchi nzima wamefahamu nia na dhamira ya Ibrahimu Lipumba kuendelea kung’ang’ania uenyekiti wa CUF hata baada ya kujiuzulu kwa hiari yake mwenyewe na ndio maana wanachama wa CUF katika maeneo ya Tanganyika ikiwa ni pamoja na Rufiji, Ruangwa, Lindi na Tanga walimfukuza na kukataa hata kumsikiliza.
Kwa upande wa mikakati na juhudi za CUF katika kulitafutia ufumbuzi suala la mgogoro wa kisiasa Zanzibar na kuhakikisha kuwa maamuzi ya wananchi waliyoyafanya tarehe 25 Oktoba, 2015 yanaheshimiwa, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kwamba CUF inaendelea kupata uungwaji mkono wa hali ya juu na Jumuiya ya Kimataifa na kwamba Jumuiya hiyo imevutiwa sana na uamuzi wa viongozi wa CUF kutumia njia za amani na kidemokrasia kulipatia ufumbuzi suala la Zanzibar na kwamba siku si nyingi ufumbuzi utapatikana na kwamba wananchi waendelee kutulia na wasiyumbishwe na kauli za kuwakatisha tamaa na kuwavunja moyo wananchi, hasa Wazanzibari, zinazotolewa na viongozi wa CCM.
Alipoulizwa kuhusu Jumuiya ya Kimataifa, hasa Umoja wa Ulaya, kuanza upya kuipa misaada Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa msaada uliotolewa hivi karibuni na Jumuiya hiyo, kinyume na wito wa CUF kuitaka Jumuiya hiyo kusitisha misaada yake kwa Tanzania, Maalim Seif Sharif Hamad amefahamisha kuwa hakuna msaada uliotolewa kinyume na inavyotangazwa, bali kilichotolewa ni ahadi ya msaada unaofungamana na masharti maalum.
Aidha, Maalim Seif Sharif Hamad alitanabahisha kuwa misaada yote inayotolewa na Jumuiya ya Kimataifa, ikiwemo Umoja wa Ulaya huambatana na masharti mahsusi ambayo huzilazimisha nchi zinazopewa msaada huo kuyazingatia na kuyatekeleza. Akitaja baadhi ya masharti hayo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema ni uzingatiwaji wa demokrasia na uhifadhi wa Haki za Binadamu.
Kwa upande mwengine, Maalim Seif Sharif Hamad ametaja vipaumbele vyake na kuonesha mipango ya CUF katika kuwatumikia wananchi muda mfupi baada ya kukamilika kwa juhudi zinazoendelea za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaoikabili Zanzibar.
Akitaja vipaumbele vyake hivyo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kuwa elimu ndio itakuwa dira na mwelekeo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na CUF kwa kutilia mkazo elimu ya ufundi na teknolojia kwa lengo la kusimamia kwa ufanisi, umakini na urahisi sera kuu ya CUF katika uchumi wa nchi ili kuifanya Zanzibar kuwa SINGAPORE ya AFRIKA MASHARIKI.
Kwa upande wa upatikanaji wa huduma za afya, Maalim Seif Sharif Hamad amesema kwamba Serikali yake itahakikisha uwepo wa kutosha wa madaktari, dawa, vifaa tiba na wahudumu wa kutosha ikiwa ni pamoja na wauguzi na wataalamu wa kufanyia matengenezo vifaa, na mashine za hospitali na vituo vya afya.
Kipaumbe namba tatu cha Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad itakuwa ni kupambana na umasikini uliokithiri miongoni mwa wananchi. Katika kufikia malengo haya mkakati wa Maalim Seif Sharif Hamad ni kuweka sera na kuandaa mazingira bora ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika sekta mbali mbali kwa uchumi wa Zanzibar na kuimarisha kipato cha wananchi kwa kuongeza kima cha mishahara kwa kada zote za wafanyakazi hasa wafanyakazi wanaolipwa kima cha chini cha mshahara.
Baada ya kukamilika kwa mahojiano hayo maalum, Maalim Seif Sharif Hamad, aliungana na wananchi wengine wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Unguja kushiriki mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF kwa wilaya hiyo, Mheshimiwa Makungu Ame Khamis, aliyefariki usiku wa kuamkia leo Bumbwini.
Imetolewa na:
Hissham Abdukadir
Afisa Habari na Mawasiliano
CUF-Makao Makuu
Mtendeni Zanzibar
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Popular Posts
- Uchaguziwa Mwenyekiti mpya wa CUF leo
- Taarifa kwa vyombo vya habari
- (no title)
- Maalim Seif na Fimbo ya Mussa
- Kituko cha Sheha na dada yangu
- CUF Zanzibar Yamtaka Rais Magufuli Aondoshe Majeshi yake Zanzibar
- MAAAMUZI YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF - CHAMA CHA WANANCHI) KUHUSIANA NA HUJUMA ZA DOLA DHIDI YA CUF
No comments:
Post a Comment