Home »
» KIKWETE NDIO ALIEVURUGA DEMOKRASIA YA ZANZIBAR
KIKWETE NDIO ALIEVURUGA DEMOKRASIA YA ZANZIBAR
Na Ismail Jussa Ladhu; Nimesoma makala iliyoandikwa na Ndugu Deus Kibamba akimuomba Rais Dr. John Pombe Magufuli amteue mtangulizi wake, Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa msul uhishi wa mgogoro wa Zanzibar. Wakati naunga mkono kuchukuliwa hatua madhubuti za kuumaliza mgogoro huo wa uchaguzi (ambao naamini suluhisho lake ni kuheshimu maamuzi halali ya Wazanzibari waliyoyafanya kupitia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015), kabisa siungi mkono pendekezo la Ndugu Deus Kibamba kwamba eti JK ndiye apewe dhamana hiyo. Kwa vipimo na vigezo vyote, Jakaya Mrisho Kikwete hana sifa, hana uadilifu, hana uthubutu, na hana uhalali wa kushughulikia mgogoro wa kufutwa matokeo halali ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015. Kwa msingi upi ataweza kulishughulikia suala hili? Ingekuwa ni kusimamishwa kizimbani, yeye atakuwa wa kwanza. Ni yeye Jakaya Kikwete akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu ndiye aliyesimamia kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu halali ambao ulikuwa umeshamalizika.
Jeshi lisingeweza kupelekwa Hoteli ya Bwawani kulikokuwa kituo kikuu cha majumuisho ya matokeo ya uchaguzi wa Urais wa Zanzibar bila ya idhini ya Amiri Jeshi Mkuu. Kwa hakika, amejipotezea heshima kubwa ambayo angekuwa nayo kama angesimamia matakwa ya kidemokrasia ya wananchi wa Zanzibar. Badala yake akaamua kuyavuruga MARIDHIANO YA WAZANZIBARI kwa kuwakorogea uchaguzi wao uliopaswa kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoasisiwa na Dr. Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad. Hiyo ndiyo LEGACY yake kwamba anakumbukwa kwa kuichafua Zanzibar na kuiingiza katika mgogoro mkubwa kuliko yote iliyowahi kuvikumba visiwa hivi. Hata pale alipopigiwa simu kupitia namba yake binafsi na mshindi wa uchaguzi ule kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar yaani Maalim Seif Sharif Hamad ambaye akimtafuta ili waonane kuzungumzia hatua ile ya kufuta matokeo ya uchaguzi akawa hapokei simu. Akaandikiwa ujumbe mfupi wa simu hakujibu. Akaandikiwa barua rasmi kuombwa wakutane hakujibu.
\
Yote alikuwa kayapanga vyema. Akamuita Maalim Seif siku moja kabla ya kuapishwa Dk. John Pombe Magufuli kuwa Rais. Na pamoja na hayo Maalim Seif hakuwa na kinyongo (kama kawaida yake) na akaitikia wito. Kumbe alimwita kwenda kumfanyia istihzai. Maana baada ya Maalim Seif kumueleza na kumpa ushahidi wa fomu halali za matokeo ya uchaguzi zikionesha kwamba yeye ndiye mshindi, jawabu la JK likawa kwamba amebakiza saa 24 tu kabla hajakabidhi madaraka na kwa hivyo asingeweza kufanya chochote. Maalim Seif alimwambia humtendei haki mrithi wako, Rais Dr. John Pombe Magufuli, kumwachia mgogoro huu wakati ndiyo kwanza anapokea madaraka lakini hayo hayakumshughulisha JK. Yeye alitaka apige picha tu na Maalim Seif ili azitumie kuihadaa jumuiya ya kimataifa kwamba alijaribu kabla hajaondoka madarakani. Bahati nzuri, jumuiya ya kimataifa ilimshtukia! Haikuwa ajabu pale Taasisi ya Mo Ibrahim Foundation ilipomnyima tuzo ya Rais bora Afrika kwa kutoheshimu kwake misingi ya demokrasia na utawala bora. Ndugu Deus Kibamba yuko sahihi kwamba mgogoro wa kufutwa matokeo halali ya uchaguzi halali wa Zanzibar unapaswa kutatuliwa, na mimi naamini utatatuliwa na kumalizika, lakini Jakaya Kikwete siye wa kumpa jukumu hilo wakati yeye ndiye mvurugaji wa yote. WACHA HISTORIA IMHUKUMU.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment