KUNA
nyakati ambapo watawala wetu lazima waambiwe ukweli. Huu ni wakati
mmojawao. Na wa kuwaambia ukweli ni sisi wenyewe.
Haitokuwa mara ya kwanza katika historia kwa umma kuwaambia ukweli watawala wao. Wala sisi hatutokuwa wa mwisho kuwaambia ukweli watawala.
Kila pale watawala wanapopandwa na kiburi cha kuamini kwamba wao ndio wenye uwezo wa kuamua nini kiwe na nini kisiwe, nani awe na sauti ya kusema na nani asiwe na sauti inatupasa tusimame pamoja tuwaambie ukweli wasiotaka kuusikia.
Ukweli wenyewe ni rahisi kuufahamu kama wana masikio yenye kusikia. Ni rahisi zaidi kuuelewa kama wana akili na wanaweza kufikiri.
Ukweli wa mwanzo wanaohitaji kuambiwa ni kuwa udhalimu haudumu daima dawamu. Ukweli wa pili wanaolazimika kuambiwa ni kwamba ijapokuwa wanajidai kuwa wao ni wababe wa kisiasa kwa sababu vyombo vya dola vimo mikononi mwao, kwa hakika ya mambo hawana ubabe unaoweza kuushinda ubabe wa nguvu za umma.
Vitendo vya mashambulizi ya kisiasa ya hivi karibuni yanayozidi kuihatarisha hali ya utulivu na amani visiwani Zanzibar, ni vitendo watavyokuja kuvijutia wenyewe.
Vitendo hivyo ni nyongeza nyingine katika kumbukumbu ya msururu wa unyama wa kisiasa unaofanywa visiwani humo.
Mashambulizi hayo yamekwishaipaka matope Zanzibar, yanawaaibisha viongozi wa serikali ya huko pamoja na wa Serikali ya Muungano. Pamoja na yote, mashambulizi hayo yanathibitisha kukosekana utawala bora na udhaifu wa demokrasia nchini Tanzania.
Katika hali hizi, ni taabu kuamini kwamba uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 utafanywa kwa njia za kistaarabu au kwamba utakuwa na uhalali unaostahiki uwe nao, licha ya kuwa huo utakuwa uchaguzi wa sita nchini tangu urejeshwe mfumo wa siasa za vyama vingi.
Watawala wetu hawawezi kujiweka mbali na yanayotokea sasa wala hawawezi kusema kwamba hawakuyatarajia. Walikwishaonywa mara kadha wa kadha kwamba kuna njama za kuirejesha Zanzibar pabaya. Ishara zikionekana alfajiri na mapema.
Zilianzia kwa uhuni wa kisiasa kwa njia ya matusi ya nguoni dhidi ya wapinzani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Waliokuwa wakitukana wakiwa juu ya majukwaa ya CCM walikuwa baadhi ya viongozi wa chama hicho.
Wengine wakiandika na kusambaza vipeperushi vya matusi dhidi ya hata kiongozi mwenzao, Rais mstaafu Amani Abeid Karume.
Wakati hayo yakiendelea, kuna viongozi wengine wa CCM walikuwa wakisema wazi kwamba watatumia nguvu kuzuia chama chao kisishindwe katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba 25. Majina ya wachochezi wote hao yanajulikana na kanda za video zenye kuthibitisha shutuma dhidi yao zipo.
Kwa bahati mbaya, wakuu wa polisi wamenyamaza kimya na hawakuwachukulia hatua yoyote viongozi hao. Hawakuthubutu hata kutoa taarifa ya kuwaonya kuhusu vitimbi vyao. Wakuu wengine wa serikali, Bara na Zanzibar, nao pia wamekaa kimya.
Lililozidi kusikitisha ni kuwaona baadhi ya vigogo vya CCM kutoka Bara wakihutubia mikutano ya hadhara Zanzibar huku wakiushadidia uovu wa wahafidhina wa chama chao wa Visiwani.
Hadi sasa ni kiongozi mmoja tu wa taifa hili anayeonekana kufanya juhudi za kuwatahadharisha viongozi wa serikali na kuujulisha ulimwengu kuhusu njama ovu za baadhi ya viongozi wa CCM/Zanzibar zinazoweza kusababisha umwagaji wa damu. Naye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Mfano mmoja wa jitihada zake ni mkutano aliokuwa nao na waandishi wa habari katika Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam, Mei 10, mwaka huu. Kwenye mkutano huo, Hamad alizilaumu Tume za Uchaguzi nchini yaani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwa zinatumiwa na CCM dhidi ya wananchi.
Alieleza kwa ufasaha kuhusu njama zinazofanywa na taasisi mbalimbali za serikali, zikiwa pamoja na vikosi vya Ulinzi na Usalama, katika zoezi zima la uandikishaji wa watu katika Daftari la Kudumu la Wapigajikura.
Taksiri zilizojitokeza katika zoezi hilo ni taksiri zilizosababishwa kwa makusudi kuiridhisha CCM, alidai Hamad. Hamna shaka kwamba yanayojiri sasa ni matokeo ya hayo aliyokuwa akiyalalamikia Hamad.
Tangu zoezi hilo la uandikishaji wapigajikura lianze kumetokea rabsha na vurugu katika vituo kadhaa vya uandikishaji wapigakura kisiwani Unguja.
Isitoshe, kumetokea na mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari kwa lengo la kutaka kuwanyamazisha wasiuseme uovu unaotendwa na vyombo vya dola. Kwanza kulikuwako na taarifa za kutekwa nyara na kupigwa mwandishi habari wa kujitegemea aitwaye Ali Omar.
Waliompiga walikuwa wamejifunika nyuso zao ki-“Ninja” na walimshutumu kuwa alikwenda kutafuta habari kwenye kituo cha kujiandikisha wapigakura huku akiwa mwandishi habari wa Upinzani.
Siku mbili baadaye, Juni 29, 2015 ilikuwa nyongeza nyingine katika orodha ya tarehe za unyama wa kisiasa unaofanywa Zanzibar.
Siku hiyo, kwa mujibu wa mashuhuda, genge la watu wasiojulikana waliokuwa pia wamejifunika nyuso na wanaokisiwa kufikia 20 walivamia kituo cha redio binafsi iitwayo “Coconut FM,” iliyo katika eneo la Kilimani, Unguja Mjini.
Dhamira ya washambulizi hao ilikuwa ni “kumshughulikia” mwandishi habari wa redio hiyo aitwaye Ali Mohamed, aliyeandaa kipindi maalumu kilichojadili hali ya vitisho katika vituo vya kuwaandikisha wapigajikura.
Chama cha Wananchi (CUF) katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ismail Jussa, Kaimu Mkurugenzi Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma, kilidai kwamba hao “watu wasiojulikana” walikuwa ni watu “wanaosadikiwa” kuwa ni askari wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Aidha, Jussa alidai kwamba watu hao walikuwa wakitumia magari yenye namba za vikosi vya polisi vya Zanzibar. Hizi ni shutuma nzito na hazistahili kupuuzwa hata kidogo.
Ikiwa shutuma hizo ni za kweli basi wahalifu katika kadhia hiyo si hao askari peke yao waliovaa “Ninja” wakiwa na silaha za namna kwa namna zikiwa pamoja na bunduki za rashasha, mapanga, marungu na msumeno.
Wanaowajibika katika kadhia hiyo ni pamoja na wakubwa wa hao askari polisi, waziri wao, Rais wa Zanzibar na Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Wakuu wa polisi wananukuliwa wakikana kama wanahusika na mashambulizi hayo lakini inashangaza kwamba wao wala wakubwa zao serikalini hawakuyalaani mashambulizi hayo seuze kuwachukulia hatua za kuwatia nguvuni wahusika.
Vikosi hivyo vimekuwa vikionekana katika vituo vya uandikishaji wa wapigakura vikiwa na silaha na vikiwa vimejifunika nyuso. Wamewajeruhi watu kadhaa katika vituo mbalimbali vya uandikishaji wa wapigakura.
Ikiwa vikosi hivyo vya washambulizi hao si vikosi vya polisi ya Serikali ya Zanzibar, vilivyo chini ya Waziri Haji Omar Kheri, basi nani mwenye kuviratibu na kuviongoza vikosi hivyo? Nani mwenye kuvimiliki?
Haya ni maswali yanayohitaji kujibiwa na viongozi wa ngazi za juu kabisa wa serikali mbili.
Tunajua kwamba mitaani vimepewa jina la “Janjaweed” vikifananishwa na wanamgambo wa Janjaweed wanaodaiwa kutumiwa na Serikali ya Sudan kufanya mauaji na vitendo vingine vya ugandamizi dhidi ya raia wa kawaida katika eneo la Darfur, magharibi mwa Sudan, na pia mashariki mwa Chad.
Mashambulizi ya Janjaweed wa Darfur ndiyo yaliyosababisha Mahakama ya Kimataifa Jinai (ICC) kutoa waranti za kutaka akamatwe Rais wa Sudan, Hassan Ahmed al Bashir, waziri wake Ahmad Harun pamoja na Ali Kushayb, anayedaiwa kuwa mmoja wa viongozi wa Janjaweed.
Ugaidi ni ugaidi. Hauna hili wala lile. Lakini nadhani hakuna ugaidi ulio wa hatari zaidi ya ule unaotekelezwa na vyombo vya dola kwa niaba ya viongozi wasiostahiki kuongoza.
Hatari nyingine ni kwamba hivi vyombo vya dola vikishaota meno na kuanza kutafuna, baadaye vikishazoea huwa havichagui tena nani wa kumtafuna, huwa mpata, mpatae.
Hali iliyopo sasa Zanzibar ni hali ya kutisha na inaashiria hatari kubwa inayovikabili visiwa hivyo tunapoukaribia uchaguzi mkuu.
Toka lianze zoezi la uandikishaji wa wapigakura, watu kadhaa wamejeruhiwa na hivyo vikosi vya watu wenye silaha za kila aina, wasiovaa nguo rasmi za polisi lakini wenye kutumia magari ya polisi na wanaoziba nyuso zao wasionekane. Watu kadhaa wamejeruhiwa na vikosi hivyo Unguja Kaskazini, Wilaya ya Magharibi, Wilaya ya Mjini na Makunduchi, Mkoa wa Kusini.
Huko Makunduchi, watu watano walijeruhiwa, wawili kwa kupigwa risasi Julai 4, wakati wa uandikishaji wa wapigakura katika Daftari la Kudumu. Mmoja wa majeruhi ni mzee wa miaka 70, aliyepigwa kwa magongo na nondo. Hili ni tukio la karibuni kabisa wakati naandika makala haya.
Vurugu lilianza watu walipokusanyika kujadili namna wasivyofurahishwa na zoezi hilo lilivyokuwa likiendeshwa kwa vile walidai kwamba mamluki walikuwa wakiandikishwa katika Daftari hilo. Ndipo walipovamiwa na kundi la askari wasiovaa sare lakini waliojifunika vinyago usoni na waliokuwa na silaha za moto.
Kamanda wa Mkoa wa Kusini, Unguja, Juma Saadi, alisema kwamba polisi walipiga risasi hewani na hakujeruhiwa mtu. La kushangaza hapa ni kwamba majeruhi walipelekwa hospitali ambako madaktari walithibitisha kwamba baadhi ya majaraha yao yalisababishwa na kupigwa risasi.
Moja ya picha zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii za majeruhi hao zinaonyesha risasi iliyotolewa kutoka kwenye mwili wa majeruhi mmoja.
Angalau Kamanda Saadi amekiri kwamba washambulizi walikuwa askari polisi. Ya kuulizwa hapa ni kwanini askari hao wakawa wanafunika nyuso zao wasijulikane? Kwa nini wanakwenda kwenye vituo vya uandikishaji wapigakura wakiwa na silaha nzito? Kwa nini wanalazimisha watu fulani waandikishwe kwenye Daftari la Wapigakura na wengine wasiandikishwe?
Swali
lililo muhimu zaidi ya yote ni: Nani aliyewapa amri ya kutenda
wayatendayo?
Hakuna lolote linaloweza kuhalalisha unyama huu. Na ndio maana kuna Wazanzibari ambao tayari wamekwishaanza kukusanya ushahidi wa hotuba, picha na video za viongozi na wakuu wa serikali waliochochea mashambulizi hayo au wenye kuhusika nayo moja kwa moja.
Nia yao ni kuuwasilisha ushahidi huo mbele ya Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC), huko Hague.
Kwa hili, ni muhali kwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, na hata mwenzake wa Muungano, Jakaya Kikwete, kuliepuka kwa vile ndio wakuu wa juu kabisa wenye dhamana ya kusimamia amani nchini na kuyalinda maisha ya wananchi wao.
Matamshi ya mara kwa mara ya Shein kuwa atahakikisha amani inalindwa na kuwa hatomvumilia yeyote atayevuruga amani hayatamsaidia kitu endapo ataendelea kushindwa kutekeleza ahadi hiyo.
ahmed@ahmedrajab.com
Chanzo: Raia Mwema
Ahmed Rajab
ahmed@ahmedrajab.com
ahmed@ahmedrajab.com
ahmed@ahmedrajab.com
Toleo la 413
8 Jul 2015
Toleo la 413
8 Jul 2015
Toleo la 413
8 Jul 2015
No comments:
Post a Comment