14/03/2016
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa tareh 25 Oktoba 2015, usalama wa raia wa Zanzibar na mali zao umekuwa katika hali tete. Hali hii inatokana na kushuhudiwa kushamiri kwa matukio ya kuogopesha wananchi kufurutu ada ukiukwaji wa HAKI ZA BINAADAMU miongoni mwa wananchi Kunakofanywa na vyombo vilivyopewa dhamana ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi yetu raia wake na mali zao.
Katika siku za hivi kadribuni, hususan baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Sali Jecha, kutangaza kinyume na katiba ya nchi, kufuta uchaguzi wa 25 Oktoba 2015 na matokeo yake, Zanzibar imeshuhudia uingizwaji na uingiaji mkubwa wa askari, vifaa na zana nzito za kivita katika visiwa vya Unguja na Pemba. Sambamba na hayo kumekuwepo kwa askari wengi na JWTZ wanaorandaranda mitaani wakiwa na silaha nzito za kivita na operasheni isiyo rasmi ya kuwakamata na kuwabambikizia kesi wananchi wasio na hatia na hatimaye kuwaweka katika vituo mbali mbali vya polisi na kuwanyima dhamana hata kwa makosa ambayo kisheria yanapaswa kudhaminiwa.
Katika mwezi wa February 2016 huko kengeja wafuasi wa CUF walikamatwa na polisi na kuwekwa ndani kwa tuhuma ya kuchoma tawi la CCM la eneo hilo Polisi walichukuwa hatua hiyo mara tu tukio hilo liliporipotiwa kwao. Aidha katika mwezi huu wa Machi baadhi ya matawi ya CUF na Baraza za CUF zilichomwa moto na kuteketea tikitiki. Taarifa ya uhalifu huu zlipripotiwa katika vituo vya polisi vya na RB kuandikwa hata hivyo hadi hii leo hakuna yoyote aliyekamatwa kwa tuhuma ya uhalifu huo.
Matukio ya uchomwaji moto na uharibifu wa mali za CUF umetokea mahala mwingi Unguja na Pemba kama vile kisauni ambapo ofisi mpya ya CUF jimbo la Dimani zilizogharimu zaidi ya sh 90m lilichomwa moto tarehe 24/03/2015 na kuteketea. Kwa makusudi kabisa, hata baada ya polisi kupata taarifa hiyo na kulikagua eneo husika hakuna yeyote aliyetuhumiwa na kukamatwa.
Mtakumbuka kwamba tabia hii ya wananchi ambao kwa asilimia kubwa huwa ni CCM au vyombo vya serikali vilikuwa vikihujumu kwa makusudi mali ya CUF na hata mali ya serikali kama vile shule, zahanati, visima vya maji nk. (Tukio la Shengajuu la 1996 ambapo watu waliofanya tukio la kcuhoma moto shule, kutia kinyesi visima walikamatwa wakiwa wamefuatana walikuwa na petrol, bunduki, mapanga, madoo ya kinyesi vyote vikiwa usoni ya gari la idara ya usalama wa Taifa ZNZ 1296).
Baada ya tukio hilo la kufedhehesha serikali na mapambamo yaliyotokea baina ya wafuasi wa CUF na wahalifu (usalama wa Taifa), serikali iliwaadhibu kwa kuwapiga, kuwaibia mali zao, kuwafanyia vitendo vya kinyama na kuwaweka ndani kwa zaidi ya miezi 9 wananchi wasio na hatia. Hivyo haya yanayoendelea hivi sasa huko Pemba si mambo mageni hasa katika kipindi hiki ambappo SMZ imechukia sana kwanini CUF wamegomea kushiriki uchaguzi batili wa madrudio wa 20/03/2016.
Sisi CUF tunaamini pasipo na shaka yeyote kwamba matukio ya kuchomwa moto kwa masikani, matawi ya CCM huko Pemba ama baadhi ya nyumba za watu binafsi na mali za serikali ni mwendelezo tu wa siasa chafu za chuki zinazoendelezwa na serikali dhidi ya wananchi wasio na hatia. CUF imesikitishwa sana na vitendo hivi vya kihuni na visivyoonyesha siasa za kistaarabu na inalaani vikali na kwa nguvu zote uhalifu huu ambao unarejesha nyuma ile spirit ya kushindana bila kupigana.
CUF imepokea taarifa kwamba zaidi ya wananchi 30 wengi wakiwa wafuasi, viongozi na wanachama wa CUF wamekamatwa na polisi na wameshikiliwa katika vituo mbali mbali vya polisi huko pemba.
Utendaji huu wa Jeshi la polisi umeigawa ZNZ vipande vipande na kuwa chanzo cha siasa za chuki, uhasama na kusababisha ZNZ kushindwa kutekeleza shughuli zake za kimaendeleo.
Kwa mfano amri ya Mkuu wa Mkoa kaskazini Pemba kupiga marufuku watu wasitembee baada ya saa 2 za usiku na kwamba atakayevunja amri hiyo atakamatwa na kushtakiwa kwa kosa la uzembe na uzururaji ni hatua nyengine ya SMZ ya kuwahalalilisha na kuwaweka wananchi wa mkoa wa Kaskazini Pemba katika hali ngumu ya maisha.
Amri hii inazuwia hata sala za Isha na Alfajiri jambo ambalo waumini wa Kiislamu hawatakubaliana nalo, Mkuu wa Mkioa awache ukereketwa na aendeshe mkoa kwa hekima, busara, weledi, wa kuongoza watu. Kuongoza watu kwa amri za kidikteta kumepitwa na wakati. Asome alama za nyakati, aache kutoa amri zinazopingana na hata haki za binaadamu na za watu.
Chama Cha Wananchi CUF kinaamini kuwa matukio haya ni mwendelezo wa njama za CCM zinazoratibiwa na kutekelezwa kimkakati kwa malengo mahususi ya kuamisha hamasa na kupandikisha joto la jazba miongoni mwa wananchi ili kuhalalisha mpango maalum na kutoa fursa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kutumika kutisha, kukamata, kupiga na kutufungulia mashtaka wananchi wa wasio na hatia.
Kutokana na unyeti wake matukio ya uvunjifu wa amani na hatua za ukiukwaji wa HAKI ZA BINAADAMU, masuala haya hayapaswi kupuuzwa kwani yanaweza kupelekea kufanikiwa kwa dhamira mbaya waliyonayo baadhi ya watu katika nchi yetu wasioitakia mema Zanzibar na kwa hivyo kuathiri umoja wa kimataifa uliopo uliopatikana kwa gharama kubwa ya jasho la viongozi wazalendo, Mheshimiwa Rais mstaafu wa Zanzibar Dr. Amani Karume na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad na uhai wa wananchi wanyonge. Kwa hivyo sisi katika CUF:
• Tunavinasihi vyombo vya ulinzi na usalama wan chi yetu kukataa katakata kuingia katika mtego wa mipango miovu ya wanasiasa waliofilisika wenye lengo la kuleta taharuki miongoni mwa wananchi na kuamsha hamasa na kupandisha jazba na ghamidha zitakazopelekea kuchafuka kwa hali ya amani ya nchi yetu. CUF inatoa wito kwa kwa vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama hapa nchini kusimamia amani na utulivu pasi na kuegemea upande wowote wa kisiasa. Ni muhimu vyombo hivyo vikajipambanua na kujijengea heshima na kulinda imani ya wananchi waliyonayo kwao. Kinyume na haya, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama hasa jeshi la polisi na jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ, ambalo katika siku za hivi karibuni limeonekana kutumika vibaya, kufahamu kuwa mustakbali wa utu na raia, mali zao na amani ya nchi yetu imo mikononi mwao na watakuwa wa mwanzo kuwajibika endapo jahazi la amani yetu litakwenda mrama.
• Tunaziomba Taasisi za kiraia za ndani kuacha woga na badala yake kupaza sauti zao juu ya mwangwi imara masikioni mwa viongozi madhalimu kukemea unyanyasaji na ukandamizaji wa haki za binadamu. Aidha, CUF inaziomba jumuiya za kimataifa kuendelea kuitazama Zanzibar kwa umakini wa hali ya juu kufuatilia mwenendo na matukio nakuweka kumbukumbu kwa hatua za baadae kwa kila anaeonekana kushtadi kuonea wananchi wanyonge kutokana na nafasi yake katika utumishi wa umma.
• Tunatoa wito kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Jhn Magufuli, kuchukua dhamana ya uongozi kukataa kuhadaiwa na wasaidizi wake na kukomesha matumizi mabaya ya vyombo vya ulinzi na usalama vilivyo chini ya amri yake na kudhibiti uhuni wa kisiasa wa baadhi ya vikosi vya Idara Maalum ya Zanzibar kama Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania. Kwa la zanzibar, Rais Magufuli hana pa kupenyea na kwamba atawajibika kutokna na mfumo wa Katiba na sheria na utaratibu wa kuongoza nchi tuliojiwekea.
• Tunatambua usumbufu, idhilali na mateso makubwa yanayowapata wananchi wa visiwa vyote vya zanzibar kufuatla maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba 2015 ya kuikataa CCM na kuamua kufanya mabadiliko katika uongfozi wa nchi. CUF inawaomba wananchi wote kuendelea na kujipamba na mavazi ya subira na kuamini kuwa hizi na hatua za mwisho za CCM kuelekea kufutika katika nyoyo za wazanzibari na kwamba wananchi wote wausiane katika kuvumilia na kukataa kuchokozeka kwa lengo la kutunza amani ya nchi yetu na kufikia malengo yetu ya muda mrefu ya kukamata hatamu za dola ya zanzibar bila kuathiri wanachi wetu.
• CUF inawahakikishia wananchi wote kuwa haitarudi nyuma katika mapambano ya kudai haki ya wananchi na kwamba maamuzi yao ya tarehe 25 Oktoba 2015 yatazingatiwa, kuheshimiwa na hatimaye haki kutamalaki katika visiwa vya zanzibar. Ni wajibu kwa wazanzibari wote kutambua kuwa giza nene hufuatiwa na miale ya nuru na kutoa faraja kwa kila mwanandamu.
Naomba kuwasilisha
HAMAD MASOUD HAMAD
KAIMU MKURUGENZI HABARI UENEZI NA MAWASILIANO KWA UMMA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Popular Posts
- CUF wamuandikia barua Mwenyekiti wa ZEC
- TAMKO LA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA JUU YA KUTEKWA KWA MWANDISHI WA HABARI WA SAUTI YA UJERUMANI ( DW ) SALMA SAID.
- Sera ya kunena na Kutenda ya Wana CUF
- (no title)
- Ufungaji wa Kampeni ya uchaguzi mdogo wa Dimani.
- Salam kwa Mkururinza wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment