Headlines News :
KARIBU CUF DIASPORA NETWORK - CUF HAKI SAWA KWA WOTE...TEGEMEA KILA JIPYA NA ZURI KUTOKA KWETU...LIKE PAGE YETU KWENYE FACEBOOK
Home » » Tujihadhari na “watoto wa kambo” wa Hitler

Tujihadhari na “watoto wa kambo” wa Hitler

Na Ahmed Rajab Na Ahmed Rajab
WIKI iliyopita nilipata baruapepe kutoka kwa rafiki yangu mmoja wa Burkina Faso ambaye kwa muda mrefu sasa amekuwa chanda na pete na Blaise Compaoré, Rais wa nchi hiyo aliyepinduliwa kwa ghadhabu ya umma mwishoni mwa Oktoba 2014.

Waburkinabé, wananchi wa Burkina Faso, walikuwa wamekwishamchoka Compaoré aliyekuwa madarakani kwa miaka 27. Alipoamua kuibadili Katiba ili aendelee kutawala zaidi waliona anawageuza mafala (malofa), ndipo walipoghadhibika wakaingia mitaani na kumpindua. Compaoré hakuwa na hila ila kuikimbia nchi na kwenda kutafuta hifadhi Côted’Ivoire.

Katika baruapepe yake rafiki yangu hakuyadhukuru hayo ya sahibu yake ambayo lazima akiyakumbuka kwani yamemjaa kichwani. Lakini aliyagusia kwa mbali kwa kutoa mfano wa hii aibu ya watawala wetu inayowafanya wawe kichekesho duniani kwa kuufuta uchaguzi uliokamilika walipoona chama chao kinaelekea kushindwa katika mchuano wa urais wa Zanzibar.

Yafuatayo ni tafsiri ya aliyoniandikia rafiki yangu: “Tanzania imepoteza fursa ya kuuthibitishia ulimwengu kwamba sisi (Waafrika) tuko tayari kufuata utawala wa sheria, utawala bora na utawala wa kidemokrasia. Bado demokrasia halisi na moyo wa kukubali kushindwa katika uchaguzi haukutia mizizi katika Bara letu ambalo lingali la giza. Walio madarakani wangali wakiwazuia wengine walioshinda uchaguzi wasiweze kuwatumikia wananchi.”

Halafu akanikumbusha yaliyotokea Côted’ivoire baada ya kufanywa duru ya pili ya uchaguzi wa urais Novemba 28, 2010 ambapo Alassane Ouattara aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 54.1 ya kura zote zilizopigwa. Ushindi huo ulitangazwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.

Chama cha Rais Laurent Gbagbo kilikataa kuyakubali matokeo hayo. Kama kisemavyo Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu kura za Pemba katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, chama cha Gbagbo nacho kilisema kwamba kulitokea ghiliba katika kura hizo za kaskazini mwa Côted’Ivoire. Tume ya Uchaguzi ilikataa na kusema hayo hayakuwa kweli, waangalizi wa kimataifa nao pia walisema uchaguzi mzima ulikuwa wa haki.

Lakini Gbagbo aliushikilia uzi ule ule wa chama chake na akalazimisha Mahakama ya Kikatiba yazifute kura zipatazo 600,000 zilizopigwa katika majimbo tisa ya kaskazini, ambako ni ngome ya Ouattara. Mahakama yakaitika “hewala bwana”, yakayafuta matokeo ya kaskazini na yakasema kwamba kwa kuondolewa kura hizo za kaskazini Gbagbo alishinda kwa asilimia 51.

Katika baruapepe yake rafiki yangu alinikumbusha kwamba “hatimaye Gbagbo aliondoshwa madarakani kwa nguvu na hii leo yuko Hague anafanyiwa kesi ya aibu.”

Alimaliza kwa kuandika: “Bado tumo tu tunayashutumu madola ya Magharibi kwa ukoloni mamboleo lakini viongozi wetu wa Kiafrika nao hawayajali maslahi ya raia zao…Inavunja moyo…Tunafuata njia mbaya.”

Kwa Zanzibar hiyo “njia mbaya” ndiyo iliyotufikisha hapa tulipo. Kwa ilivyo hivi sasa, zaidi ya nusu ya wananchi wa Zanzibar wamepokonywa haki yao ya kimsingi ya kuongozwa na Rais wamtakaye. Wamebakishiwa uhuru wa kuzitii amri za CCM, chama chenye kushika mpini wa utawala.

Jamii isiyokubali mabadiliko ni jamii iliyochakaa. Haitaki mambo mapya, inayashikilia yaleyale ya kale. Vivyo hivyo kwa watawala. Chama chochote kinachotawala kisipokubali kuondoka madarakani wananchi wanapokitaka kiondoke, huwa pia kimechakaa. Ukaidi wa kukataa kupumzika kwa miaka mitano mpaka uchaguzi ujao ni dalili moja tu ya kuchakaa kwake.

Pamoja na kuchakaa, bila ya shaka zipo sababu nyingine za kwa nini CCM kinakataa kuyaachia madaraka Zanzibar licha ya kujuwa kwamba kilishindwa katika uchaguzi wa urais wa Zanzibar mwaka jana. Moja ni haja ya kuyalinda maslahi ya kibinafsi ya baadhi ya viongozi wake wakuu, lakini sababu kubwa au tuseme kisingizio kikubwa nadhani ni kile cha kuuhifadhi Muungano.

Wanavyoamini wao ni kwamba Chama cha Wananchi (CUF) kikiushika uongozi wa Zanzibar kitauvunja Muungano.

Kuna vizingiti viwili vikubwa alivyovikuta Rais John Magufuli aliposhika uongozi wa taifa, na vyote vimewekwa na sera za chama chake; navyo ni vizingiti vya demokrasia na Zanzibar. Vizingiti hivyo vinafungamana.

Kwa vitendo na matamshi yao watawala wa Zanzibar pamoja na wa CCM-Taifa ni wazi kwamba hawaiamini kwa dhati dhana ya demokrasia na wala hawakubali Zanzibar iwe inajiamulia mambo yake yenyewe. Kila siku zikisonga mbele tangu Muungano uundwe Aprili 1964 majaaliwa ya Zanzibar ndipo yanapozidi kuamuliwa Dodoma, kwenye makao makuu ya CCM.

Ndio maana haikustaajabisha, ingawa ilisikitisha, kusoma kwenye gazeti moja karibuni Dk. Hassy Kitine, mkurungenzi wa zamani wa Usalama wa Taifa, akinukuliwa akitamka kwamba Maalim Seif Sharif Hamadi, aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba mwaka jana, anaota akidhani kwamba ataiongoza Zanzibar. Hatoruhusiwa kamwe.

Miongoni mwa mengine aliyonukuliwa Kitine kusema ni haya: “Wenzetu wamepata uhuru wao kwa kumwaga damu, tofauti na sisi huku, ambako Mwalimu Nyerere alitumia meza ya mazungumzo kusaka uhuru, kwa wenzetu siyo”.

Sasa tuseme Kitine, na usomi wake wote, hatambui kwamba Zanzibar ilipata uhuru wake kamili Desemba 10, 1963? Na kwamba uhuru huo, haukupatikana kwa umwagaji wa damu bali kwa mazungumzo yaliyofanywa kwenye meza katika jumba la Lancaster House, London?
Mazungumzo yalikuwa baina ya Serikali ya Uingereza na wanasiasa kutoka Zanzibar, akiwemo Sheikh Abeid Amani Karume, kiongozi wa Afro-Shirazi Party (ASP).

Damu ilimwagwa na Mapinduzi ya Januari 12, 1964, mapinduzi ambayo hayakuupindua utawala wa Uingereza bali yaliipindua serikali huru ya Zanzibar iliyokuwa ikiongozwa na Waziri Mkuu Sheikh Mohamed Shamte Hamadi.

Kitine alitoa kauli nyingine yenye kusikitisha na usiyoitarajia kwa mtu kama yeye. Hakuona aibu kutamka kwamba watu wanahangaika kutafuta uongozi wa Zanzibar “jambo ambalo haliwezekani kwa sababu nchi hiyo haikukombolewa kwa makaratasi,” yaani kwa kura.

Sasa angelitueleza kwa nini matrilioni ya fedha za umma zinatumiwa kwa udanganyifu wa kujidai tuna demokrasia ilhali imekwishaamuliwa kwamba CCM kikishinda kisishinde katika uchaguzi kitaendelea tu kutawala naiwe iwavyo?

Huo ni uamuzi wa wale wanaoamini kwamba ni wao pekee wenye haki ya kuziongoza serikali mbili za Tanzania, ya Muungano na ile ya Zanzibar. Niliwahi kuandika mwaka jana katika sahafu hii kuhusu lile nililoliita “dubwasha” na ambao wengi nchini wanaliita “the system”.

Huu ni mfumo usio rasmi wenye kuwaunganisha walio kwenye Usalama wa Taifa na vyombo vingine vya usalama na ulinzi pamoja na wahafidhina wa CCM. Waliomo humo ndio wanaojiona kuwa ni wao wenye haki na dhamana ya kuiendesha, na kwa dhana yao, kuilinda Tanzania. Huo ndio undani wa siasa za kwetu.

Mantiki inatuambia kwamba ikiwa “system” imeamua kuwa haitokubali CCM kishindwe katika uchaguzi Zanzibar, basi pia haitokubali CCM ishindwe Bara. Haitokubali kwa sababu ya kuhofia kwamba upinzani ukishinda na ukaruhusiwa ushike madaraka ya taifa zima hautozivumilia siasa za kijinga zinazoendeshwa Zanzibar na wenye kutumia nguvu za dola kubakia madarakani.

Tutaziona nguvu hizo zikizidi kutumika tunapoukaribia ule uitwao uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanywa Machi 20. Kuna ishara mbaya. Wale waitwao “mazombi” wanaendelea na mashambulizi yao kwa raha zao na wapinzani wanatishwa.

Ninavyoandika haya kuna mpinzani mmoja aliye nje kwa dhamana baada ya kushikiliwa na polisi. Anatuhumiwa kutoa video yenye kumtukana Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein. Kamishna Msaidizi wa Polisi Zanzibar, Salum Msangi, wiki iliyopita alisema kuwa Jeshi la Polisi linakusudia kuwahoji watu 34, kwa kuitumia mitandao ya kijamii kuwatukana viongozi wa kitaifa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na maadili ya Wazanzibari.

Aliyoyasema Msangi ni sawa sawa. Matusi ni kinyume cha ustaarabu wetu, akitukanwa kiongozi au mwananchi wa kawaida. Na hatua ya kuwafikisha watuhumiwa mbele ya mahakama ni sawa ilimradi isiwe kisingizio cha kuwatia adabu wapinzani.

Aidha, Msangi asisahau kwamba kabla na wakati wa kampeni za uchaguzi umma ulishtushwa kwa matusi ya nguoni ya baadhi ya wanasiasa kwenye majukwaa yao. Jeshi la Polisi lioneshe kwamba halina upendeleo kwa kuwashughulikia watuhumiwa wote bila ya kujali ni wa chama gani cha siasa. Kanda za video zenye ushahidi wa tuhuma wanazotuhumiwa zipo.

Kadhalika asilisahau lile bao jeusi kwenye maskani maarufu ya CCM ya Kisonge ambalo mara kadha wa kadha limekuwa na maandishi ya uchochezi, chuki na matusi dhidi ya viongozi wa CUF na hata wa CCM.

Kwa muda mrefu, kumekuwa na shutuma kwamba CCM, kupitia serikali zake, kimekuwa kikilitumia jeshi kuwatishia wakazi wa Zanzibar. Hii ndiyo sababu inayowapa watawala wetu jeuri ya kuthubutu kufanya walitakalo na ndiyo inayowafanya wawe na kibri. Wanatambua kwamba wanao wa kuwalinda.

Labda wenyewe hawajui kuwa matamshi yao na lugha wanayoitumia ni ya vitisho. Hamna shaka kuwani ya vitisho ela safari hii, kwa nionavyo, wananchi wamekuwa sugu, hawatishiki tena. Na hapo ndipo penye hatari.

Na hatari inazidi kuwa kubwa kwa vile watawala wetu hawaoneshi kama wamejifunza kitu. Wanajifanyia mambo utadhani wao ni watoto wa kambo wa Adolf Hitler, yule dikteta wa Ujerumani aliyekuwa na sera za kibaguzi, aliyetawala kwa mabavu na aliyesababisha vifo visivyosemeka.

Kwa hali hiyo wapinzani wa Bara wasihadaike wakafikiri kwamba viongozi wa CCM wa huko kwao ni tofauti na wale wa Zanzibar. Wote ni “dugu moja”. Kwa hivyo, kuna haja ya wapinzani wa Bara kuyaangalia yanayojiri Zanzibar kwa makini, wayaone kuwa kama ni somo kwao, tena somo kubwa, katika harakati zao za kuleta mabadiliko.

Hii huzuni iliyotanda sasa Zanzibar inaweza ghafla tukashtukia imehamia Bara. Watawala ndio walewale, mbinu zao ndizo zilezile na maadui zao ndio walewale — haki, uwazi na ukweli.

CHANZO: RAIA MWEMA
Share this article :

No comments:

Post a Comment

 
Support : ZENJIBARZA
Copyright © 2011. ACT WAZALENDO DIASPORA NETWORK - All Rights Reserved