TAARIFA YA JUMUIYA YA VIJANA – CUF (JUVICUF)
KWA VYOMBO VYA HABARI
24 Juni, 2016
Ndugu zangu waandishi wa Habari,
Awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima wa afya na tukaweza kukutana hapa asubuhi hii ya leo. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kuwajaalia wananchi wa nchi yetu kuendelea kuwa na busara, hikma na uvumilivu mkubwa kwa lengo la kuhakikisha hali ya amani na utulivu wan chi yetu licha ya kuwepo kila aina ya uonevu na udhalilishaji wa raia unaoendelea kuratibiwa na watawala waovu, na kutekelezwa na makundi yao waliyoyaandaa kwa lengo la kuzima sauti za wananchi kudai haki zao za kimsingi kufuatia kufutwa kwa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
Pili, nichukue fursa hii kukushukuruni nyinyi waandishi wa habari kwa mashirikiano yenu kwetu na kuitikia wito wetu kila tunapowaita kuja kutusikiliza. Naamini, kama ilivyo kawaida yenu, leo pia mtatusikiliza kwa makini na kisha mtawafikishia wananchi yale ambayo tumewaeleza.
Ndugu Wanahabari; katika siku za hivi karibuni juhudi mbalimbali za kuikwamua Zanzibar, kutokana na mkwamo wa kisiasa uliosababishwa na kitendo binafsi na kilicho kinyume na sheria za nchi cha Jecha Salim Jecha kufuta matokeo halali ya Uchaguzi Mkuu wa 25 Oktoba 2015 kwa lengo la kukinusuru chama chake CCM kufuatia kushindwa katika uchaguzi huo, ziliendelea.
Hivi tunavyozungumza Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amekamilisha ziara yake ya kikazi katika nchi za Marekani na Canada ambapo alikutana na Mamlaka na taasisi mbalimbali za nchi hizo kwa madhumuni ya kuelezea kadhia ya Zanzibar inayotokana na uvurugwaji wa demokrasia na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Katika ziara yake hii, Maalim Seif amepata mapokezi, heshima kubwa na uungwaji mkono wa hali ya juu. Katika jiji la Washington DC kwa mfano, Maalim Seif Sharif Hamad, alikutana taasisi na mamlaka mbali mbali ikiwa ni pamoja na Rais wa Taasisi ya International Republican Institute (IRI), Balozi Mark Green), Mkurugenzi wa masuala ya Afrika katika Taasisi ya Center for Strategic and International Studies (CSIS) Jennifer Cooke, na Naibu Mkurugenzi anayeshughulika na Afrika Mashariki na Kusini wa Taasisi ya National Democratic Institute (NDI), Marcedeh Momeni kwa lengo la kujadili na kutathmini hali ya kisiasa Zanzibar kufuatia Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Wananchi – CUF (JUVICUF), inampongeza kwa dhati, na kumuunga mkono Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ni Rais halali wa Wananchi wa Zanzibar kupitia uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015, kwa jitihada zake hizi anazoendelea kuzichukuwa.
Sisi Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Wananchi – CUF, tunamuahidi Maalim Seif Sharif Hamad, kuwa tuko pamoja naye na hatutorudi nyuma katika kuhakikisha maamuzi ya wazanzibari waliyoyafanya kupitia njia za kidemokrasia tarehe 25 Oktoba 2015 YANAHESHIMIWA, na HAKI yao inapatikana.
JUVICUF tunamhakikishia Maalim Seif Sharif Hamad kutumia ushawishi wetu tulionao kwa idadi kubwa ya vijana wa nchi hii kupigania haki zetu na za wazanzibari wenzetu licha ya kuwepo kila aina ya njama za kutufunga midomo zinazofanywa na watawala waovu kwa kuwatumia vibaraka wao walio katika maeneo na mamlaka mbali mbali za nchi yetu.
JUVICUF haitotetereka wala haitokubali kurejeshwa nyuma kwa vitimbi vya watawala waovu vyenye lengo la kuzima sauti na madai dhidi ya haki zetu. Badala yake, JUVICUF itaunganisha nguvu za vijana madhulumu wa Zanzibar na kutumia ari na nguvu zao kuhakikisha mtawala muovu anang’oka katika khatamu za Dola ya Zanzibar kwa kutumia njia za kidemokrasia zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria za nchi.
Msimamo huu wa JUVICUF hautokani na khulka ya ubishi, ubabe, ama kibri kinachotokana na nguvu, bali silka ya uzalendo wa kuitetea nchi yetu na kupigania haki zetu za kiraia zilizoorodheshwa katika Katiba yetu. JUVICUF inaongozwa na Utaifa na kuamini katika ustaarabu wa siasa za kweli za mfumo wa vyama vingi, badala ya kujigamba na kutisha wananchi kwa kumiliki vifaru na silaha za moto kama inavyofanywa na watawala madikteta na kuigwa na watawala wetu wa Zanzibar waliojiweka katika madaraka ya nchi kupitia vikosi vya Ulinzi na Usalama. Hivi karibuni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, aliyejiweka madarakani kinyume na sheria za nchi, Ali Mohamed Shein, alinukuliwa na vyombo mbali mbali vya habari akijinasibu kuwa hamuogopi yoyote kwa kuwa yeye ndiye anaye miliki silaha tulizozitaja.
Ndugu Wanahabari, tumekuiteni hapa leo kwa lengo la kukuelezeni, na kupitia nyie kuwaeleza wananchi na kuutanabahisha ulimwengu juu ya matukio ya kihuni, kinyama na yasiyo ya kiungwana yanayofanywa na watawala waovu dhidi ya raia wasiokuwa na hatia kufuatia uamuzi wa wananchi hao kuamua kutoitambua serikali iliyojiweka madarakani kwa mtutu wa bunduki baada ya kusaliti matakwa na matarajio na matlaba ya wananchi hao.
Licha ya kujiweka madarakani kwa njia ya mtutu wa bunduki na kushika khatamu za dola, baada ya kupindua maamuzi ya wazanzibari ya tarehe 25 Oktoba 2015, serikali iliyo chini ya watawala wasiokuwa na ridhaa ya wananchi imekuwa ikiratibu na kutekeleza vitendo vya KIDIKTETA, kwa kuvitumia na kuviamrisha vyombo vya Ulinzi na Usalama kukiuka Sheria za nchi na kuvunja haki za msingi za wananchi wasiokuwa na hatia.
Amri hizi za watawala wa kiimla zimepelekea vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kukiuka taratibu za kuanzishwa kwake na kufanya kazi zake kwa kuwaridhisha watawala hawa waovu walio tayari kutumia gharama yoyote, hata ikibidi kumwaga damu za wananchi, kujibakisha madarakani. Matokeo ya amri hizi za watawala hawa waovu ni kuongezeka kwa dhulma, mateso na unyanyasaji wa wananchi katika wilaya mbali mbali za Zanzibar.
Baadhi ya matendo ya ovyo yanayoendelea kuchochea kuondoka kwa hadhi ya vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama, ambayo kimsingi haipo, hasa Jeshi la Polisi lenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao, kwa lengo la kuwaridhisha watawala waovu ni pamoja na kuvamia wananchi, kuwashambulia, kwa vipigo ikiwa ni pamoja na kutumia silaha za moto, kudhalilisha wanawake, kuita watu katika vituo vya Polisi na kuwahoji kwa kutumia lugha za kibabe na vitisho, kukamata raia na kuwabambikizia kesi zinazotokana na matukio ya hujuma yanayofanyika katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar ambazo nyingi zinaratibiwa na kutekelezwa na makundi ya kiharamia yanayofadhiliwa na CCM.
Ndugu wanahabari, mfano wa maelezo tunayoyatoa kwenu kuhusu unyama wa vyombo vya Ulinzi na Usalama, yanadhihirika katika matukio ya hivi karibuni yaliyofanywa na askari wa jeshi la Polisi dhidi ya raia wasiokuwa na hatia katika maeneo mbali mbali ya visiwa vyetu vya Zanzibar. Kwa mfano, usiku wa tarehe 19 Juni, 2016 askari wa Jeshi hilo lilivamia kisiwa cha Mtambwe na kuwashambulia raia wa kisiwa hicho kwa mfululizo wa mabomu ya machozi usiku kucha.
Aidha, Jeshi la Polisi limekuwa likiwakamata kiholela wananchi wasio kuwa na hatia, hasa wafuasi na wanachama wa chama cha wananchi CUF, na kuwabambikizia makosa ambayo kiuhalisia ni ya kutengenezwa na kupangwa na genge la Wahafidhina.
Kwa mfano, siku ya Alkhamis tarehe 9 Juni, 2016 Jeshi la Polisi liliwakamata wananchi wafuatao wa shehia ya Kiwani na Shehia ya Kendwa:
S/N JINA JINSIA UMRI KITUO CHA POLISI
1 Said Ali Abdalla Me 25 Chake chake
2 Twahir Moh’d Mussa Me 24 Chake chake
3 Othman Yahya Said Me 48 Chake chake
4 Ali Omar Abdalla Me 28 Chake chake
5 Nassor Hafidh Moh’d Me 70 Chake chake
6 Moh’d Juma Khamis Me 65 Chake chake
7 Vuai Haji Vuai
Me 70 Chake chake
8 Omar Salim Juma Me 25 Chake chake
9 Moh’d Othman Faki Me 70 Chake chake
Mbali na kamata kamata hii ya raia wasio na hatia, Jeshi la Polisi limekuwa pia likiwaita baadhi ya wananchi katika vituo vya Polisi na wakati mwengine kuwasafirisha kwenda Makao Makuu ya Polisi kwa kisingizio cha kuwahoji kutokana na tuhuma mbali mbali. Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya wananchi wasiokuwa na hatia walioitwa na Polisi kwa mahojiano katika kituo cha Polisi Konde, kisiwani Pemba:
S/N JINA JINSIA KITUO CHA POLISI KIJIJI
1 Hamad Bakar Ali Me Konde Tumbe
2 Nassor Sleiman (Cholo) Me Konde Tumbe magharib
3 Ali Haji Mjaja Me Konde Tumbe mashariki
4 Bakar Hamad Shehe Me Konde Tumbe mashariki
5 Ali Khamis Kale Me Konde Tumbe
6 Masssoud Salum Said Me Konde Tumbe magharib
Hali hii na utendaji wa aina hii wa Jeshi la Polisi imekuwa ikiwakosesha amani wananchi hawa kwani wamekuwa wakiishi kwa khofu kutokana na vitisho vya Jeshi hilo nyakati za mahojiano na kukosa raha, kwa sababu ya usumbufu wanaoupata wa kuitwa Polisi mara kwa mara, katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani huku wakikabiliwa na ukata wa hali ngumu kulikosababishwa na kupanda maradufu kwa gharama za maisha kunakotokana na vikwazo na kutengwa kwa Zanzibar kufuatia kiburi na ghilba za watawala waovu.
Pamoja na matukio haya, jana Alkhamis tarehe 23 Juni, 2016 kikundi cha askari wa vikosi vya SMZ wakiongozwa na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) walivamia eneo la Tomondo na kuwafyatulia wananchi wa eneo hilo risasi na kuwajeruhi sehemu mbali mbali za miili yao wananchi wasio na hatia.
Katika hujuma hizi wananchi watatu walijeruhiwa vibaya kwa risasi za moto. Waliojeruhiwa ni pamoja na: Salim Masoud mwenye umri wa miaka kumi na nane (18) ambaye alijeruhiwa kwa kupigwa risasi ya mkono wa kulia, Yussuf Ali Juma (23) amejeruhiwa kwa kupigwa risasi ya mkono wa kushoto, na Ibrahim Shaame Ali (18) amejeruhiwa kwa kupigwa risasi ya shingo.
Tukio hili la kuwafyatulia risasi wananchi wasio na hatia limelenga kuhalalisha mpango haramu wa watawala wa CCM kuhujumu mali za wananchi, ikiwemo kuteketeza kwa kuyakata na kuyachoma moto mazao ya wananchi, kama inavyotokea katika kisiwa cha Pemba, na kukamata mifugo, kama inavyotokea sasa sehemu mbali mbali za kisiwa cha Unguja.
Dhamira kubwa ya utekelezaji wa mkakati huu ni kuwakomoa, kuwavunja moyo, na kuwanyamazisha wananchi walioamua kupaza sauti zao dhidi ya dhulma za watawala waovu waliojiweka madarakani kwa nguvu ya mtutu wa bunduki. Pia mpango huu umelenga kuamsha hamasa kwa lengo la kuzusha taharuki miongoni mwa wananchi wa Zanzibar ambao wengi wao wakiwa ni Waislamu wanaoendelea na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani ili kuvipa vyombo vya Ulinzi na Usalama sababu na uhalali wa kuwashambulia kama ilivyotokea jana.
Ili kuficha kilichotokea, Jeshi la Polisi lilijipa dhamana ya kuwazuia waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao ya kukusanya taarifa kwa lengo la kuzichapisha katika vyombo mbali mbali vya habari wananvyoviwakilisha hapa Zanzibar. Kwa mfano, wakati waandishi wa habari wakitekeleza majukumu yao ya kukusanya taarifa za tukio hili katika hospitali ya Al Rahma, Jeshi la Polisi lilimkamata na kumuweka chini ya ulinzi mwandishi wa habari na mwakilishi wa gazeti la Tanzania Daima ndugu Talib Ussi Hamad.
Kitendo cha kuwazuia waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao na kumtisha mwandishi Talib Ussi Hamad kwa kumuweka chini ya ulinzi ni kitendo kinacholenga kuendeleza mkakati wa kuvinyamazisha vyombo vya habari na waandishi wa habari ili waogope kuanika uovu unaofanywa na watawala waovu.
JUVICUF tunalaani vikali vitendo hivyo vya hujuma vinavyoshamiri kila uchao katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar na inaichukulia hatua hii ya vyombo vya Ulinzi na Usalama, kukiuka taratibu zake za utendaji na kutekeleza uhuni dhidi ya raia wanyonge, unatokana na:
1. mwendelezo wa utekelezaji wa mkakati wa kutisha raia na kuwanyamazisha ili kupunguza kasi zao za kuidai haki yao ya msingi ya kidemokrasia iliyoporowa na Wahafidhina na madalali wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015.
2. Tahayuri kubwa iliyowapata watawala hawa kwa kujiweka madarakani kwa mtutu wa bunduki, katika karne hii ya ustaarabu wa hali ya juu na uungwana uliotukuka, imewafanya kuchanganyikiwa, baada ya jumuiya zote, za kikanda na kimataifa, kuwafedhehesha na baadhi kuwatenga, wameamua kudhihirisha ghadhabu zao kuwaadhibu wananchi waliojidhatiti kuwakataa na kutowatambua wao binafsi na serikali yao haramu iliyojiweka madarakani kinyume na utaratibu na kuamua kuisusia na kuapa kutoshirikiana nayo.
3. Maya waionayo watawala waovu mbele ya uso wa ulimwengu, baada ya mbinu zao ovu za kukiuka demokrasia kudhihirika wazi wazi na kila mtu kuzishuhudia na kuzithibitisha.
Kutokana na hali hii: sisi katika JUVI-CUF:
1. Tunamtaka Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ernest Jumbe Mangu kuwafukuza kazi mara moja watendaji walio chini yake na waliopewa dhamana ya Jeshi hilo kwa upande wa Zanzibar, Kamishna Hamdani Omar Makame na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya jinai (DDCI), Salum Msangi, kutokana na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za nchi na matakwa ya kanuni na maadili ya Jeshi la Polisi na kutenda kazi zao kwa kufuata maelekezo nje ya Malaka hiyo na amri za wanansiasa wa CCM. Utendaji wa aina hii utasababisha maafa makubwa miongoni mwa wananchi wasio na hatia waliochoka kudhalilishwa na kuonewa bila ya makosa.
2. Inawataka vijana wote wa Zanzibar kufuata maelekezo ya viongozi wa Chama cha Wananchi CUF ya kutokubali, kwa namna yoyote, kuendelea kuonewa na kuhujumiwa na kwamba ni haki yao ya kikatiba na kimaumbile kujitetea na kujihami kutokana na aina zote za hatari, ikiwemo unyanyasaji na udhalilishaji wa haki na heshima ya utu na ubinadamu wao kwa mujibu wa sheria za nchi na matakwa ya katiba ya Zanzibar.
3. JUVICUF inawatanabahisha vijana wote wa Zanzibar na wananchi wote kuwa kamwe wasikubali kurejeshwa nyuma na kukatishwa tamaa na vitimbi vya watawala waliokosa uhalali na ridhaaa ya wananchi. JUVICUF inawaunga mkono vijana na wananchi wote walioamua kufuata maelekezo ya viongozi wa chama kwa kuendelea kuigomea na kutoipa mashirikianao serikali ya kidikteta na kutekeleza mgomo dhidi ya madhalimu na vibarakja wao wote.
4. Inawatanabahisha watawala wa kiimla, waliokosa ridhaa ya wananchi na kuamua kujiweka madarakani kwa mtutu wa bunduki, kwamba taarifa zao na vibaraka wao wote kuhusiana na uhuni wao wa kisiasa wa kudhalilisha na kuonea raia, waliowakataa kwa kutumia njia za kidemokrasia, zinahifadhiliwa na kwamba JUVICUF itakuwa mstari wa mbele kuchochea hatua zote za kuhakikisha taarifa za uhuni huu unaoendelea unawasilishwa katika mamlaka za kimataifa zinazohusika na kuchukua hatua kwa matendo ya aina hii.
5. Inaziomba Jumuiya za kimataifa ziendelee kufuatilia kwa karibu matukio yanayoendelea Zanzibar na mwenendo wa mambo kwa ujumla na kuendelea kuweka kumbukumbu ya matukio haya kama ushahidi wa uvunjwaji wa wajibu wa Mikataba ya Kimataifa inayohusu haki za binadamu na Utawala bora ukiwemo ule unaohusu wajibu wa Tanzania katika Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Ahsanteni sana
HAKI SAWA KWA WOTE.
MAHMOUD A. MAHINDA
KATIBU MTENDAJI – JUVICUF.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment