MAAZIMIO NA MAAMUZI YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LILILOKUTANA KWENYE MAKAO MAKUU YA CHAMA, MJINI ZANZIBAR
TAREHE 27 SEPTEMBA, 2016
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) limekutana leo, Jumanne, tarehe 27 Septemba, 2016 katika kikao cha dharura kilichofanyika Makao Makuu ya Chama, mjini Zanzibar na ambacho kiliitishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa mujibu wa Katiba ya Chama ya 1992 (Toleo la 2014), Ibara ya 80 (1). Wajumbe 43 kati ya wajumbe 53 wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa walihudhuria kikao hicho.
Agenda tatu zilizotayarishwa na kuwasilishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa zilijadiliwa na kufanyiwa maamuzi ambazo ni:
1. Kujadili barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya tarehe 23/09/2016;
2. Kupokea na kujadili mashtaka dhidi ya Prof. Ibrahim Lipumba kutokana na hujuma alizozifanya tarehe 24/09/2016 Afisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es Salaam;
3. Kumjadili na Kumhoji Prof. Ibrahim Lipumba mbele ya kikao na kumchukulia hatua za kinidhamu.
Baada ya mjadala wa kina wa agenda hizo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limefikia maazimio na maamuzi yafuatayo:
KUHUSU BARUA YA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA YA TAREHE 23/09/2016:
1. Baraza Kuu limeukataa ushauri, msimamo na mwongozo wa Msajili wa Vyama vya Siasa alioutoa kupitia barua yake ya tarehe 23/09/2016 kwa sababu Sheria ya Vyama vya Siasa (Political Parties Act, No. 5 of 1992) – Sura ya 258 haimpi mamlaka wala uwezo wowote kutoa ushauri, msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi ya vikao vya Chama na kwa kulitambua hilo ndiyo maana katika matamko yake yote aliyoyatoa, Msajili huyo ameshindwa kutaja kifungu gani cha sheria hiyo kinampa uwezo huo.
2. Baraza Kuu limesikitishwa sana na kitendo cha Jaji Francis Mutungi kujishushia hadhi, kujifedhehesha na kujivunjia heshima mbele ya macho ya jamii ndani na nje ya nchi, yeye na Ofisi anayoiongoza kwa kuvunja sheria na kudharau maamuzi ya Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia UAMUZI wa tarehe 9/5/2005 wa Jaji T.B. Mihayo katika kesi ya Emmanuel Nyenyemela na Magnus Msambila v/s Registrar of Political Parties & Others (Civil Case No. 6 of 2003) ambapo Jaji Mihayo aliamua kwamba:
“… I do not see anywhere in the Political Parties Act where the Registrar has power to bless or condemn meetings of political parties or decisions that they make.”
Tafsiri yake ikiwa ni kwamba, “… Sioni popote katika Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo Msajili ana madaraka ya kubariki au kupinga vikao vya vyama vya siasa ay maamuzi ambayo vikao hivyo vinafanya.”
3. Baraza Kuu limemuagiza Katibu Mkuu wa Chama kumjibu kwa maandishi na kwa kina Msajili wa Vyama vya Siasa na kumueleza maamuzi ya Baraza hilo ambalo kikatiba ndilo lenye madaraka ya kusimamia uendeshaji wa Chama kwamba halitambui ushauri, msimamo na mwongozo huo na limeutupilia mbali kwa kukosa kwake mantiki, hoja na pia kukosa nguvu za kisheria.
4. Baraza Kuu linamtanabahisha Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba atabeba dhamana kwa yote yaliyofanywa na yatakayofanywa na Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake cha wahuni ambacho kilivamia Ofisi Kuu ya CUF, Buguruni, Dar es Salaam tarehe 24 Septemba, 2016 na kupiga watu na kufanya uharibifu wa mali kutokana na tamko lake hilo ambalo halina msingi wa kisheria.
KUHUSU MASHTAKA DHIDI YA PROF. IBRAHIM LIPUMBA KUTOKANA NA HUJUMA ALIZOZIFANYA TAREHE 24/09/2016 AFISI KUU YA CHAMA, BUGURUNI, DAR ES SALAAM:
1. Baraza Kuu limepokea mashtaka dhidi ya Prof. Ibrahim Lipumba yaliyoandaliwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ambayo kwa mujibu wa Katiba ya Chama, Ibara ya 108 (1) ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia nidhamu ya Chama katika ngazi ya Taifa na kuyawasilisha mapendekezo yake mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
2. Baraza Kuu limeridhika kwamba Kamati ya Utendaji ya Taifa imefuata masharti yote ya Katiba ya Chama ya 1992 (Toleo la 2014) katika kuanda mashtaka hayo kutokana na mtuhumiwa, Prof. Ibrahim Lipumba, kuvunja Katiba ya Chama, Ibara ya 12 inayohusu ‘Wajibu wa Mwanachama” hasa Ibara ndogo za 12 (6), 12(7) na 12(16).
KUHUSU KUMJADILI NA KUMHOJI PROF. IBRAHIM LIPUMBA MBELE YA KIKAO NA KUMCHUKULIA HATUA ZA KINIDHAMU:
1. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeridhika kwamba Kamati ya Utendaji ya Taifa ilimfikishia mtuhumiwa, Prof. Ibrahim Lipumba, barua ya wito (Kumb. Nam. CUFHQ/OKM/WM/2016/Vol.1/49 ya tarehe 24/09/2016) ambayo pia ilikuwa na maelezo ya tuhuma na kumtaka afike mbele ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kilichofanyika leo, tarehe 27 Septemba, 2016, mjini Zanzibar kuja kujieleza na kujitetea kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Katiba ya Chama kwa kuvunja masharti yanayohusu “Wajibu wa Mwanachama” Ibara ya 12(6), 12(7) na 12(16).
2. Baraza Kuu limesikitishwa na dharau iliyooneshwa na Prof. Ibrahim Lipumba dhidi ya kikao hiki ambacho ni chombo cha juu chenye mamlaka ya kusimamia uongozi wa Chama pamoja na kupelekewa wito wa kumtaka afike mbele yake. Kitendo hicho cha dharau kinaonesha tu jinsi gani heshima na uaminifu wa Prof. Ibrahim Lipumba kwa Chama ulivyoshuka.
3. Baraza Kuu limeridhika kwamba kwa kuwa Prof. Ibrahim Lipumba akiwa mtuhumiwa alichagua mwenyewe kudharau wito wa kufika kujieleza na kujitetea ambayo ni haki yake kama mwanachama kwa mujibu wa Ibara ya 11(6) ya Katiba ya Chama, halikuwa na sababu ya kutoendelea kumjadili na kuchukua hatua dhidi yake.
4. Baraza Kuu limeridhika na mashtaka dhidi ya Prof. Ibrahim Lipumba kwamba kwa kitendo chake cha kuongoza na kusimamia kikundi cha wahuni kuvamia Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es Salaam, siku ya Jumamosi, tarehe 24 Septemba, 2016 na watu hao aliowaongoza na kuwasimamia kupiga walinzi waliokuwepo, kuvunja na kuharibu mali za Chama na hivyo kuharibu heshima na taswira ya Chama mbele ya jamii ndani na nje kwamba amtenda makosa kinyume na “Wajibu wa Mwanachama” kama ilivyoelezwa kwenye Ibara ya 12(6), 12(7) na 12(16) za Katiba ya Chama.
5. Baada ya kuridhika na mashtaka hayo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeamua kwa kutumia uwezo wake kwa mujibu wa Ibara ya 10 (1) (c) na kwa kura zote 43 za wajumbe wake waliohudhuria kumfukuza uanachama Prof. Ibrahim Lipumba, kuanzia tarehe ya leo, Jumanne, tarehe 27 Septemba, 2016.
6. Kwa maamuzi haya, Baraza Kuu linaweka bayana kwa wanachama wa CUF, Watanzania na mamlaka zote nchini kwamba kuanzia tarehe ya leo, Prof. Ibrahim Lipumba hana haki ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na shughuli zozote za Chama.
MWISHO:
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linawapa pole wanachama wa CUF walioathirika kutokana hatua ya Msajili kuingilia mambo ya Chama kinyume na uwezo alio nao na pia kwa matendo ya kihuni yaliyofanywa na Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake kuvamia Ofisi Kuu ya Chama. Wakati huo huo, Baraza Kuu linawapongeza wanachama wote kwa kusimama imara kukilinda Chama chao na linawahakikishia litasimamia wajibu wake wa kikatiba kukiongoza na kukilinda Chama hiki dhidi ya njama za maadui wa ndani na nje.
HAKI SAWA KWA WOTE
BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi)
27 Septemba, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Popular Posts
- CUF wamuandikia barua Mwenyekiti wa ZEC
- TAMKO LA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA JUU YA KUTEKWA KWA MWANDISHI WA HABARI WA SAUTI YA UJERUMANI ( DW ) SALMA SAID.
- Sera ya kunena na Kutenda ya Wana CUF
- (no title)
- Toleo la Annur June 23
- Ufungaji wa Kampeni ya uchaguzi mdogo wa Dimani.
- Salam kwa Mkururinza wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment