THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF-Chama cha Wananchi)
Office of the Secretary General
Magomeni, Dar es Salaam
TAARIFA KWA WAANDISHI WA HABARI
(Press Conference)
KUHUSU KUAPISHWA KWA WAFUASI WA LIPUMBA BUNGENI DODOMA.
1. Tarehe 28 Julai, 2017 Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilikutana katika kikao chake cha dharura kilichofanyika katika ofisi ndogo ya Makao Makuu Vuga, Unguja –Zanzibar. Katika maazimo yake yaliyotolewa mbele ya waandishi wa Habari na kusomwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad ilielezwa kwa kina juu ya Njama na hila zinazovyofanywa na Serikali ya CCM ili kuihujumu CUF na kutaka kuua mfumo wa Demokrasia nchini.
2. Baada ya Kutangazwa na Spika wa Bunge Job Ndugai hatua ya kuwavua Ubunge Wabunge [8] wa CUF kwa kasi ya Ajabu (supersonic speed) na baadae haraka haraka Tume ya Taifa ya Uchaguzi[NEC] kuwatangaza wafuasi wa Lipumba kuchukua nafasi hizo bila ya kuzingatia utaratibu. Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshindwa mpaka leo kujibu hoja za Baraza Kuu na (Challenge) iliyotolewa ya kuitaka kutoa hadharani barua ya Katibu Mkuu wa CUF iliyoandikwa kwao mwaka 2015 ikiwa na majina ya wanachama wake walioteuliwa kuwa wagombea wa viti maalum vya wanawake na kuonesha iwapo hao iliowatangaza walikuwa katika mpangilio wa majina yaliyoteuliwa na Chama.
3. Wabunge wetu walifungua shauri la madai Mahakama Kuu ya Tanzania Namba 143/2017 na Shauri dogo la Madai namba 479/2017. Kutokana na michakato ya kisheria haikuwezekana Mahakama kuamua ndani ya wakati muafaka juu ya maombi ya Zuio. [Temporary Injunction and To Maintain Status Quo]. Mashauri hayo yamepangwa kusikilizwa na au kutolewa maamuzi Tarehe 8 Septemba, 2017 na Tarehe 17 Oktoba, 2017. Kutokana na hali hiyo Mahakama haijatoa ruhusa ya Wafuasi wa Lipumba Kuapishwa kuwa Wabunge au Kukataza Wasiapishwe.
4. Jana tumeshuhudilia jinsi Wafuasi wa Lipumba walivyopokelewa na Wabunge wa CCM Dodoma na kuandaliwa dhifa ya kusheherekea ushindi wa hujuma dhidi ya CUF. Hii ni mara ya kwanza kwa Wanaoitwa Wabunge wa Upinzani kuingia Bungeni kuapishwa na kusindikizwa na Wabunge wa CCM. CUF ikiwa Taasisi makini ya kisiasa nchini haitakubali kutumiwa kutengeneza Upinzani FEKI wa kisiasa wa kuisaidia CCM iendelee kubaki Madarakani.
5. Kwa hakika Spika Ndugai amepoteza sifa na haiba ya kuongozo Bunge ambalo ni mhimili mmojawapo wa Dola na ambao ulipaswa kuwa alama ya uadilifu katika nchi. Bunge lilipaswa Chombo muhimu ca Watanzania katika kuisismamia serikali ili wananchi wapate Maendeleo Endeleo, bunge lilipaswa kuwa chombo huru chenye kujisimamia, na kuacha kutumiwa na Serikali kukandamiza upinzani, kutokufuata sheria za nchi na kuminya demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini. Spika anapaswa ajitathmini na aone kwamba anahitaji watanzania wamkumbuke kwa jambo lipi baada ya kuondoka katika nafasi hiyo. Spika Job Ndugai amejidhalilisha, kuidhalilisha na kuichafua heshima na haiba ya nafasi ya Spika. Katika mazingira ya kawaida kabisa katika kipindi hiki ambacho chama kipo katika unaoitwa ‘Mgogoro wa Uongozi’ na kwamba Mashauri yanaendelea Mahakamani, hatukutarajia kama Spika, NEC na vyombo vingine vya Serikali kuweza kushirikiana kwa kasi ya ajabu kuratibu vitendo hivi vyenye nia ovu kwa ustawi wa demokrasia.
MSIMAMO NA MUELEKEO:
6. The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kinawapongeza Wabunge wote wa kambi ya upinzani Bungeni kwa umoja wao na kuweka msimamo thabiti wa pamoja na kususia kushirikiana na vibaraka wa CCM Bungeni.
7. Chama Cha CUF kupitia Baraza Kuu la Uongozi La Taifa Linaendelea na msimamo wake uleule wa kuwatambua Wabunge na Madiwani waliodaiwa kuvuliwa uanachama kuwa bado ni wanachama halali wa CUF.
8. Pamoja na hatua ya jana ya Bunge kuwaapisha Wafuasi wa Lipumba, msimamo wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa upo palepale wa kuendelea kuwatambua kuwa wao ndio Wabunge halali walioteuliwa na Baraza Kuu hapo awali na msimamo huo hautabadilika. Tunawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wetu walioonesha Msimamo usiyoyumba na kukataa kutumika kuwa sehemu ya kutaka kuiharibu Historia ya CUF katika Madai haki sawa kwa watanzania wote.
1. Mhe. Severina Silvanus Mwijage, (MB);
2. Mhe. Saumu Heri Sakala, (MB);
3. Mhe. Salma Mohamed Mwassa, (MB);
4. Mhe. Riziki Shahari Mngwali, (MB);
5. Mhe. Raisa Abdallah Mussa, (MB);
6. Mhe. Miza Bakari Haji, (MB);
7. Mhe. Khadija Salum Ally Al-Qassmy, (MB); na
8. Mhe. Halima Ali Mohamed, (MB). Na Madiwani wa Viti Maalum, Mhe. Leila Hussein Madibi (Ubungo) na Mhe. Elisabeth Magwaja (Temeke).
9. THE CIVIC UNITED FRONT-CUF haina Wabunge wapya waliopitishwa na Vikao halali vya Chama na kuwasilishwa kwa Tume ya Uchaguzi ya Taifa [NEC] na kwa Spika kwa ajili ya Kuapishwa. Hao wanaoitwa ‘Wabunge walioapishwa’ wanaungwa mkono na serikali ya CCM hawatokani na CUF.
10. Tunatoa wito kwa wanachama na viongozi wote wa CUF nchini kutowapa ushirikiano wowote ule na kutowatambua kwa nafasi hizo za ubunge FEKI waliopewa na Serikali ya CCM kwa lengo la kuihujumu Taasisi ya CUF. Kila mmoja wetu mahala alipo achukue hatua za kudhibiti hujuma hizi za Wasaliti wa Chama kwa kadri atakavyoweza.
11. Tunapenda kuwatoa hofu wanaCUF na watanzania kwa ujumla. Kwamba masuala haya bado yanaendelea Mahakamani na tunaimani kubwa na Mahakama kuwa itasimamia na kutenda Haki. Tuendelee kuwa na subira, Lazima tujue ni nani adui yetu wa demokrasia nchini, na namna gani ya kukabiliana nae. USHINDI UPO KARIBU.
HAKI SAWA KWA WOTE
Imetolewa Leo Tarehe 6/9/2017 Katika Ukumbi Wa Wabunge Wa Cuf, Magomeni –Dar Es Salaam.
MBARALA MAHARAGANDE
K/NAIBU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA-CUF TAIFA.
Mawasiliano: 0715 062 577/ 0767 062 577
maharagande@gmail.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment