Zanzibar.
CUF imetangaza majina ya wagombea waliopendekezwa kuwania ubunge na uwakilishi Zanzibar katika majimbo 50, likiwamo jina la kada wa CCM, Mohamed Hashim Ismail.
Wakati Ismail akitangazwa kuwania nafasi ya uwakilishi wa Jimbo la Dimani kwa tiketi ya CUF, Chadema imepewa jimbo moja.
Kuondoka kwa Ismail ni pigo jingine kwa CCM ambayo
katika siku za karibuni imekuwa ikipoteza wanachama wake waandamizi,
akiwamo Hassan Nassor Moyo ambaye alivuliwa uanachama kwa madai ya
kukiuka taratibu za chama.
Kupitishwa kwa majina ya majimbo 50 ya Unguja na
Pemba, ni baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya Taifa ya CUF
kilichofanyika chini ya mwenyekiti wake, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, majina matatu
yamependekezwa kupigiwa kura ya maoni ngazi ya jimbo kwa kila jimbo na
wilaya kwa wagombea wa nafasi za viti maalumu, ili kupata mgombea mmoja
kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Mkurugenzi wa mipango na uchaguzi wa CUF, Omar Ali
Shehe aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika ofisini
kwake Vuga jana, kuwa wanachama 517 walijitokeza kuwania ubunge, wakati
242 wanataka uwakilishi na 67 ni viti maalumu, huku waandishi wa habari
wanne wakifanikiwa kupenya katika hatua ya kwanza ya mchujo ya kutafuta
wagombea.
Waandishi hao wa habari, ni aliyekuwa mtangazi wa
BBC, Ali Saleh ‘Alberto’ (Mji Mkongwe), Maua Mohamed Mussa (Tanzania
Daima) ambaye anawania nafasi za viti maalumu Wilaya ya Mjini, Talib
Ussi (Mwananchi) anawania ubunge wa Jimbo la Mgogoni na Mwajuma Juma
Kombo (Majira) anayewania uwakilishi wa jimbo la Amani.
Mkurugenzi huyo alisema mchakato huo umefanyika
kwa umakini wa hali ya juu, ili kuhakikisha wanapatikani watu wenye sifa
na uwezo wa kuingia katika vyombo hivyo viwili vya kutunga sheria.
“Tumeamua kutangaza majina ya wagombea kabla ya
Tume ya Uchaguzi kumaliza kazi ya kukata mipaka mipya ya majimbo ya
uchaguzi. Hii inatokana na wenzetu (Tume ya Uchaguzi, Zec) kupoteza
mwelekeo. Wameshindwa kutangaza mipaka tangu Machi mwaka huu,” alisema
Omar Ali Shehe.
Alisema mabadiliko yoyote yatakayotokea, chama
hicho kitaamua kulingana na mazingira halisi, lakini CUF ni chama cha
siasa kina ratiba yake na lazima itekelezwe kwa wakati mwafaka na kama
mtu hayupo tayari kuendelea na safari ni bora kutangulia kuliko
kumngoja.
Wakati hayo yakitokea, wagombea watatu wa CUF
wamepita bila ya kuwa na wapinzani. Wagombea hao ni Ismail Jussa
(uwakilishi Mji Mkongwe), Mansour Yusuph Himid (uwakilishi Kiembesamaki)
na Khamis Msabah Mzee (ubunge Jimbo la Dole).
Pia, CUF haijasimamisha mgombea ubunge katika
Jimbo la Kikwajuni na badala yake imekiachia Chadema ambayo
itamsimamisha naibu katibu mkuu wake upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu
ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa) ya kuachiana majimbo.
Chanzo: Mwananchi
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment