Ibrahim Lipumba ni mchumi wa kimataifa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF). Alizaliwa Juni 6, 1952 katika Kijiji cha Ilolangulu mkoani Tabora. |
Alipata elimu ya msingi mkoani Tabora mwaka 1959 katika Shule ya Wamisionari wa Sweden waliokuwa Tanzania wakati huo, shule hiyo iliitwa “Swedish Free Mission Primary School”, alimaliza mwaka 1962 na akasoma Shule ya Kati (Middle School) mwaka 1962 – 1966 kabla ya kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika Shule ya Sekondari Tabora mwaka 1967 – 1972 kisha akaelekea mkoani Dar es Salaam na kusoma kidato cha tano na sita katika Shule Sekondari ya Pugu kati ya mwaka 1971-1972.
Alipata shahada mbili za kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mbili nyingine amezipata katika Chuo Kikuu cha Stanford, Marekani ambacho ni miongoni mwa vyuo 10 bora duniani. Shahada zote nne alizonazo ni za uchumi.
Alisoma na kupata shahada ya kwanza katika uchumi mwaka 1973 – 1976 na shahada ya Uzamili akiianza mwaka 1976 – 1978. Lipumba ni miongoni mwa Watanzania waliowahi kuweka rekodi nzito UDSM katika shahada ya kwanza, ndiye aliyekuwa mwanafunzi bora katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii akiwa amepata daraja la kwanza la juu kuliko wanafunzi wote (GPA 5) na alitunukiwa zawadi ya Makamu Mkuu wa Chuo katika Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii.
Profesa Lipumba alipojiunga Chuo Kikuu cha Stanford alisoma shahada mbili na kupata ufaulu wa heshima, kwanza alisoma na kuhitimu Shahada ya Uzamili mwaka 1977/1978 na kisha akasoma na kuhitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika uchumi kati ya mwaka 1978 – 1983. Kwa ujumla, elimu ya uchumi ya Profesa Lipumba imejikita katika masuala ya fedha na biashara za kimataifa na eneo la pili ni maendeleo ya uchumi na uchumi wa kilimo.
Kwa miaka mingi sasa Profesa Lipumba amekuwa mhimili mkubwa wa masuala mbalimbali ya uchumi duniani, ameshiriki katika majopo ya wanazuoni nguli wa uchumi duniani katika kutafuta mbinu bora za kusaidia nchi zilizoendelea na zinazoendelea ili kujikwamua kiuchumi. Ameshiriki moja kwa moja katika shughuli za kitaalamu kutathmini uchumi wa nchi nyingi duniani na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua, amefundisha katika vyuo vikuu vinavyoheshimika duniani na amewatumikia Watanzania katika nyanja za kiuchumi kwenye Serikali kadhaa.
Alianza ajira akiwa mhadhiri msaidizi UDSM na akawa mhadhiri mwandamizi baada ya kuhitimu PhD, alikuwa profesa mshiriki kuanzia mwaka 1989 kabla ya kuwa profesa miaka ya 1990.
Kimataifa amekuwa profesa mwalikwa katika Kituo cha Maendeleo ya Uchumi katika Chuo cha Williams Marekani 1989 – 1993, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Uchumi (UNU/WIDER) kilichopo Finland mwaka 1993 – 1995.
Amekuwa akisimamia masuala ya uchumi wa dunia kwa ngazi ya ushauri wa kimataifa, amekuwa mchumi mshauri wa Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia, Shirika la Fedha Duniani (IMF), UNDP, Sida, Norad, Danida, mashirika ya kikanda kama Comesa na baadhi ya nchi za Afrika, Ulaya na Asia.
Amefanya kazi kubwa za kiushauri ili kuinua mashirika mbalimbali ya umma nchini, amewahi kuwa mjumbe wa bodi ya TKAI, NIC, TWICO, Imara Wood Industries, Tume ya Rais ya kushughulikia masuala ya uchumi wakati wa Awamu ya Pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi, mwenyekiti wa tume kadhaa zilizoundwa na Rais za uchunguzi wa matatizo ya mashirika mbalimbali ya umma.
Profesa Lipumba amezaliwa na kukulia katika familia ya kisiasa. Baba yake mzazi ni miongoni mwa waasisi wa Tanu na alishiriki mkutano wa mwaka 1958 uliojadili kuharakishwa kwa uhuru wa Tanganyika. Mwenyewe amekuwa kada wa Tanu na baadaye CCM tangu akisoma hadi alipokuwa anafanya kazi.
Miaka michache baada ya vyama vingi kuanzishwa alijiunga na CUF. Moja ya mambo yaliyomsukuma ni kule kuona mambo mengi ambayo yeye na wenzake walikuwa wakiishauri Serikali ili kuinua uchumi wa nchi yalikuwa hayafanyiwi kazi au yanafanyiwa kazi kisiasa na matokeo yake uchumi unazidi kudidimia na umaskini unaongezeka. Profesa Lipumba ameoa na ana watoto wawili.
Mbio za ubunge
Profesa Lipumba hajawahi kugombea ubunge tangu alipojiunga na siasa.
Mbio za urais
Profesa Lipumba alianza mbio za urais mwaka 1995 kupitia CUF akaibuka nafasi ya tatu kwa asilimia 6.43, akiwa nyuma ya mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa (asilimia 61.82) na Augustine Mrema wa NCCR (asilimia 27.77).
Mwaka 2000, aligombea urais kwa mara ya pili na kushika nafasi ya pili akipata asilimia 16.26 ya kura zote. Huu ni uchaguzi ambao Rais Mkapa wa CCM aliibuka mshindi kwa kupata asilimia 71.74 ya kura zilizopigwa.
Mwaka 2005, CUF ilimpa tena kazi hiyo kwa mara ya tatu, alipambana vilivyo na mwanasiasa maarufu wakati huo, Jakaya Kikwete wa CCM na kushika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 11.68. Kikwete alikuwa na asilimia 80.28.
Mwaka 2010, CUF ilimtaka akatupe karata kwa mara ya nne, safari hii aliibuka mshindi wa tatu kwa kupata asilimia 8.28 nyuma ya Rais Kikwete wa CCM aliyekuwa na asilimia 62.83 na Dk Willibrod Slaa wa Chadema aliyepata asilimia 27.05.
Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Profesa Lipumba ni mmoja wa Watanzania mashuhuri wanaotajwa kuwa na sifa, uwezo, vigezo na nafasi ya kuwa Rais wa Tanzania, hasa ikizingatiwa kuwa vyama vya upinzani vyenye wabunge nchini vimeweka azimio la kusimamisha mgombea urais mmoja kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mwezi uliopita akiwa mkoani Tabora alitangaza kwamba atachukua fomu na kukiomba chama chake kimpe fursa ya kufanyiwa tathmini na wagombea wengine wa Ukawa ili kumpata mtu mmoja atakayesimama katika nafasi hiyo.
Nguvu yake
Sifa na nguvu yake ya kwanza ni umaarufu na kuheshimika ndani na nje ya nchi. Hakuna mahali popote katika nchi hii utakapotaja jina lake watu wasimfahamu, lakini hata kimataifa wanamfahamu vizuri kwa uchapakazi wake na misimamo yake katika ukuzaji wa uchumi.
Kinachonistaajabisha ni kuwa, si mtu wa kupenda kutumia umaarufu wake kufanya “siasa rahisi” (cheap politics). Anaamini kuwa siasa si ujanjaujanja wala jambo la masihara.
Lakini jambo la pili ni uadilifu na uwazi. Kwa bahati nzuri nimefanya kazi naye kwa zaidi ya miaka mitano na namfahamu katika eneo hili. Hata mara moja ndani ya chama chake hawezi kujaribu kuingilia masuala ya fedha na hayamhusu kabisa lakini pia anachukia mbinu zozote zile ambazo zinaweza kufanywa ndani ya chama chake na hata nje, ambazo zitaleta taswira ya kukosa uaminifu kwenye fedha.
Nadhani ndiyo sababu kuu kwamba CUF kwa muda mrefu imekuwa ikipata madhara kidogo katika ukaguzi wa hesabu zake za fedha, kulinganisha na vyama vingine vyote vinavyopokea ruzuku kutoka serikalini na hata michango ya wanachama.
Tatu, Profesa Lipumba ni mtu wa kawaida na anaishi maisha ya kawaida. Hupenda kufanya mazoezi mara kwa mara na haiwezekani apite bila kukusalimia. Nakumbuka mwaka 1995 alipoanza kampeni za urais alikuwa anatumia “kigari” cha milango miwili tu, wa dereva na wa kwake, alikitumia kuzunguka nchi nzima bila kuhofia kuwa hadhi yake si ya kuendeshwa na kigari kama kile. Ni wanasiasa wachache Afrika wenye ustahimilivu na maisha haya.
Ni Mtu wa kujitolea. Nimeshuhudia CUF ikimlipa kiongozi huyu shilingi milioni moja tu kwa mwezi za posho (CUF hawalipi mishahara). Kwa mwaka, anaweza kutumia posho yake ya miezi hadi sita akielekeza (posho nzima) ipelekwe mahali fulani kusaidia wagonjwa au watu wengine. Kuna wakati amewahi kuniagiza (nikiwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF), kupeleka posho yake yote ya mwezi kwa waathirika wa mabomu ya Arusha. Haishi kwa kutegemea siasa, anaamini siasa si ajira wala sehemu ya kujinufaisha na ndiyo maana hata mimi hadi leo hii nimekuwa na mtazamo na msimamo wa namna hiyo.
Mwisho, huenda ndiye mwanasiasa pekee (kwa siasa za kuanzia mwaka 1995 – 2015) aliyewahi kuzunguka Tanzania na kushuhudia matatizo ya wananchi kuliko mtu mwingine yeyote. Kila mwaka anatumia wastani wa siku hadi 130 akiwa kwenye ziara za ujenzi wa chama mikoani lakini kila baada ya miaka mitano kuanzia mwaka 1995 alipata wasaa wa kuzunguka, bila kupumzika, kwenye majimbo yote kuomba kura kwa wananchi. Sijui nani mwingine ameweka rekodi hii.
Udhaifu wake
Kwa siasa za Tanzania, moja ya udhaifu mkubwa wa Profesa Lipumba ni kuchukulia kila jambo kitaaluma, “He is too academic”. Hali hii inamfanya wakati mwingine asieleweke kwa watu wanaomsikiliza. Mathalan, anaweza kuhutubia wananchi na akatumia muda mwingi kutoa takwimu za Benki ya Dunia au masuala ya tafiti za kutaalamu. Watanzania wengi hawana elimu kubwa na hata waliosoma wana ufahamu wa kadri mno, kuwapangia mikakati ya uhuishaji wa siasa na nchi kitaaluma kunawafanya wasijue mipango inayoongelewa.
Kuna wakati huzungumzia masuala ya uchumi na maendeleo na akamaliza mkutano na waandishi wa habari, akishaondoka waandishi wanakufuata na kukuuliza mambo mengi yanayohitaji ufafanuzi. Akiwa mtu ambaye anatajwa kuwa na sifa na vigezo vya urais, udhaifu huu unamfanya asifikishe ujumbe wake wa mabadiliko kirahisi.
Pili, ni mtu aliyeweka familia yake mbali na siasa, Hili si jambo dogo. Kuna watu hawakumpigia kura katika chaguzi alizoshiriki kwa kupewa propaganda kali kuwa hana mke na hajawahi kuwa na mke wala mtoto. Ukweli ni kuwa Lipumba ana mke na watoto wawili wakubwa, ni mmoja wa wanasiasa wenye familia na ndoa imara huku akijua majukumu yake ya ulezi wa familia katika jamii. Sielewi kwa nini hapendi kuchanganya familia yake na siasa kwa sababu taswira anayoipata kwa jamii kutokana na uamuzi huo nadhani siyo nzuri. Ndiyo maana wengi wanadhani yeye ni “Senior Bachelor”.
Mwisho, kuna nyakati hatumii nafasi yake ya uenyekiti wa chama sawasawa. Ameacha mambo mengi yaamuliwe kwa mawazo, maoni na ushauri wa watu waliomzunguka kuliko kufanya uamuzi mgumu wakati mwingine akiwa mwenyekiti. Anataka kila jambo liamuliwe kwa pamoja na sikuwahi kuona hata mara moja akiamua jambo peke yake, sielewi kama ni lengo la kukwepa lawama za uamuzi au ni utaratibu wake. Kwa siasa za Afrika, kiongozi wa juu wa taasisi kuna nyakati nyingi tu anapaswa achukue uamuzi mwenyewe na abebe lawama mwenyewe kwani huwezi kuwa na uhakika kama watu wote waliokuzunguka wana uwezo wa kukushauri vizuri muda wote.
Nini kinaweza kumfanya apitishwe?
Mambo kadhaa yanaweza kufanya CUF impitishe kugombea urais na kurahisisha pia tiketi yake ndani ya Ukawa:
Moja, msomi mahiri wa uchumi katika ngazi ya kimataifa na kwa Tanzania, amekuwa akionekana kama mchumi bora zaidi kuliko wote. Profesa Kitila Mkumbo, Mhadhiri wa UDSM katika andiko lake juu ya kiongozi huyu, anaeleza kuwa “…Wasomi kadhaa wa uchumi niliozungumza nao wanaamini kwamba Profesa Lipumba ndiye mchumi bora zaidi hapa Tanzania. Aidha, pamoja na kwamba yupo katika siasa, Profesa Lipumba ameendelea kuheshimika katika taaluma ya uchumi duniani. Hata hivyo, taaluma yake imekuwa haitumiki ipasavyo hapa nyumbani kwa sababu watawala wetu hujali ufuasi wa vyama zaidi kuliko utaalamu wa mtu katika kupanga watu katika nafasi nyeti za kazi”. CUF na Ukawa nadhani vinahitaji mgombea mwenye sifa hii.
Pili, naamini kwa siasa za upinzani za Tanzania, Profesa Lipumba ndiye kiongozi pekee mwenye uzoefu mkubwa wa kusimamia masuala ya kimataifa kumshinda mtu mwingine yeyote. Ametumia sehemu kubwa ya maisha yake akisimamia miradi mikubwa ya kiuchumi katika nchi nyingi na mashirika ya kimataifa duniani. Uzoefu wa kimataifa ni turufu muhimu kwa kiongozi yeyote wa kisiasa.
Mwisho, ana uzoefu mkubwa na utendaji wa ngazi ya juu ndani ya Serikali kwa sababu amefanya kazi serikalini, ameshauri mambo mengi kuhusu uhuishaji wa mashirika ya umma, amekuwa mtu muhimu kiushauri kwenye miaka ya nyuma katika Benki Kuu ya Tanzania na nyinginezo. Rekodi hizi nadhani zinakifanya chama chake kimpe nafasi kubwa kabisa kumshinda mtu yeyote yule na huenda hata ndani ya Ukawa awaka na sifa za juu kuwashinda wanasiasa wengine.
Nini kinaweza kumwangusha?
Jambo moja tu ndilo naliona kama kikwazo kwake. Ikiwa makubaliano ya ndani ya Ukawa yataonyesha kuwa CUF haipaswi kutoa mgombea urais kwa sababu labda umoja huo umeamua mgombea atoke kati ya NCCR, NLD na Chadema. Hili peke yake ndilo linaweza kumkwamisha.
Asipochaguliwa (Mpango B)
Kwa mtizamo wangu, ikiwa hatagombea urais mwaka huu na labda kutochaguliwa na chama chake, Ukawa inaweza kumtumia kugombea ubunge kwenye majimbo ya Kinondoni, Segerea au Temeke. Watu wengi niliozungumza nao wanaumia kwa kumkosa bungeni.
Mfano wa umuhimu wake kwenye vyombo vya uamuzi wa mambo makubwa ya nchi ulijidhihirisha kwenye Bunge la Katiba. Nitaumia hatagombea urais halafu tena asigombee ubunge. Pia, ikiwa Ukawa itashinda uchaguzi wa mwaka huu, simuoni waziri mkuu bora wa Serikali ya kisasa kama Profesa Lipumba.
Lakini pia kama hatagombea urais nadhani atakuwa na jukumu la kuongoza chama chake kwa miaka minne ya kipindi chake ambacho nadhani ni cha mwisho kabisa, kuendelea kuishauri Serikali ijayo bila kujali itaundwa na Ukawa au CCM na kuendelea kufanya kazi za kitaalamu za kitaifa na kimataifa.
Hitimisho
Sikupata shida kumtathmini Profesa Lipumba kwa sababu nimefanya naye kazi kwa karibu. Watu waliofanya kazi chini yake wamejifunza bidii kazini, nidhamu, kutunza muda, kuchukulia siasa kama kazi ya kujitolea na kusaidia wananchi na kuamini kuwa siasa inawajibika kutumikia uchumi. Ni mmoja wa wanasiasa wa kweli na wanaochukia mikakati ya ki-propaganda hata kutoka ndani ya chama chake. Sielewi ni wanasiasa wangapi nchi hii wana uwezo, uthubutu, elimu, umashuhuri, wajibikaji na kujituma kama kiongozi huyu. Namtakia kila lililo jema katika safari yake ndefu katika siasa za Tanzania.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment