TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu Waandishi wa habari,
Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na uzima wa afya na tukaweza kukutana hapa asubuhi hii ya leo. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa kuijaalia nchi yetu kuendelea kubaki katika hali ya amani na utulivu licha ya matatizo mengi yanayotukabili.
Pili, nichukue fursa hii kukushukuruni nyinyi waandishi wa habari kwa kuitikia wito wetu na kuja kutusikiliza. Ni imani yangu kuwa kama ambavyo mmekuwa mkitupa mashirikiano mazuri katika kuwafikishia wananchi yale ambayo chama chetu kupitia kwenu kimekuwa kikiyatolea taarifa, kwa uzito wa kipekee taarifa hii nayo mtawafikishia Watanzania wote kupitia vyombo vyenu vya habari.
Ndugu Waandishi wa habari,
Tumewaita leo hii kuwaeleza juu ya maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa katika kikao chake cha dharua kilichofanyika jana, Jumapili ya tarehe 28/08/2016 Katika ukumbi wa Makao Makuu ya Chama, ofisi za Vuga. Kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa muda Mhe, Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Jimbo la Mchinga kilihudhuriwa wa Wajumbe 46 katika ya Wajumbe 60.
Ndugu Wandishi wa Habari,
Kama mnavyojua tarehe 21/08/2016 Chama Cha Wananchi – CUF kilikuwa na Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa uliofanyika katika ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo Plaza, Dar es Salaam. Mkutano huo ulikuwa na agenda mbili kuu, ambazo ni:-
1. Kupokea barua ya Profesa Ibrahim Haruna Lipumba ya kujiuzulu nafasi yake ya uenyekiti ya tarehe 05/08/2015; na
2. Kufanya Uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi - Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wanne wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
Kufuatia hujuma za makusudi zilizoandaliwa kwa mashirikiano ya maadui wa ndani na nje ya chama, aliyekuwa Mwenyekiti wa muda wa Mkutano Mkuu Maalum, Mhe Julius Mtatiro alilazimika kuakhirisha Mkutano ule mara baada ya kumalizika kwa ajenda ya kwanza ambapo Mkutano Mkuu uliridhia kujiuzulu kwa Profesa Ibrahimu Haruna Lipumba kwa azimio lililoungwa mkono na wajumbe 476 dhidi ya wajumbe 14 waliokataa. Hivyo basi agenda namba 2 haikuwahi kukamilishwa, na kwa hivyo haikufanyiwa maamuzi.
Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi, kilichokaa jana kimejadili kwa kina juu ya hujuma za kuvuruga Mkutano Mkuu Maalum wa tarehe 21/08/2016. Baraza kuu limesikitishwa sana na kitendo kile ambacho mbali ya kukisababishia chama hasara ya zaidi ya Shillingi milioni 600, pia kimepelekea kuharibu taswira ya chama ndani na nje ya nchi.
Baraza Kuu lilipata nafasi ya kupokea maelezo ya kina kutoka kwa wajumbe mbali mbali hasa wale wanaotokea Tanzania Bara walioeleza kwamba hujuma zilizofanywa kuvuruga Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa tarehe 21 Agosti, 2016 hazikuwa za bahati mbaya au za kushtukiza bali ni matokeo ya njama na mbinu ovu na chafu ambazo zimekuwa zikipangwa na kutekelezwa chini kwa chini kwa muda mrefu. Wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa walieleza kwa ushahidi jinsi baadhi ya viongozi wa Chama walioaminiwa na kupewa nyadhifa za juu walivyogeuka na kuanza kutumiwa na maadui wa nje ya Chama kukihujumu Chama.
Baraza Kuu limezingatia kuwa CUF ni chama cha kistaarabu, ni Chama cha Kidemokrasia na ni Chama chenye kutoa matumini ya mabadiliko ya kweli kwa Watanzania walio wengi. Vurugu zilizojitokeza ni aibu na fedheha kwa chama chetu mbele ya macho ya Watanzania na wapenda demokrasia.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeridhika kwamba watu hao waliokuwa vinara wa vurugu na njama hizo ovu walipewa nafasi mara kadhaa kujirekebisha dhidi ya mwendo wao huo dhidi ya Chama lakini waliendelea na vurugu na hujuma zao hizo. Kwa hatua iliyofikia, Baraza Kuu limeona halina njia nyengine ya kukinusuru Chama isipokuwa kuchukua hatua kali na madhubuti kukilinda Chama ambao ni wajibu wake kikatiba.
Kwa msingi huu basi, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa kauli moja (unanimously) limeamua kuchukua hatua za kinidhamu kwa viongozi na wanachama mbali mbali waliohusika kwa njia moja au nyengine katika kuchochea vurugu zile. Baraza kuu limechukua hatua mbili kubwa ambazo ni kutoa karipio kali, kusimamisha na kufukuza uanachama wahusika wote walioshiriki kuchochea vurugu hizo.
Viongozi waliopewa karipio kali kwa mujibu wa Katiba ya Chama, Ibara ya 83 (5)(b) ambao ni wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ni:
1. Rukiya Kassim Ahmed na
2. Athumani Henku
Viongozi waliosimamishwa uanachama kwa mujibu wa Katiba ya Chama, Ibara ya 83 (5)(c), hadi hapo watakapopata fursa ya kujieleza mbele ya Baraza Kuu ni;
1. Prof Ibrahim Haruna Lipumba
2. Magdalena Sakaya
3. Abdul Kambaya
4. Ashura Mustafa
5. Omar Mhina Masoud
6. Thomas Malima
7. Kapasha M. Kapasha
8. Maftaha Nachumu
9.Mohamed Habib Mnyaa
10. Haroub Shamis
na
11. Mussa Haji Kombo
Mwanachama aliyefukuzwa chama ambaye alipata fursa ya kujieleza mbele ya Baraza Kuu na kikao kuamua kumfukuza chama kwa mujibu wa Katiba ya Chama, Ibara ya 83 (5)(c) ni aliyekuwa Kaimu Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wazee wa CUF (JUWACUF), Shashu Lugeye.
Kufuatia maamuzi hayo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limewateua viongozi mbali mbali kukaimu nafasi mbali mbali zilizoachwa wazi.
Kwa kuzingatia kwamba kutokamilika kwa Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa tarehe 21 Agosti, 2016 kulipelekea kushindwa kufanyika kwa uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Chama, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limetumia uwezo liliopewa na Katiba ya Chama, Ibara ya 101 na 118, kuunda Kamati ya Uongozi ambayo itakuwa ikifanya kazi za Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti hadi hapo uchaguzi wa kujaza nafasi hizo utakapofanyika. Baraza Kuu la Uongozi limewateua wafuatao kuwa wajumbe wa Kamati hiyo ya Uongozi:
1. Mhe. Julius Mtatiro – Mwenyekiti;
2. Mhe. Katani Ahmed Katani – Mjumbe; na
3. Mhe. Severina Mwijage – Mjumbe.
Aidha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, kwa kufuata Ibara ya 105 (1) na (3) ya Katiba ya Chama, limemteua Mhe. Joran Bashange kuwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama kwa upande wa Tanzania Bara na Mhe. Mbarala Maharagande kuwa Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma hadi hapo nafasi hizo zitakapojazwa rasmi kwa mujibu wa masharti ya Katiba ya Chama.
Mwisho, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linawahakikishia wanachama na wapenzi wake na Watanzania wote kwa ujumla kuwa Chama Cha Wananchi – CUF kipo imara na makini na katu hakitoyumbishwa kwa hila na njama ovu na chafu zinazofanywa na maadui wa chama hichi. Tangu kuasisiwa kwake, CUF imeandamwa na maadui wa kila aina, na imepitia katika misuko suko mingi. Tunaamini hila na njama hizo ovu zimekuwa zikielekezwa CUF kwa kutambua kwamba Chama hichi ndicho kinachobeba dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko ya kweli hapa nchini.
Kutokana na umadhubuti, umakini na uimara wa Katiba ya Chama na safu ya viongozi wake, CUF imeweza kuvuka salama kila ilipoingia katika misuko suko hiyo na kwa hivyo, hata wimbi hili lililoonekana kukitikisa Chama limekabiliwa ipasavyo na sasa kazi iliyopo mbele yetu ni kuendeleza harakati za kisiasa za kuwaletea Watanzania wa Bara na Zanzibar mabadiliko wanayoyataka.
HAKI SAWA KWA WOTE
Nassor Ahmed Mazrui
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Popular Posts
- TAMKO LA UMOJA WA KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI TANZANIA JUU YA KUTEKWA KWA MWANDISHI WA HABARI WA SAUTI YA UJERUMANI ( DW ) SALMA SAID.
- CUF wamuandikia barua Mwenyekiti wa ZEC
- Sera ya kunena na Kutenda ya Wana CUF
- (no title)
- Ufungaji wa Kampeni ya uchaguzi mdogo wa Dimani.
- Salam kwa Mkururinza wa Zanzibar
No comments:
Post a Comment