Na. Julius Mtatiro, (Darubini ya Mtatiro) – Gazeti la Mwananchi,
Jumapili, 16 Agosti 2015
Huu ni mwaka wa uchaguzi hapa nchini kwetu na wadau wa wazi wa uchaguzi ni watu mbalimbali wakiwemo wanasiasa na vyama vyao, vyombo vya ulinzi na usalamam serikali kwa ujumla na wananchi wote.
Uchaguzi ni kwa taifa zima na kila mmoja anahusika, upande wowote ambao utafanya ndivyo sivyo, uchaguzi mzima unaweza kuharibika bila kusita, ndiyo maana kila mdau na kila upande una jukumu la kujichunga sana.
Mathalani, kwenye uchaguzi kama huu ikiwa vyama vinavyopimana maguvu, vyote au kimoja kitatoka hadharani na kusema kuwa ‘Damu itamwagika” ina maana kwamba vyama vinawaandaa wananchi kumwaga damu na vinawatoa hofu kwamba “umwagikaji wa damu ni kitu muhimu” au ni kitu cha kawaida. Vivyo hivyo kwa chama kinachoongoza dola, kikitangaza kuwa ushindi wake ni wa lazima au ni wa goli la mkono n.k. ina maana kuwa chama hicho kinawaandaa wananchi kisaikolojia kukubali hali ya mambo itakavyokuwa pindi kitakapokuwa kimeiba kura au kuvuruga uchaguzi.
Moja ya mdau mkubwa sana wa uchaguzi wowote ule katika nchi yetu ni vyombo vya ulinzi na usalama hususani polisi. Jeshi la Polisi lilianzishwa kwa misingi ya kusaidia katika ulinzi wa amani na utulivu ndani ya nchi huku likiisaidia serikali “kuwarudisha kwenye mstari” wale wote wanaojaribu kuvunja taratibu zinazoongoza nchi.
Jeshi lolote la polisi duniani hufanya kazi kwa weledi (ndiyo maana kukawa na vyuo maalum vya mafunzo), weledi unatokana na mafunzo na wala si mazoea au utekelezaji wa amri zisizo halali, weledi unataka kila mara askari polisi wafanye kazi kwa mujibu wa taratibu za polisi ambazo ni kulinda sheria bila kupokea maelekezo yasiyo ya kisheria kutoka kwa watu wasio polisi.
Miaka michache iliyopita nilialikwa kuhudhuria maandamano ya wakulima wa korosho huko mkoani Mtwara katika wilaya ya Tandahimba, maandamano yale yaliripotiwa polisi na wakaahidi kuyalinda.
Waandamanaji walikuwa kwa maelfu wakielekea kwenye ofisi za mkuu wa wilaya hiyo ili kujibiwa ni kwa nini fedha zao za korosho hazikuwa zimelipwa kwa miaka kadhaa na malimbikizo yakikua.
Tulipofika kwenye ofisi za mkuu wa wilaya alikuwa na kazi ndogo tu ya kuongea na waandamanaji, hakufanya hivyo na badala yake akamuamrisha mkuu wa polisi wa wilaya (OCD) awatawanye waandamanaji mara moja.
Kwa macho na masikio yangu nilimuona OCD yule akikataa amri hiyo kwa maneno na vitendo. Akamwambia mkuu wa wilaya “Afande siwezi kufanya hivyo, toka nje uongee na wananchi uwape majibu waondoke kwa amani”. DC alirudia amri yake zaidi ya mara tatu na OCD alikataa kata kata.
Huyu OCD ni mfano wa askari mwenye weledi mkubwa wa kazi yake, alikataa amri isiyo halali tena kutoka kwa mkubwa wake wa kazi ambaye hana weledi na mambo ya polisi.
Mara nyingi sana nchi yetu inajiingiza kwenye migogoro isiyo na tija na hata kupoteza maisha ya rais kwa sababu ya “mambo ya kijinga sana”.
Mara nyingi unakuta askari wamekataa kulinda maandamano ya raia wema lakini raia hao wakijaribu kuandamana polisi wanapelekwa kwa mamia kuwadhibiti, wakati kumbe maandamano yangefanyika yangehitaji askari kumi au ishirini hadi yakafika mwisho.
Je, hata hili nalo linahitaji mafunzo kutoka ulaya kuona kuwa ni jambo jepesi sana kiutekelezaji?
Wiki hii jeshi la polisi kupitia kwa Naibu Kamishna wa jeshi hilo limeanzisha chokochoko ambazo zina dalili zote za kupoteza weledi na uwepo wa jeshi lenyewe.
Jeshi letu limepiga marufuku maandamano na mbwembwe kwenye shughuli za utafutaji wadhamini kwa wagombea wa vyama kwa kile ilichokiita “kuimarisha ulinzi” na kuondoa usumbufu kwa wananchi.
Nilishtuka sana nilipomuona na kumsikiliza kiongozi huyu mkubwa akiongea kwa niaba ya polisi.
Hivi polisi ina hofu gani na uchaguzi wa mwaka huu? Mbona ianze mikwara na marufuku zisizo na maana, mbona ianze kupanda juu ya katiba ambayo inahubiri uhuru wa kukusanyika ambao natambua umeminywa ipasavyo kupitia sheria ya ‘Polisi na Polisi Wasaidizi’?
Kwa nini siku 60 kabla ya kupiga kura ndipo jeshi linaanza kupiga marufuku maandamano? Kwamba linataka miezi hii miwili watu na vyama vyao wasijimwage barabarani kupokea wagombea, kuonesha hisia zao na mapenzi yao n.k? Mbona enzi za chama kimoja kulikuwa na maandamano na matembezi ya hisani na kila aina ya misafara ya watembea miguu wakiisifu TANU, Fikra za Mwenyekiti n.k.?
Leo hii kuna jambo lipi kubwa hadi matembezi, maandamano na mbwembwe za kisiasa vianze kupigwa vita? Naamini kuwa hapa kuna kitu jeshi la polisi linakitafuta na huwenda linataka jambo fulani litokee.
Sote tunakubaliana kuwa watanzania ni watu wanaopenda amani na wanajiheshimu sana, niliwaona majuzi wagombea wa vyama vya CCM na yule wa UKAWA kupitia CHADEMA wakikusanya mamia na maelfu ya wakazi kuelekea kuchukua fomu, pamoja na hofu za polisi bado walinzi wa vyama hivyo walifanya kazi kubwa ya kulinda utulivu wakilisaidia jeshi la polisi ambalo nalo lilikuwa “flexible” kupokea mabadiliko ya njia za waandamanaji, mahali pa kuhutubia n.k bila kuleta matata na matatizo, ama ni kwa sababu kipimo cha maandamano yale kilionesha kuwa mgombea wa UKAWA amekusanya maelfu mengi ya wananchi kuliko yule wa CCM? Na kama ndivyo, ina maana mpango huu wa polisi wa kuzuia maandamano na mbwembwe zingine za kisiasa unalenga kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kisikumbwe na aibu ya maandamano makubwa kukishinda kwenye mikoa mingine? Jamani, ama hofu ya jeshi la Polisi ni ipi?
Nataka kusema kuwa Jeshi letu ambalo watanzania wanalitegemea sana lisihame kwenye mstari wa weledi na maadili, ni vema kubaki kwenye mstari huo ili kutenda haki kwa vyama vyote kwenye uchaguzi huu kuliko kukengeuka. Zama za mabadiliko zinapofika ni vema sana vyombo vya dola vikawa watizamaji na walinzi wa amani zaidi kuliko kuanza kuingilia michakato ya kidemokrasia na kutoa amri ambazo siyo halali kama hizi za kuzuia maandamano nchi nzima kana kwamba jambo hilo ni takwa la kikatiba.
Ikiwa polisi wataendelea na chokochoko zao na zikasababisha dhahma kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kila mmoja aliyeacha weledi na kuanza kutumikia amri zisizo halali kutoka kwa wanasiasa atabeba mzigo wake na tutambebesha hasa kwa sababu tunalihitaji taifa letu na tunahitaji uhuru wetu ulindwe.
(Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala ya Kijamii na Kisiasa B.A, M.A, L LB (Completed): +255787536759, juliusmtatiro@yahoo.com).
No comments:
Post a Comment