Wakati mgombea urais wa Chadema chini ya
mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa akiiteka Wilaya ya Chato ambako ni
nyumbani kwa mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli kwa kufanya mkutano
mkubwa wa kampeni, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT)
wilayani humo, Lucas Michael alitumia nafasi hiyo kueleza kilio cha
walimu nchini na kumponda Dk Magufuli kwa kushindwa kutetea maslahi yao.
Lucas ambaye baadaye alilieleza Mwananchi
kuwa hawezi kujuta kwa kutoa kauli hiyo hadharani akieleza “sijafanya
kosa nimesema ukweli”, akiwa jukwaani alisema Dk Magufuli ambaye alikuwa
mbunge wa Chato amewatupa walimu wa wilaya hiyo kwa madai kuwa
wananunua wenyewe chaki, hawalipwi fedha za safari baada ya kustaafu na
Halmashauri ya wilaya hiyo inagoma kuwasomesha.
Wakati mwalimu Michael akieleza hayo,
Lowassa akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika stendi ya
mabasi ya zamani mjini Chato na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi
waliomsubiri kuanzia saa nne asubuhi hadi saa 10 jioni, aliahidi kufufua
viwanda vilivyopo mkoani humo na kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria baada
ya kuelezwa kero za wananchi wa wilaya hiyo na mgombea ubunge,
Benedicto Lukanima (Chadema).
Michael aliyekuwa ameshika kipeperushi
chenye picha ya Lowassa alimuomba kada mpya wa Chadema, Tambwe Hiza
aliyekuwa akizungumza jukwaani kabla ya Lowassa kufika eneo hilo, kuwa
ana ujumbe mzito kwa walimu wa Chato.
“Nimelazimika kuja hapa kuyasema
yafuatayo. Tanu ilipata nguvu baada ya Mwalimu Julius Nyerere, Oscar
Kambona na wafanyakazi wengine kuungana na Rashid Kawawa kudai uhuru wa
Tanganyika. Bila wafanyakazi kujitetea na kudai haki yao hakuna maisha
ya kweli na ya uhakika.
“Namuuliza Dk Magufuli mbona katika
halmashauri yake haisomeshi wafanyakazi, mbona wakistaafu hawapewi fedha
za safari kulejea makwao, mbona walimu tunachanga fedha kununua chaki,”
alisema na kushangiliwa na wananchi.
Huku akirejea kauli ya Dk Magufuli
aliyotoa hivi karibuni kwamba wananchi wamchague kwa kuiga mfano wa
alichokifanya Chato Michael alisema, “Wanasema tuchague CCM kwa kuiga
Chato sasa tunachagua nini kwa haya yanayotokea Chato.”
“Kazi ya mwalimu ni kufundisha elimu ya
darasani na ya watu wazima. Walimu wasiwe waoga wawafundishe ukweli watu
wao. Bendera ya taifa ina rangi ya njano, kijani, nyeusi na bluu huku
nyeupe ikiwa imeizunguka bendera hiyo hivyo walimu wafanye uamuzi sahihi
wakati sahihi na wakati ndiyo huu,” alisema Michael na kuibua shangwe
katika mkutano huo.
Michael alilieleza Mwananchi kuwa ni
mwalimu wa Shule ya Sekondari Chato tangu mwaka 2007 na kwamba alianza
kazi ya ualimu mwaka 1987.
“Nimekuwa mwenyekiti wa CWT hapa Chato
tangu Machi mwaka huu. Sihofii kufukuzwa kazi kwa sababu sijavunja
sheria. Jambo linaloniuma zaidi ni kitendo cha walimu wanaoonekana
kuunga mkono vyama vya upinzani kuadhibiwa na wale wanaounga mkono CCM
kuachwa. Jambo hili si sahihi kabisa,” alisema.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment