Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia chama
cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amewaahidi wakulima wa zao la
mwani Zanzibar kuwa atapandisha bei ya zao hilo mara moja, iwap
atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
Maalim Seif alisema bei wanayolipwa
wakulima ya shilingi 700 na 800 hivi sasa ni ndogo na hailingani na
gharama wanazozitumia wala haiwasaidii wakulima wengi wao wakiwa ni
akinamama katika kuondokana na umasikini.
Mgombea huyo ambaye pia ni Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema hayo alipowatembelea wakulima wa
mwani, wakulima wa mpunga na kukagua soko la mboga mboga na samaki
katika majimbo ya Tumbe na Konde, mkoa wa Kaskazini Pemba.
Awali katika risala ya wakulima wa mwani
na wavuvi wa maeneo hayo iliyosomwa na Aisha mour Ali walisema
wanakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa vifaa, bei isiyoridhisha na
kukosa boti za kisasa za kufanyia shughuli za uvuvi.
“Tangu 1994 tulipoanza kulima mwani
hatujafaidika na bei tunayo lipya, shilingi 700 tunazopewa hazilingani
na ugumu wa kazi hii na hilo tumelilalamikia miaka mingi”, walisema
katika risala hiyo.
Maalim Seif alisema utafiti uliofanywa
unaonesha iwapo wakulima wa mwani watawezeshwa kutumia mbegu za kisasa
na kufanya kazi kitaalamu zaidi, zao hilo linaweza kutoa mchango mkubwa
katika juhudi za kuwatoa wakulima katika umasikini.
Aliaahidi kuwa akichaguliwa kuwa Rais wa
Zanzibar atahakikisha wanaleta wataalamu wa kutosha kutoa mafunzo ya
uzalishaji bora wa zao hilo, kutafuta vifaa pamoja na mbinu mbadala
kuliongezea thamani za la mwani.
“Azma yangu ni kuona wakulima wa mwani
wananufaika na jasho lao kama vile wanavyonufaika wakulima wenzao wa zao
la karafuu”alisema Maalim Seif.
Aidha, aliahidi kuwa atahakikisha mwani
unaozalishwa Zanzibar una sarifiwa (processing) kabla a kuuzwa na
kuondokana na utaratibu wa kuuzwa mzima, utaratibu ambao huukosesha
thamani kubwa katika soko la Kimataifa.
Kilimo cha zao la mwanai kimepata
umaarufu mkubwa Zanzibar kwa kujumisha wakulima katika vijiji vya
mwambao wa bahari, wengi wao wakiwa ni akina mama, kwa mwaka wastani wa
tani 13, 000 huzalishwa Zanzibar na kuuzwa nje ya nchi.
Kuhusu uvuvi, Malim Seif alisema azma
yake ya siku nyingi ni kuhakikisha wavuvi kote Zanzibar wanapatiwa
vyombo vya kisasa vya uvuvi ambavyo vitawawezesha kufanya shughuli zao
kwa ufanisi mkubwa.
Alieleza kuwa kinachojitokeza hivi sasa
ni kupungua kwa samaki katika eneo la mwambao wa visiwa, hivyo
atahakikisha anaandaa mikakati ya kuwawezesha wavuvi wa Zanzibar ambao
wanafikia 32, 000 kufanya shughuli hizo katika bahari ya kina kirefu
ambapo kuna samaki wa kutosha.
Sambamba na mikakati hiyo, Maalim Seif
alisema atafanya kila njia kuhakikisha zao la mpunga linazalishwa kisasa
chini ya utaratibu wa umwagiliaji maji, kwa vile mchele ndio chakula
kikuu kwa watu wa Zanzibar.
Akizungumza na wakulima wa mpunga katika
mabonde la kinyakuzi na Saninga alisema nia yake ni kuhakikisha Zanzibar
inapunguza utegemezi wa bidhaa za chakula kutoka nje ya nchi na iweze
kuzalisha asilimia 60 ya mahitaji yake ya chakula hasa mchele.
“Mipango hiyo itawezekana bila wasi wasi,
nitaanzisha benki maaluma ya kusaidia wakulima, wavuvi na wajasiriamali
na wataweas kupata mikopo yenye masharti nafuu”, aliahidi Maalim Seif.
Aliwataka watendaji wa Halmshauri ya
Wilaya ya Micheweni kutafuta watu wenye uwezo wa kuliendesha soko jipya
la kisasa lililopo katika kijiji cha Tumbe ili liweze kutumika na
kuwanufaisha wakaazi wa maeneo hayo.
Chanzo: OMKR
No comments:
Post a Comment