Na Ahmed Omar
Katika vitabu vyote vya dini kubwa duniani, kuna mkasa wa Nabii Musa
aliyetumwa na Mungu kuwakomboa wana wa Israel kutoka utawala kandamizi
wa Firauni. Firauni aliwatawala kama watumwa Waisraeli na akafanya
vituko vingi duniani vya kukufuru hadi kufikia kujiita Mungu.
Mungu
alimpelekea habari Firauni kwamba angelizaliwa mtoto wa kiume ambaye
atakua nabii na kuleta nuru na ukombozi kwa watu wa Israel.
Baada ya kupata habari hizo, Firauni hakuruhusu uhai wa mtoto yeyote
wa kiume aliyezaliwa akifahamu kwamba ndiye adui kwa utawala wake.
Aliwaangamiza watoto wachanga wote wa kiume waliozaliwa ili kuunusuru
utawala wake.
Jambo la kushangaza ni jinsi Nabii Mussa (mtoto wa kiume)
alivyozaliwa mbali ndani ya kipindi hicho hicho na alivyokuja kulelewa
na kukulia ndani ya kasri ya Firauni mwenyewe.
Hii ni kwa sababu Nabii Mussa ni rehma kutoka kwa Mungu, hivyo
Firauni na wasaidizi wake hawakuwa na uwezo wa kumuangamiza. Nabii Mussa
alikuwa yuko chini ya nusura ya Mungu ambayo bila shaka inashinda nguvu
za wote ambao wangetamani kumdhuru.
Chini ya kivuli cha simulizi hiyo kutoka vitabu vitukufu, hebu
tugeukie historia ya kisiasa ya Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ambayo inaonesha kwamba hakuwahi kabisa
kutamani kuwa mwanasiasa wala kuwa kiongozi tokea utoto wake na ujana
wake, ijapokuwa kipaji cha uongozi kilionekana kwake mapema mno.
Mnamo mwaka 1975, akiwa kwenye kazi yake ya ualimu katika chuo cha
uwalimu Beit-el-Raas (sasa sehemu ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar,
SUZA) alipokea wito kutoka Ofisi ya Rais, wakati huo Mzee Aboud Jumbe
Mwinyi. Ikumbukwe kwamba wakati huo, ikiwa ndio kwanza ni muongo mmoja
baada ya Mapinduzi na Muungano, na pia mwaka mmoja tu baada ya kuuawa
kwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Karume, nchi ilikuwa kwenye
kipindi kigumu cha giza la kisiasa na kijamii. Kuitwa Ikulu hakukuwa na
maana njema sana, katika hali ya kawaida.
Akiwa ameshangazwa na wito huo, kwa vile hakuwahi kuwa na mawasiliano
wala mahusiano ya moja kwa moja na Ikulu, Maalim Seif aliitikia wito na
Rais Aboud Jumbe akamwambia Maalim Seif kwamba kuanzia siku hiyo
angelianza kufanya kazi katika ofisi yake kama katibu msaidizi maalum
(special assistant) wa Rais. Hivyo ndivo rehema ya Mungu ilivyomfikisha
Maalim Seif ikulu ya Zanzibar ndani ya zama za “sharia za kimapinduzi”
(revolutionary justice). Hakuota, hakuwaza, hakujisogeza wala hakuomba.
Mwaka 1977, Rais Jumbe aliamua kufanya mabadiliko ya baraza la
mapinduzi. Kupitia mabadiliko hayo alimtangaza Maalim Seif pamoja na
wenzake kuwa ni mawaziri wapya wateule wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, yeye Maalim Seif akiwa ni waziri wa elimu.
Kufuatia mabadiliko hayo serikali ya Jumbe ikapata nuru. Ilitoa
unafuu mkubwa kwa wananchi ukilinganisha na utawala wa Karume
uliotangulia. Baada ya Mapinduzi, wanafunzi hawakuweza kuendelea na
maomo kwa mujibu wauwezo wao wa kupasi mitihani bali ilikuwa kwa
kuzingatia makabila ya baba zao. Utaratibu uliotumika uliruhusu Waafrika
asilimia themanini (80%), Waarabu asilimia kumi na tano (15%), Wahindi
asilimia nne (4%) na Wakomoro asilimia moja (1%) kuendelea na masomo.
Baada ya kuwa waziri Maalim Seif alimshauri Jumbe kuubadilisha
utaratibu huo na badala yake wanafunzi wachaguliwe kuendelea na masomo
kwa uwezo wao wa kupasi mitihani na sio makabila yao. Jumbe na Seif
walifanikiwa kufanya hivyo, japokuwa walipambana na upinzani mkali wa
akina Seif Bakari na Natepe waliokuwa wakijifanya kuwa waasisi wa
Mapinduzi ya Zanzibar (Burgess 2009).
Sambamba na hili Maalim Seif alifanya jitihada ya kuwatafutia
wanafunzi wa Kizanzibari nafasi maalum za kujiunga na Chuo Kikuu cha
Dar-es-Salaam hata kama kiwango chao cha kufaulu kilikuwa chini
ukilinganisha na wanafunzi wa Tanzania Bara. Hoja ya Maalim Seif, kama
waziri wa elimu, ilikuwa ni kwamba Zanzibar inatoa kiwango kidogo cha
wanafunzi wanaokwenda katika elimu ya juu ukilinganisha na Tanzania Bara
na kwa kuzingatia kwamba elimu ya juu ni suala la Muungano.
Maalim Seif pia alimshauri Rais Jumbe nafasi za elimu ya juu baina ya
wanafunzi wa Pemba na Unguja iwe kwa uwiano wa asilimia 40 – Pemba na
asilimia 60 – Unguja. Kabla ya hapo kulikuwa na kiwango kikubwa cha
ubaguzi katika kuchagua wanafunzi wa kujiunga na vyuo vikuu baina ya
Unguja na Pemba kukiwa na upendeleo mkubwa kwa kisiwa cha Unguja, ili
kujenga chuki baina ya watu wa Unguja na Pemba. Hata hivyo, kutokana na
asilimia kubwa (60) ya nafasi za Unguja, wanafunzi kutoka Unguja
hawakuweza kujaza nafasi zao na hivyo nafasi hizo kukamilishwa na
wanafunzi kutoka Pemba (Burgess 2009).
Baada ya Rais Jumbe kulazimishwa kujiuzulu mwaka 1984, Rais mpya Ali
Hassan Mwinyi aliingia madarakani. Mwinyi alimteua Maalim Seif kuwa
waziri kiongozi wa serikali yake. Chini ya ushauri mzuri wa Maalim Seif,
Zanzibar ilizidi kupata neema katika utawala wa Mwinyi. Zanzibar
ilirudisha matumizi ya paspoti ili kudhibiti uingiaji holela wa watu na
hivyo basi mambo mengi ya udhia kama vile ujambazi, uhalifu, madawa ya
kulevya na maradhi ya kuambukiza yaliweza kudhibitiwa.
Upigaji watu mikwaju kiholela na kuwaweka ndani mambo ambayo yalikuwa
yakifanywa na Youth League katika awamu zilizotangulia yaliondoshwa.
Serikali mpya pia ikawashawishi vijana kusoma na kupatiwa nafasi za
masomo nje ya nchi. Halikadhalika vijana wasomi wakashawishiwa kuomba
nafasi za uongozi serikalini, bila ya kuzingatia makabila ya baba zao au
mahusiano ya baba zao na Uhizbu, Uafro au Ukomredi kama ilivyokuwa
kabla (Burgess 2009).
Isitoshe, Mwinyi na Maalim Seif walianzisha katiba mpya ya mwaka 1984
iliyoruhusu utawala wa sheria na mipaka ya madaraka kwa mihimili ya
dola ambayo iliandikwa na mwanasheria mkuu wa serikali wa wakati huo
ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria wa sasa, Abubakar Khamis Bakar.
Vile vile, chini ya uongozi wa viongozi hao wawili, ulianzishwa mfumo
mpya wa mahakama za kisheria na kufutilia mbali mahakama za wananchi
zilizoanzishwa na Sheikh Karume ambazo zilikuwa zikiendeshwa kinyume na
misingi ya sheria na haki. Haki za binaadamu katika katiba ya Zanzibar
zililingana zaidi na zile zilizomo kwenye Tangazo la Haki za Binaadamu
la Umoja wa Mataifa kuliko zile zilizokuwemo katika Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Kwa kweli serikali ya Mwinyi na Maalim Seif pamoja na kudumu kwa muda
mfupi sana, iliweza kuleta mabadiliko mengi. Mabadiliko mengine
yalikuwa ni pamoja na uhuru wa wananchi kutoa maoni yao. Mambo mengi
ambayo kwa njia moja au nyingine yalionekana kuwa ni ya kubana haki za
raia ambayo yalikuja mara baada ya Mapinduzi, yalibadilishwa katika
wakati huo. Vizuizi vingi vya kufaidi uhuru na haki za kiraia
viliondolewa. Vyombo vya habari vya Serikali vilitakiwa kuanzisha
vipindi maalum vya kuwapa nafasi wananchi kutoa maoni yao juu ya
uendeshaji wa nchi yao. Vipindi kama ‘Zanzibar ni Njema’ katika Radio ya
Zanzibar na ‘Jicho’ katika Televisheni ya Zanzibar (TVZ) vilivyotoa
fursa kwa Wazanzibari kutoa maoni yao kuhusu uendeshaji na utendaji wa
Serikali yao vilianzishwa katika kipindi hicho.
Lakini kubwa zaidi katika utawala wa Mwinyi na Maalim Seif ilikuwa ni
kuruhusiwa biashara huria, yaani ‘Trade Liberalisation’ hatua ambayo
ilipelekea ghafla kubadilika kwa hali za maisha ya watu na kuimarika kwa
uchumi na pato la taifa. Jambo hili lilimchukiza sana Nyerere kwani ni
kinyume na siasa yake ya ujamaa, lakini Mwinyi na Seif walimjibu Nyerere
kuwa “tunataka kuuimarisha ujamaa kwa kutumia mfumo huria”. Majibu hayo
yalimpoza Nyerere. Uhaba mkubwa wa chakula uliokuwepo kabla ulimalizika
na umasikini ukapungua makali yake kwa kiwango kikubwa. Wafanyabiashara
kutoka nchi za jirani kama Kenya na Tanzania Bara wakawa wanakuja
Zanzibar kutafuta bidhaa. Maisha ya watu yakaboreka na neema kutanda.
Hapo ndipo Mwinyi alipozaa msemo wake maarufu, Zanzibar ni njema atakae
naaje na baadaye msemo huu ukawa miongoni mwa maneno ya hekima.
Huu ni upande mmoja wa hadithi ya mafanikio katika safari ya kisiasa
ya Maalim Seif Sharif Hamad, ambayo ilidumu kwa kiasi ya muongo mmoja
ndani ya serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM). Lakini ukweli ni kwamba
safari hii haikuwa nyepesi sana na kulikuwa na vigingi vingi ndani yake.
Baada ya kifo cha Edward Sokoine, Nyerere alimteua Salim Ahmed Salim
kuwa waziri mkuu mpya. Hivyo basi Salim Ahmed Salim kwa upande wa
Jamhuri ya Muungano alitarajiwa sana kuwa mrithi wa kiti cha urais baada
ya kustaafu Nyerere.
Kwa upande wa Zanzibar nako Maalim Seif alitarajiwa sana kurithi kiti
cha urais baada ya Mwinyi kumaliza muda wake. Upepo huo wa kisiasa
haukuwa ukiwapungia vyema wanamapinduzi wa Zanzibar. Wanamapinduzi
hawakupendelea mabadiliko hayo kutokea na walifanya kila wawezalo
kuubalisha upepo huo wa kisiasa ili Salim Ahmed Salim kwa upande wa
Jamhuri ya Muungano na Maalim Seif kwa upande wa Zanzibar wasiweze kuwa
marais wanaofuatia.
Kosa la Maalim Seif lilikuwa ni Upemba wake, wakati Salim Ahmed
alikuwa na makosa matatu kwa mujibu wa kamusi la kihafidhina la
Zanzibar: Kosa la kwanza ni Uarabu, kosa la pili ni Upemba kama Maalim
Seif na kosa la tatu ni mwanachama wa zamani wa ZNP.
Ijapokuwa Nyerere
na Mwinyi walimuona Salim ndiye anayefaa zaidi kuwa raisi wa Jamhuri ya
muungano, lakini alipigwa vita na wanamapinduzi.
Nyerere kwa kuwatii wanamapinduzi akasitisha azma ya kumteua Salim na
badala yake akamteua Mwinyi kuwa rais mpya wa Jamhuri ya Muungano,
baada ya yeye kung’atuka mwaka 1985. Kwa upande wa Zanzibar majina
matatu ya Idri Abdul-wakil, Maalim Seif na Salmin Amour ndio
yaliojadiliwa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa (NEC) kuteua mmoja wao kuwa
rais mpya baada ya Mwinyi kupelekwa katika kiti cha urais wa Jamhuri ya
Muungano.
Mzee Idris alikuwa wa mwanzo kuomba jina lake liondoshwe kutokana na
uzee. Maalim Seif alikuwa kijana na alijulikana zaidi katika chama,
katika NEC na wananchi wa Unguja na Pemba, hivyo kulikuwa na kila aina
ya uwezekano wa kushinda kura nyingi kulinganisha na Idris Abdul-wakil.
NEC ilishangazwa sana kutangazwa ushindi wa Idris Abdulwakil. Hapana
shaka wanamapinduzi waliingilia kati suala hilo na kumfanya Nyerere
kuchakachua matokeo ya kura ili kumpinga Maalim Seif na kumpitisha
Idris.
Hapa ndipo wakati mgumu kwa siasa za Zanzibar baada ya kuzaliwa CCM
ulipoanza. Wazanzibari hawakufurahia Mwinyi kupelekwa Bara wala
hawakufurahishwa na uteuzi wa Idris na kuachwa Maalim Seif kwa kuwa Mzee
Idris hakujulikana vyema na Wazanzibari.
Takriban asilimia 80 ya wananchi wa Pemba na asilimia 63 ya wanachi
wa Mkoa wa Mjini Maghrib Unguja walimpigia Idris kura ya “hapana” na
hivyo kuzua mtafaruku mkubwa wa kisiasa. Baada ya wimbi la kukataliwa
Idris kutanda Zanzibar na hivyo siasa za CCM kuwa ngumu mno, Nyerere
alimshauri Idris kumteua Maalim Seif kuwa waziri kiongozi. Lakini hata
uteuzi huo wa waziri kiongozi haukuwafurahisha wanamapinduzi. Wao
walitaka waziri kiongozi awe Salmin Amour. Hivyo basi wakazidisha na
kuendeleza chuki na vita vyao dhidi ya Maalim Seif. Kila aina ya shutma
na visingizio wakavitoa ili kumpotezea umaarufu Maalim Seif ndani ya
chama na ndani ya serikali.
Moja ya shutma zilizowahi kutolewa ni kuwadharau, kuwavunjia heshima
na kuwadhalilisha wanamapinduzi, akina Seif Bakari. Shutma nyengine ni
kutaka kurejesha usultani Zanzibar.
Katika kipindi hichi kuliimarika
mahusiano ya kidiplomasia baina ya Zanzibar na Falme za Kiarabu.
Wanamapinduzi wakatumia fursa hiyo kutoa shutma kwamba Maalim Seif ana
mipango wa kurejesha utawala wa kisultani Zanzibar.
Katika ziara moja ya Maalim Seif nchini Oman katika jitihada zake za
kuiletea neema Zanzibar, Sultan Qaboos Busaid alisema wazi kwamba ana
kila sababu ya kuisaidia Zanzibar kwa kiwango kikubwa kwa kuwa ni wasomi
wa Kizanzibari ndio walioijenga Oman bila ya serikali ya Oman kuchangia
chochote katika elimu zao (Burgess 2009).
Maalim Seif na Qabous kupitia ziara hiyo waliahidiana mambo mengi ya
maendeleo kwa Zanzibar kama vile ujenzi wa viwanja vya ndege, kutanua
miradi ya maji na ujenzi wa barabara. Ahadi zote hizo zilibezwa,
kupuuzwa na kuzuiliwa utekelezaji wake na wanamapinduzi.
Tuhuma nyengine dhidi ya Maalim Seif ni kuwapendelea Wapemba. Maalim
Seif alituhumiwa kuwapendelea wapemba kwa ushauri wake wa mgao wa huduma
na mipango ya maendeleo kwa asilimia 60 kwa Unguja na 40 kwa Pemba.
Baada ya tuhuma kadhaa wa kadhaa kushindikana kutumika kama sababu na
visingizio vya kumtoa Maalim Seif katika wadhifa wake, ikatumika shutuma
ya kufanya upinzani ndani ya chama. Kupokonywa Maalim Seif uwaziri
kiongozi kukawadia na habari zikazagaa kila upande. Mrithi wa nafasi
Maalim Seif iliamuliwa kuwa Dk. Omar Ali Juma ili kuwatuliza Wapemba
baada ya kitendo cha kutolewa Maalim Seif.
Hata hivyo Dk. Omar aliposikia habari hizo haraka alifika kwa Maalim
Seif na kumwambia kwamba kuna habari kwamba unataka kutolewa katika
nafasi yako na baadae nafasi nipewe mimi, lakini mimi sitokubali nikijua
ni kuwagawa Wazanzibari na kujenga fitna. Tarehe 18 Januari 1988, Seif
Sharif akapokonywa wadhifa wa uwaziri kiongozi na Dk. Omar Ali Juma
akachaguliwa kuwa waziri kiongozi mpya, huku Dk. Omar akifurahia na wala
hakukataa kama alivyoahidi kabla.
Baada ya kitendo cha Maalim Seif kufukuzwa Zanzibar haikuwa shuwari.
Mengi yalizungumzwa, chama cha CCM kulaaniwa na kukataliwa, Nyerere
kuonekana ndiye anayewagawa Wazanzibari na Muungano kushutumiwa. Matukio
hayo yalimkera sana Nyerere na ndipo alipolazimika kumfukuza Maalim
Seif kabisa katika chama ili akose jukwaa la kufanyia siasa.
Kikao cha NEC kilichofuatia kilijadili tuhuma dhidi ya Maalim Seif na
wenzake saba tuhuma dhidi ya Seif na wote walitakiwa kujiuzulu nafasi
zao katika chama, ambapo baada ya wote kugoma kufanya hivyo Nyerere
akatamka mbele ya wajumbe wa NEC “kama mmegoma kujiuzulu kwa nafasi
niliyonayo nimekufukuzeni nyote katika chama”. Maalim Seif na wenzake
walifukuzwa katika chama siku ya mwezi 27 Ramadhani, kwa mujibu wa
Waislamu ni usiku wenye uwezekano mkubwa wa kupatikana lailatul-qadr.
Baada ya Maalim Seif kutolewa serikalini na kufukuzwa katika chama,
Wazanzibari wakaghadhibika mno. Watu makundi kwa makundi wakarudisha
kadi za chama na wengine kuzichana. Wengine walitengeneza sanamu za
Nyerere, hususan huko Pemba, na kuziharibu hadharani kuonyesha hasira
zao.
Mara tu Maalim Seif alipowasili kisiwani Pemba kutokea Dodoma makundi
kwa makundi ya watu walikuwa wakikusanyika wakiwa na hamu na shauku ya
kuzungumza nae. Nchi ilipooza na siasa za chama cha mapinduzi Zanzibar
zikakwama. Nyerere akahisi kwamba hata kuwa nje ya chama na serikali,
Maalim Seif ataendelea kuwa tishio kwa nchi na chama hivyo tuhuma kadhaa
zikabuniwa ili kumtia gerezani.
Serikali ilijaribu kwanza kutaka kumshtaki Maalim Seif kwa madai
kuiba nyaraka za serikali lakini baada ya kushindwa kuthibitisha
walimshtaki kwa kosa la kuitisha mikutano haramu. Seif alifungwa jela
kwa kipindi cha miezi 30 kuanzia mwezi wa Mei 1989 hadi mwezi wa Novemba
mwaka 1991.
Jitihada mbali mbali zikachukuliwa za kidiplomasia, Shirika la
Amnesty International na wasomi kudai Seif Sharif atolewe jela. Baada ya
hapo akatolewa pamoja na masharti na vikwazo vingi. Pamoja na yote hayo
bado Maalim Seif aliapa kutimiza ahadi yake ya kuwatetea Wazanzibari
kama alivyoahidi. Na hilo ndilo ambalo amekuwa akifanya tangu wakati huo
na hadi sasa. Mwalimu huyu ambaye hakuwahi kuwaza kama angekuwa
kiongozi siku moja. Hii ina maana uongozi haikuwa tunu yake wala ndoto
yake.
Tunaweza kusema uongozi kwa Maalim Seif ni rehma kwa Wazanzibari
kutoka kwa Mungu ili aje awakomboe kutokana na utawala uliojengewa
misingi imara kwa muda mrefu ya ubaguzi, chuki, farka, unyanyasaji,
ukandamizaji na maonevu kadhaa wa kadhaa.
Maalim Seif ameletwa kuja kuwaunganisha Wazanzibari waliogawanywa
tokea miaka ya 1950 na kuwafanya waonane kwamba wao ni ndugu wa damu.
Maalim Seif amekuja kuwaunganisha Wazanzibari kudai nchi yao iliyopotea
kupitia Muungano wa 1964 na kuirejesha ndani ya mamlaka yao ili waweze
kujiamulia mambo yao yote kijamii, kisiasa na kiuchumi na hivyo wapate
kuifaidi keki ya taifa lao tukufu.
Hivyo basi majemedari wa mapinduzi hawakuweza kuizuia rehema ya Mungu
na hivyo hawakuwa na nguvu za kuiepusha rehma ya Mungu isimpeleke
Maalim Seif ikulu ya serikali yenye misingi ya kimapinduzi. Viongozi
wote wengine wanazuka, wanakuwa maarufu na kupotea, lakini sivyo kwa
Maalim Seif ambae nyota yake inazidi kung’ara kila siku zikienda.
Jambo hili linawatahayarisha na kuwaiaibisha wale wote wenye mawazo
ya akina Borafya Silima na Balozi Seif Ali Iddi ambao wanaodhani ipo
siku wanaweza wakamtukana Maalim Seif akatukanika, wakamfedhehi
akafedheheka, wakamkejeli akakejelika na wakamdharau akadharaulika. Kwa
huyu haliwi, maana yeye ni mtu wa rehma kwa Wazanzibari na Zanzibar na
wajiandae kumpisha akikalie kiti cha Utawala wa Zanzibar na awaletee
wazanzibari maisha yenye utulivu wa nafsi sambamba na kiu yao ya muda
mrefu ya haki, usawa na neema.
Chanzo:
Mzalendo